Thursday, September 10, 2015

KWA NINI MWANAUME WA ZAMANI AKUVUNJIE NDOA?

BILA shaka yoyote kwamba mmeamka na afya njema na mnaendelea vizuri sana na ujenzi wa taifa, hasa kipindi hiki cha siasa kushika hatamu kuelekea uchaguzi mkuu, mwezi ujao. Mimi kura yangu ni siri yangu.

Leo mada yetu ni kwa nini mwanaume wako wa zamani awe sababu ya wewe kuvunja ndoa yako? Mada ambayo imekuja kutokana na ujumbe nilioandikiwa na msomaji wangu mmoja nami kujikuta katika msukumo wa kuiandika.

Simu ndiyo iliyotibua mambo

“Mimi ni mwanaume ambaye nimejaliwa kuoa mke na kupata naye mtoto mmoja. Siku za hivi karibuni mke wangu alianzisha tabia ya kupenda sana kutumia simu hasa kwa kuchati.

“Awali, sikuona kuwa ni tatizo kwani alikuwa akinifanyia kila kitu. Nikaona mambo yanakwenda sawasawa.

“Lakini siku moja tukiwa sebuleni muda mfupi nikiwa nimerudi kutoka kazini, alinitengea chakula, sasa nikiwa nakula, yeye akiwa amekaa pembeni anachati na simu baada ya muda simu yake iliita akapokea kisha akakata nilipatwa na mshtuko kidogo nikahisi kuna kitu. Nikamuuliza huyo mtu ni nani? Akakataa katakata kuniambia.

“Niliamua kuichukua kwa nguvu simu yake ndipo nikakuta jina la mtu aliyepiga limeseviwa kwa jina la Ayubu. Simu hiyo nikampa mdogo wangu wa kike aongee na huyo Ayubu na kumwelekeza jinsi atakavyoongea kwa mahaba ili asishtuke kuwa si mke wangu.

Alivyopokea tu Ayubu akamuuliza mdogo wangu mbona ulikata simu? Kisha akaongeza kusema kuwa, alimpigia ili kujua kama ile safari bado ipo ili atangulie akachukue chumba yeye angemkuta.

“Mdogo wangu akiigiza yeye ndiye mke wangu, alimwambia kuwa safari ipo palepale na wakapanga muda wa kukutana.

“Baada ya kukata simu, nilimwa-mbia mke wangu afungashe aondoke moja kwa moja asirudi kwani nilipombana aliniambia yule alikuwa ni mwanaume wake wa zamani.”

Huyo alikuwa ni mume wa mtu ambaye alinipigia na kunielezea hayo, nikaona niwaase akina mama wanaoendekeza wanaume wao wa zamani na kujikuta wanavunja ndoa zao kizembe.

ALIKUWA WAPI ASIKUOE?

Kama mlipendana sana kwa nini hukuolewa naye mpaka mkaachana ukaenda kuolewa na huyo unayetumia muda mwingi kumsaliti?

Huoni kama huyo hakupendi ana nia ya kukuharibia maisha tu. Unampa nafasi ya nini wakati ulishakwenda kwa mwingine?

UKIACHIKA KIMBILIA KWAKE UONE ‘MZIKI’ WAKE

Kama yeye atashiriki kukuvunjia ndoa yako pale utakapoachika kimbilia kwake uone kama atakupokea. Anakupenda kwa wakati huo kwa sababu anajua hata kugharamia chochote.

WENGINE HUWATISHIA NYAU WAUME ZAO

Wanawake wengine hupendelea kuwatishia nyau wanaume zao pale wanapogombana kidogo. Utasikia mtu anamwambia mumewe; ‘namkumbuka x wangu, yeye yuko tofauti na wewe.’ Au; ‘bora x alikuwa ananifanyia hivi.’

Wana-sahau kuwa, hilo ni tatizo kubwa sana ambalo halitakiwi kabisa kwenye ndoa na hata uhusiano usiokuwa wa ndoa.

Kama x wako ulimuona wa maana sana basi ujue yeye hakukuona wa maana ndiyo maana alikuchezea weee…mwisho wa siku akatokea aliyekupenda akakuoa. Kwanza tambua hiyo ni aibu kwako.

Sasa katika ukoo wetu, mwanamke akionekana anarudia uhusiano na bwana wake wa zamani wakati yupo kwenye ndoa, ni aibu kwake na kwa wazazi wake. Kwani watu wanajiuliza kama alimpenda kwa nini asimuoe?

USHAURI WANGU

Nakushauri mwanamke mwenzangu ukishapata mume au mwenza tofauti na yule wa awali, fanya kama amekufa ili kulinda ndoa yako.

GPL

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake