Thursday, September 10, 2015

TANZANIA YAHIMIZA USHIRIKIANO KATIKAKUWASAIDIA WAKIMBIZI

Balozi Tuvako Manongi akizungumza wakati wa Majadiliano ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu dhana ya kuwalinda raia (R2P) majadiliano yaliyojielekeza katika kutathimini mafanikio na changamoto za utekelezi wa dhana hiyo ikiwa ni miaka kumi tangu kuasisiwa kwake.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, akizungumza wakati wa Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu dhana ya wajibu wa kuwalinda raia, ambapo alisema licha ya kuasisiwa kwa dhana hiyo dunia bado imeendelea kushuhudia maisha ya watu wasiokuwa na hatia yakiendelea kupotea kwa sababu tu Jumuiya ya Kimataifa inashindwa kutumiza wajibu wake kwa wakati.
Wakimbizi katika kambi moja nchini Tanzania, ambao jana jumanne akizungumza katika Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika UN Balozi Tuvako Manongi amesema kutoka na wimbi kubwa linaloendelea la wakimbizi kukimbilia mataifa mengine kutafuta usalama wao. Jumuiya ya kimataifa haina budi kushirikiana na bila kubagua katika kuwalinda na utoaji wa huduma na misaada ya kibinadamu kwa wakimbizi

Na MwandishiMaalum, New York
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imetoa wito kwa Jumuiya ya Kimataifa wakushirikiana katika wajibu wa kuwalinda na kuwapatia misaada ya kibinadamu, wakimbizi wanaokimbia machafuko, vita na migogoro katika nchi zao.
Wito huo umetolewa siku ya jumanne na Balozi Tuvako Manongi,Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, wakati Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, lilipokutana kwa majadiliano ya siku moja kuhusu utekelezaji wa dhana juu ya wajibu wa kulinda raia (R2P) mafanikio na changamoto zake.

Dhana ya wajibu wa kuwalinda raia dhidi ya mauaji ya kimbari, uhalifu wa kivita, mauaji ya kikabila na uhalifu dhidi ya binadamu ilianzishwa mwaka 2005 wakati wa mkutano wa Kimataifa uliofanyika mwaka huu, ambapo viongozi wakuu wa nchi na serikali walikubaliana kwamba wajibu wa kwanza wa kuwalinda raia dhidi ya udhalimu wa aina yoyote ile ni wa serikali yenyewe husika.

Kupitia dhana hiyo ya R2P viongozi hao walikubaliana pia kwamba ikiwa itadhihirika kuwa serikali ya nchi husika inashindwa kuwalinda raia wake kwa sababu zozote zile basi jumuiya ya kimataifa inapashwa kuchukua maamuzi ya kuwalinda raia hao.

Akichangia majadiliano hayo ambayo yaliyofunguliwa na Katibu Mkuu Ban Ki moon, Katika Balozi Manongi, ameeleza kwamba, dhana ya kuwalinda raia inapashwa pia kuhusisha tatizo la wakimbizi wanaokimbia nchi zao kwa sababu mbalimbali na kwenda kutafuta usalama katika mataifa mengine.

Akasema, Tanzania ambayo kwa miaka mingi imekuwa ikiwapokea na kuwahifadhi wakimbizi kutoka mataifa mbalimbali, kwa uzoefu wake inatambua dhahiri kuwa ushirikiano wa kimataifa ni muhimu sana na kwamba Jumuiya ya kimataifa inatakiwa kuuboresha na kuimarisha ushirikiano huo.

“Tatizo linaloendelea hivi sasa la wimbi kubwa la wakimbizi wanaokimbilia Ulaya wakitokea Syria, Libya na kwingineko, ni changamoto yetu sote, ni changamoto ya kimataifa, wakimbizi hawa na wengineo wanapashwa kulindwa na kusaidiwa kwa mujibu wa sheria za kimataifa zikiwamo sheria za haki za binadamu ”. Akasema Balozi Manongi.

“Tanzania kama nchi ambayo kwa miaka mingi imekuwa ikiwapokea na kuwahifadhi wakimbizi,inatambua kwamba ushirikiano wa kimataifa ni muhimu katika kuwasaidia wakimbizi.
Ni Muhimu basi tuimarisha na kuboresha misingi ya kusaidia na katika kulibeba jukumu hili” akasema Balozi Manongi Akizungumzia Zaidi kuhusu dhana ya wajibu wa kuwalinda raia, dhana ambayo tafsiri yake bado haijapokelewa vema miongoni mwa nchi wanachama Balozi amesema.

Tanzania inaamini kwamba kanuni za sheria za kimataifa zikiwamo zile za uhusianona ushirikiano baina ya nchi marafiki ni muhimu katika kuielewa, kutafsiri na utekelezaji wa dhana ya wajibu wa kuwalinda raia kutokana ukweli kwamba ni dhana ambayo haijitegemei.

Aidha Mwakilishi huyo wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, amebainisha kuwa, ingawa wajibu wa kwanza wa utekelezaji wa wajibu wa kuwalinda raia ni wa Nchi au Serikali husika, lakini nchi hiyo inaposhindwa kutimiza wajibu wake huo, basi Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kusaidia kwa kuiwezesha nchi hiyo kutekeleza wajibu huo.

Awali Akifungua majadiliano hayo Katibu Mkuu, Ban Ki Moon, asema, ni jambo la kusikitisha sana kwamba miaka kumi tangu kuasisiwa kwa dhana hiyo ya R2P bado watu wengi wakiwamo watoto wameendelea kupoteza maisha kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo za vita na migogoro.

“ Ninasitiza kueleza kwamba miaka kumi tangu kuanzishwa kwa dhana hii, dunia imeendelea kushuhudi matukio ya watu kupoteza maisha yao kwa sababu tumeshindwa kuwalinda.

Tunaendelea kushuhudia watu wakipoteza maisha huko Sudan ya Kusini, Sudan katika jimbo la Darfur, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Libya, Syria, Yemen, Mali, Jamhuri ya Afrika ya Kati na kwingineko”.akaeleza Ban Ki Moon.

Na kwa sababu hiyo Katibu Mkuu amependekeza mambo kadhaa ambayo anaamini yatasaidia kuongeza kasi ya utekelezaji wa dhana hii.

Baadhi ya Mambo hayo ni, nchi wanachama na hasa Baraza Kuu la Usalama, kuwa tayari kwa kuweka mazingira ya kisiasa ya kuzuia na kuitikia pale inapojidhirisha kuwapo kwa dalili za kutokea kwa uhalifu, utoaji wa tahadhari na kuchukua hatua.

Wazungumzaji wengine katika mkutano huo wamelinyoshea kidole Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa na hasa katika matumizi ya kura ya Veto yanayofanywa na wajumbe wa kudumu wa baraza hilo.

Baadhi ya wachangiaji wameeleza kwamba ili kanuni ya wajibu wa kuwalinda raia iweze kutekelezwa kwa haraka na kwa wakati, wajumbe wa watano wa kudumu wa Baraza Kuu la Usalama, wanapaswa kuonyesha utashi wa kisiasa na kuacha kutumia kura hiyo kwa maslahi binafsi.

Wajumbe wengine, licha ya kuelezea nchi zao kutoridhishwa kwa tafsiri ya dhana ya wajibu wa kuwalinda raia lakini pia wamesema hawakubaliani na matumzi ya nguvu kuingilia nchi nyingine kwa na hata kuwaondoa madarakani viongozi kwa kisingizio utekelezaji wa dhana ya wajibu wa kuwalinda raia.

Wajumbe wengine wameeleza wazi wazi kupinga kwao hoja ya kutaka kuingizwa kwa dhana hiyo ya R2P katika ajenda za Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Sababu zikiwa ni pamoja na kuwa dhana hiyo bado inautata na inahitaji kuendelea kujadiliwa miongoni mwa nchi wanachama.

1 comment:

  1. Oops kuwasadia wakimbizi au ili wapige Jura kwa CCM mwaka huu
    Manongi mwenyewe kachina na kuchoka kwenye hii picha
    Oops ndo balozi huyu
    Uliza mtanzania wa kijijini yukoje kwenye serikali ya CCM
    Tumechoka tumechoka Lowassa tuokowe

    ReplyDelete

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake