Uteuzi huo wa Tanzania kuwa miongoni nchi za mfano kutimiza malengo hayo, umefanyika juzi baada ya malengo hayo kujadiliwa na kukubaliwa na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa (UN), ambayo ndiyo msimamizi mkuu wa malengo hayo muhimu katika kukabiliana na changamoto kuu duniani. Mbali na Tanzania, nchi nyingine katika kundi hilo la nchi nane za mfano duniani, ni pamoja na nchi zilizoendelea za Ujerumani, Sweden na Brazil pamoja na Liberia, Tunisia, Colombia na Timor ya Mashariki.
Uzinduzi Utekelezaji wa malengo hayo, umezinduliwa usiku wa juzi katika hafla maalumu iliyoandaliwa na Waziri Mkuu wa Sweden, Stefan Lofven kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa (UN) mjini New York, Marekani. Katika hafla hiyo, viongozi wa nchi hizo nane, walionesha na kuthibitisha dhamira yao ya kuongoza mapambano ya kisiasa ya kutekeleza malengo hayo kwa kutia saini azimio maalumu, ambako kila nchi imejithibitisha dhamira yake katika mapambano hayo.
Viongozi ambao wametia saini azimio hilo ni Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete; Waziri Mkuu wa Sweden Lofven; Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel; Rais wa Brazil, Dilma Rousseff; na Rais wa Jamhuri ya Liberia, Mama Ellen Johnson Sirleaf. Wengine ni Rais wa Colombia, Juan Manuel Santos; Rais wa Timor Mashariki, Taur Matan Rauk na Waziri Mkuu wa Tunisia, Habib Essid ambaye alimwakilisha Rais wake.
*Kikwete
Akizungumza katika hafla hiyo, Rais Kikwete amesema kuwa utekelezaji wa malengo hayo umeonesha dhahiri kuwa masuala makuu yanayoongoza mafanikio ya shughuli hiyo, ni upatikanaji wa fedha za kutosha kutekeleza malengo hayo na kuwepo kwa mfumo thabiti wa kufuatia utekelezaji.
“Na haya mawili, kwa pamoja, yalitegemea sana utashi wa kisiasa wa utekelezaji wa malengo hayo… nimesimama hapa kukuambia yale ambayo nilikuambia nchini Sweden tulipokutana kiasi cha miezi mitatu iliyopita, kwamba naunga mkono wazo la kuanzishwa kwa kundi la nchi hizi nane.
“Niko tayari kutoa utumishi wangu kwa kazi hii sasa na katika siku zijazo, baada ya kustaafu kutoka kwenye uongozi wa nchi yangu,” alisema Rais Kikwete. *Malengo umasikini Lengo la kwanza miongoni mwa malengo hayo endelevu limetajwa kuwa ni kufuta umasikini wa aina zote ambao unaendana na kukuza uchumi na pato la wananchi.
Kwa sasa Tanzania ina rekodi ya miaka kumi ya ukuaji wa uchumi, ambapo Pato la Taifa (NNP) limekua kwa wastani wa takriban asilimia saba na kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa mataifa 10 ya Afrika na 20 duniani ambayo uchumi wake unakua kwa kasi kubwa.
Aidha Pato Ghafi la Taifa (GNP), liko katika rekodi ya kuongezeka zaidi ya mara tatu kutoka Sh trilioni 14.1 mwaka 2005 hadi kufikia Sh trilioni 79.4 mwaka 2014 na kufanya pato la wastani la Mtanzania kuongezeka kutoka Sh 441,030 kwa mwaka 2005 hadi Sh milioni 1.7 mwaka 2014.
*Njaa, kilimo
Lengo la pili ni kufuta njaa, kuwa na uhakika wa kujitosheleza kwa chakula, kuboresha lishe na kujenga kilimo endelevu. Kwa sasa Tanzania katika miaka kumi iliyopita, bajeti ya sekta ya kilimo iliongezwa kutoka Sh bilioni 233.3 mwaka 2005/06 hadi Sh trilioni 1.08 katika Bajeti ya 2014/15.
Hali iliyowezesha fedha za ruzuku ya mbolea na pembejeo kuongezeka kutoka Sh bilioni 7.5 mwaka 2005/06 hadi Sh bilioni 299.3 mwaka 2013/14. Jitihada hizo zimesaidia uzalishaji wa mazao ya chakula kuongezeka kutoka tani milioni 9.66 mwaka 2005 hadi tani milioni 16.01 mwaka 2014, na kuwezesha Taifa kujitosheleza kwa chakula kwa asilimia 125 mwaka 2014 ikilinganishwa na asilimia 95 mwaka 2005.
Afya
Lengo la tatu ni kuhakikisha huduma bora za afya zinatolewa kwa wote na kwa watu wa umri mbalimbali, lengo ambalo pia limekuwa likifanyiwa kazi na Serikali. Kwa sasa juhudi kubwa zimefanyika katika kusogeza huduma ya afya karibu na wanapoishi watu, kwa kujenga vituo vya kutoa huduma ya afya vipya na kuimarisha vilivyopo. Kati ya mwaka 2005 na 2014 vituo vya kutolea huduma za afya 2,175 vilijengwa na kati ya hivyo, hospitali zilikuwa 19, vituo vya afya 168 na zahanati 1,883.
Aidha Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, hospitali za rufaa za Kanda, mikoa na wilaya, zilipatiwa vifaa vya tiba na uchunguzi vikiwemo vifaa vya MRI, CT Scan, X ray, Ultra Sounds na maabara. Serikali pia imejenga maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii ambayo ndiyo Maabara ya Kimataifa ya Rufaa kwa nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya kusini mwa Afrika (SADC).
Elimu Lengo la nne ni kuhakikisha kwamba kuna kuwa na huduma bora ya elimu inayotolewa kwa usawa na kuhakikisha fursa za kujipatia elimu wakati wote wa maisha ya binadamu zinaendelea kuwepo.
Katika sekta hiyo, jitihada zimekuwa zikifanyika ambapo bajeti ya elimu katika mwaka huu wa fedha imekuwa kubwa kuliko ya sekta zingine, inayofikia Sh trilioni 3.4 kutoka Sh bilioni 600 iliyokuwepo mwaka 2005.
Aidha Serikali kwa kushirikiana na wananchi ilianza kujenga shule za sekondari za kata, ambapo wananchi walihamasishwa, wakahamasika na wakajenga shule nyingi za sekondari, ambapo sasa nchi imejiandaa kutoa elimu ya msingi mpaka kidato cha nne bure kuanzia mwakani.
Kutokana na uhamasishaji huo, kwa sasa Tanzania ina wanafunzi 1,800,000 wanaosoma sekondari na katika Afrika Mashariki, imeshaipita Uganda yenye wanafunzi 1,700,000 wanaosoma elimu ya sekondari, lakini imezidiwa na Kenya ambayo ina wanafunzi 2,100,000.
Kwa upande wa elimu ya juu, vyuo vikuu vimeongezeka kutoka 26 mwaka 2005 hadi kufikia 52 na idadi ya wanafunzi walio katika vyuo vikuu ilitoka 40,719 hadi kufikia 200,956.
Malengo mengine ni pamoja na kujenga usawa na kuwezesha wanawake na wasichana, kuhakikisha kunakuwa na upatikanaji wa maji na huduma za maji taka. Mengine ni kuhakikisha Taifa linakuwa na huduma za bei nafuu za nishati, ziwe za uhakika, kisasa na endelevu na kujenga uchumi unaokuwa, unatoa ajira bora kwa wote.
Serikali katika makubaliano hayo aliyosaini Rais Kikwete, itatakiwa kujenga miundombinu mtambuka na viwanda endelevu na kuboresha masuala ya ubunifu. Pia lipo lengo la kimataifa, ambalo nchi zitatakiwa kupunguza tofauti zao za kiuchumi, kijamii na kisiasa kati ya nchi na nchi, lakini nchi zenyewe zimetakiwa kupunguza tofauti hizo kwa wananchi wao.
Miji nayo imetakiwa iwe na makazi bora kwa wote, yawe salama, mtambuka na endelevu pamoja na kuchukua hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
HABARI LEO
No comments:
Post a Comment