ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, September 15, 2015

Ukweli elimu bure ya Lowassa huu hapa.

Ahadi aliyoitoa mgombea urais kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema), ya kutoa elimu ya Chuo Kikuu bure inaweza kugharimu Taifa kiasi cha Sh. trilioni 1.35($675millioni) kwa mwaka, Nipashe limebaini.

Lowassa katika uzinduzi wake wa kampeni alitoa ahadi ya kutoa elimu bure kuanzia chekechea mpaka chuo kikuu iwapo atachaguliwa kuwa rais wa awamu ya tano-hali iliyozua ubishi kutoka kwa Chama Cha Mapinduzi.

Baadhi ya vigogo wa CCM wanadai ni ndoto kutoa elimu bure kwa kuzingatia hali ya uchumi wa nchi, huku kambi ya Lowassa ikisisitiza kwamba jambo hilo linawezekana endapo raslimali za taifa zitatumika ipasavyo.

Gazeti hili limefanya uchambuzi kwa kutumia takwimu mbalimbali zikiwamo zile za serikali ili kuweza kubaini gharama za elimu bure, lakini kwa kuzingatia elimu ya chuo kikuu tu.

Kwa mujibu wa uchambuzi huo, kwa mwaka 2016 pekee, endapo mathalan kutakuwa na wanafunzi 300,000 katika vyuo vikuu vya umma na binafsi, gharama zinaweza kuwa Sh. trilioni 1.35 kwa mwaka.

Gharama hizi kwa mwaka ni sawa na asilimia 6 ya bajeti ya Serikali kwa kuzingatia bajeti ya mwaka 2015/16 ambayo ni Sh. 22.495 trillion kama ilivyowasilishwa na kupitishwa na bunge Juni mwaka huu mjini Dodoma.

Gazeti hili limetumia wastani wa Sh. milioni 4.5 kwa kila mwanafunzi wa chuo kikuu kwa mwaka kwa ajili ya ada na matumizi mengineyo.

Hata hivyo, zipo baadhi ya shahada kama uhandisi na udaktari ambazo wanafunzi hupewa wastani wa milioni 6 kwa mwaka kama gharama ya masomo na matumizi mengineyo.

Kwa maana nyingine, gharama yote ya kuwasomesha wanafunzi bure katika vyuo vikuu Tanzania kwa mwaka kama alivyoahidi Lowassa ni sawa na thamani ya kununua mashangingi (Toyota Land Cruiser VX-V8) 3,375.

Ghari jipya aina ya Land Cruiser VX-V8 maarufu kama shangingi hugharimu kiasi cha dola za Marekani 200,000(Sh. milion 440) kulingana na takwimu ambazo Nipashe imezikusanya toka vyanzo mbali mbali.

Kwa lugha rahisi kwa mujibu wa uchambuzi wa Nipashe, Shangingi moja huweza kugharimia masomo kwa wanafunzi 97 kwa mwaka kusoma shahada ya kwanza chuo kikuu.

Gharama hizi pia ni sawa na asilimia 11 ya makusanyo yote yaliyofanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika kipindi cha mwaka wa fedha 2013/14.

Kwa mujibu wa uchambuzi wa Nipashe, gharama hizi ni sawa na asilimia 75 ya misamaha yote ya kodi iliyotolewa nchini katika mwaka wa fedha wa 2013/14.

Kwa mwaka kulingana na ripoti ya kamati ya Bajeti ya Bunge misamaha ya kodi nchini ilifikia kiwango cha juu cha Sh. trillion 1.8 kwa mwaka wa fedha wa 2013/14, sawa na asilimia 4.3 ya pato la taifa—zaidi ya kiwango kinachokubalika kitaalamu cha asilimia moja tu.

Ingawa Nipashe haikuweza kuipata idadi kamili ya magari ya shangingi yanayomilikiwa na serikali, uzoefu unaonyesha kuwa aina hiyo ya magari inatumiwa na watumishi wakubwa wa serikali.
Watumishi hawa ni wa kuanzia hadhi ya wakurugenzi, makamishina, makatibu wakuu, naibu mawaziri, mawaziri, majaji na wakurugenzi wote wa mashirika ya umma.

Pia magari hayo yanatumika na wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama, kama vile jeshini, Polisi, Magereza, Takukuru na hata kwenye idara za serikali zinazojitegemea.

Waziri Mkuu Mizengo Pinda alipoingia madarakani alitangaza kuchukua hatua madhubuti za kupunguza matumizi ya magari hayo serikalini, lakini juhudi zake hazikuzaa matunda.

Matumizi ya magari hayo yanatajwa kuwa ni moja ya eneo ambalo serikali inatumia fedha nyingi za walipa kodi, huku mahitaji mengine ya msingi ya wananchi kama elimu, afya na maji yakikosa fedha za kuleta matokeo makubwa chanya kila mwaka wa fedha.
CHANZO: NIPASHE

2 comments:

Anonymous said...

Lowassa alivyokuwa mwanafunzi Chuo Kikuu na ambacho kilikuwa ni chuo pekee tu nchini kwa wakati huo, idadi ya wanafunzi ambao walikuwa wanasoma kwenye chuo hicho na pia kwenye vyuo vingine nje ya nchi chini ya dhamana ya serikali walikuwa 3,000 tu kwa mwaka. Ndiyo maana wakati huo serikali ya Mwalimu iliweza kugharamia mafunzo ya hao wanafunzi wachache waliobahatika kwenda chuo kikuu. Leo tunaongelea wanafunzi 300,000 (tokana na takwimu za Nipashe ambazo mwandishi amenukuu)kwa mwaka. Idadi hii ya wanafunzi wa sasa imeongezeka mara 100 idadi ya wanafunzi katika miaka ya 1970 - 1979 au ambayo pia kwa lugha nyingine ni sawa na ongezeko la asilimia mia 1,000 (1,000%). Hapa tunaongelea wanafunzi wa chuo kikuu pekee, bado hatujaweka wanafunzi wa shule za awali, msingi na sekondari. Je kweli uchumi wetu umeongezeka kiasi hiki kuwa Lowassa atatoa elimu bure kwa wanafunzi wetu hata kama mashangingi yatatolewa yote?

Anonymous said...

Ni ndoto kusema elimu itakuwa ya bure mpaka chuo kikuu. Na ikitokea ndoto hii ikawa kweli basi ni wanafunzi wachache sana watasoma elimu ya juu maana watachukuliwa wachache sana. Enzi za mwalimu shule za msingi kufaulu kwenda sekondari ilikua mbinde sio kwamba wanafunzi walikua wabaya kitaaluma hapana ila nafasi ya kifedha na nafasi za kwenda sekondari zilikua chache hali hiyo hiyo na chuo kikuu.
Ikifanikiwa hii ndoto tunarudi kutengeneza matabaka zaidi ya walionacho na wasionacho na wazururaji wengi zaidi. Wenye nacho watawapeleka watoto wao shule za kulipia, wasionacho watawaacha watoto bila elimu ndo wazururaji hao nawazungumzia hapa. Ilivyo sasa uchaguliwaji wa watoto kuingia sekondari na chuo ni mkubwa na walio wengi wanapata mikopo na wanaweza kusoma.
Lowassa alikua waziri mkuu, alifanya vizuri kutuletea shule za kata tunamshukuru ila kwa hii sera ya elimu bure zile shule za kata zote zitakuwa maficho ya wezi na wazururaji maana zitakosa wanafunzi.