KILA jambo la nafsiri yake. Maadhimisho ya Miaka Kumi ya uwepo wa Michuziblog hayawezi kupita bila kutafutiwa tafsiri yake.
Kwanza kabisa, kwa niaba ya wajumbe wangu wote, nichukue fursa hii kumpa pongezi za dhati ndugu yangu Kaka Muhidin Issa Michuzi kwa mafanikio makubwa aliyoyapata na pia mchango wake mkubwa alioutoa kwa Wanablogu wengine, nikiwamo mimi.
Muhidin Michuzi ataingia kwenye vitabu vya kumbukumbu ya historia kama Mtanzania aliyekuwa mstari wa mbele katika kufanya mapinduzi ya mitandao ya kijamii hapa nchini hususan eneo la blogu. Michuzi amechangia sana katika kuwafanya Wanablogu na blogu kwa ujumla wake, kuwa ni sehemu ya vyombo vya habari vinavyopaswa kutiliwa maanani katika kutoa mchango wa maendeleo ya nchi.
Bila shaka kuna waliomfahamu Muhidin Michuzi kupitia blogu yake. Nina bahati ya kumfahamu Michuzi kabla ya ulimwengu wa mitandao ya kijamii.
Kwangu mimi, na kwa wengi, Muhidin Issa Michuzi ni mbunifu na mwenye bidii na nidhamu ya kuifanya kazi yake. Ni mtu wa watu.
Nitasimulia hapa kwa mara ya kwanza, kuwa mwanzoni mwa miaka ya 90, Marehemu kaka yangu, Grey Mjengwa, alifiwa na binti yake wa mwaka mmoja tu, aliitwa Rahma. Shughuli ya msiba ilikuwa pale nyumbani kwetu Kinondoni Biafra.
Wakati huo hakukuwa na simu za mikononi wala mitandao ya kijamii. Lakini, nilifarijika sana, nilipomuona Muhidin Issa Michuzi akiwa mmoja wa waliokuja msibani. Enzi hizo mitandao ya kijamii ilikuwa midomo ya watu, bila shaka habari za msiba ule Michuzi alizisikia kutoka kwa watu. Si rahisi kuyasikia ya kijamii kama si mtu wa watu.
Ndugu zangu,
Mara ya kwanza kulifahamu jina Muhidin Issa Michuzi ilikuwa ni pale Tambaza Sekondari, ni mwaka 1986, nilikuwa Kidato cha Tatu. Tayari wakati huo nilikuwa na kijarida changu ' Tambaza News' nilichokuwa nikikiandika kwa mkono kwenye A4 na kubandika kwenye ubao wa matangazo. Nilikuwa na wasomaji wengu akiwamo Makamu Mkuu wa Shule, Mr. Mwaipopo.
Jumamosi moja niliangalia kwenye gazeti la Mfanyakazi nikakutana na picha iliyopigwa Mtaa wa Msimbazi ikionyesha ghorofa lililoporomoka kutokana na kukosa viwango. Na ni nani basi aliyekuwa wa kwanza kufika hapo kurekodi tukio hilo?
Ni Muhidin Issa Michuzi!
Nami nilikuwa mpenzi sana wa kupiga picha tangu utotoni. Nikajiuliza ni nani huyu Muhidin Michuzi? Miaka mitano baadae nikakutana nae pale Daily News.
Na nini ni special kwa Michuzi?
Michuzi ana 'Jicho la picha'. Kupiga picha ni sanaa. Mpiga picha mzuri ni yule mwenye ' Jicho la Picha'.
Vinginevyo, unaweza ukabeba kamera yako na kutembea kutoka Kinondoni hadi Kariakoo usione hata picha moja. Na ukijilazimisha kupiga basi itakuwa unapiga 'picha bubu'- Picha zisizoeleza chochote.
" HAPPY BIRTHDAY MICHUZIBLOG!"
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake