ANGALIA LIVE NEWS

Friday, September 11, 2015

BENDERA YA PALESTINA KUPEPERUSHWA MAKAO MAKUU YA UMOJA WA MATAIFA

Ubao wa Matangazo ndani ya Ukumbi Mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, ukionyesha matokeo ya kura katika tukio la kihistoria kufanyika ambapo Baraza hilo limepitisha azimio linalotoa fursa kwa Palestina kupeperusha bendera yake. Nchi wanachama walipiga makofi kushangilia kupitishwa kwa azimio hilo, ambalo Israel imesema Palestina inatafuta umaarufu kwa njia za mkato badala ya kurejea kwenye meza ya mazugumzo.
Bendera ya Palestine itapepea nje ya Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, hii inafuatia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kupitisha azimio ambalo linatoa fursa kwa nchi ambazo si mwanachama kamili wa Umoja huo kupeperusha bendera yake Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa.

Na Mwandishi Maalum New York


Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, jana Alhamis, limepitisha Azimio ambalo kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa Umoja huo, litaruhusu nchi ambazo siyo mwanachama kamili kupeperusha bendera yake katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa.

Kupitishwa kwa azimio hilo ambalo limepigiwa kura za ndiyo 119 za hapana nane na zisizofungamana na upande wowote 45 kunaipa fursa Palestina kupeperusha bendera yake nje ya Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa.

Mara baada ya matokeo ya kura kutangazwa rasmi, Wajumbe wa Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa walipiga makofi kama ishara ya kufurahia kupitishwa kura nyingi azimio hilo.

Palestina kama ilivyo kwa Vatican inahadhi ya Nchi Mwangalizi isiyo Mwanachama wa Umoja wa Mataifa (Non -Member Observer States)

Kwa mujibu wa Azimio hilo nambaA/69/L.87 linaloelezwa kuwa ni la kihistoria, linamtaka Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhakikisha kwamba Bendera ya Palestina inapeperushwa ndani ya siku 20 ( septemba 30)wakati wa Mkutano wa Baraza Kuu la 70 la Umoja wa Mataifa.

Akiwasilisha azimio hilo mbele ya wajumbe, Mwakilishi wa Kudumu wa Iraq na ambaye ni mwenyekiti wa kundi la nchi za kiarabu alisema kupeperushwa kwa bendera ya Palestina ni kielelezo cha utekelezaji wa matakwa yaliyomo ndani ya Katiba ya Umoja wa Mataifa ya kwamba, nchi zote na watu wake wako sawa na wana haki sawa.

Hata hiyo si mataifa yote yaliyoridhika ya uamuzi huo, kwa kile ambacho wengine wameeleza kuwa ni ukiukwaji wa kanuni za Umoja wa Mataifa ambazo zinaeleza wazi wazi kwamba bendera zinazopashwa kupeperushwa katika Umoja wa Mataifa ni zile tu za nchi ambazo ni wanachama kamili.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Kudumu wa Israel katika Umoja wa Mataifa, yeye alisema kwamba kupeperushwa kwa bendera ya Paletina katika Umoja wa Mataifa, hakubadilishi hali halisi na mazingira ya sintofahamu yanayoendelea kati yake na Palestina.

Akizungumza kwa hisia kali huku akizilaumu nchi ambazo zimeunga mkono azimio hilo, Mwakilishi huyo wa Israel, ameeleza kwamba Palestina inatakiwa kufanya maamuzi magumu yakiwamo ya kurejea katika meza ya mazungumo badala ya kutafuta njia za mkato zikiwamo hizo za kupeperusha bendera katika Umoja wa Mataifa.

Akasema yeye kama mwakilishi wa Israel picha ambayo anaamini ndiyo inayostahili kuwa maarufu ni ile ya viongozi wa Israel na Palestine watakapokuwa kwa pamoja wanapandisha bendera ya matumaini inayoonesha mataifa hayo mawili yakiishi kwa pamoja kwa Amani na usalama.

Hoja ya kutaka Israel na Palestina kurejea kwenye mazugungumo ya kutafuta ufumbuzi wa kudumu baina ya pande hizo mbili imeungwa mkono na wazungumzaji wengi wakiwamo wale waliopiga waliopiga kura ya hapana kama vile Marekani .

Kwa upande wa wale waliounga mkono azimio hilo, walieleza kwamba nchi inapo peperusha bendera yake hata ni kielelezo cha ufahari, utambulisho na uwepo wake na kwa sababu hiyo Palestine ilikuwa na kila sababu ya kupeperusha bendera yake ambayo kwayo haibadilishi hadhi yake ya kuwa nchi mwangalizi, lakini ikiandika historia nyingine.

Mwakilishi wa Palestina akiwa na furaha tele amezishukuru nchi zote ambazo zimeunga mkono azimio hilo.

Pamoja na kupitishwa kwa Azimio hilo linalotoa fursa kwa nchi ambazo si wanachama kamili kupeperusha bendera, Wajumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa pia walipitisha kwa kupiga kura azimio linalotaka kuangaliwa kwa misingi ya utaratibu wa marekebisho ya ulipaji wa madeni kwa nchi zinazodaiwa.

Azimio hilo namba A/69/L.84 lililowasilishwa na Mwenyekiti wa Kundi la Nchi 77 na China ( G77&China) lilipita kuwa kura 136 za ndiyo, sita za hapa na 41 zisizofungamana na upande wowote

2 comments:

Anonymous said...

Bado bendera ya Zanzibar kupepea un
Chini ya Lowassa

Anonymous said...

Tunajua hoja yenu ni kutaka kuvunja muungano. Bahati mbaya hamtafanikiwa.