
Dar es Salaam. Wakati siku ya kupiga kura ikikaribia, madhehebu zaidi yametangaza kubadili muda wa ibada ili kuruhusu waumini wao kushiriki kikamilifu kwenye Uchaguzi Mkuu Oktoba 25.
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) yameshatoa utaratibu wa ibada kwa waumini wake siku ya Jumapili ya Oktoba 25 ambayo ni siku ya kupiga kura kumchagua Rais, wabunge na madiwani.
Mchungaji wa Usharika wa Azania Front, Charles Mzinga alisema mkuu wa kanisa wa KKKT, Dk Fredrick Shoo ametoa maelekezo kuwa siku hiyo ya uchaguzi, muda wa ibada upunguzwe.
Alisema kwa kawaida kwenye usharika huo huwa kuna ibada tatu lakini siku ya uchaguzi kutakuwa na ibada moja fupi itakayochukua saa moja.
“Tutaanza ibada saa 1.00 asubuhi na itakapofika saa 2.00 tutakuwa tumemaliza ili kuwaruhusu waumini kwenda kupiga kura,” alisema.
Alisema baada ya saa 2.00 asubuhi waumini watatawanyika kwenda kupiga kura na kwamba kanisa hilo lina imani muda huo utawatosha kutumia haki yao ya kidemokrasia.
Uamuzi kama huo ulifanywa na Mchungaji Thadei Kibwaga akisema Usharika wa Iringa utapunguza muda wa ibada siku ya Jumapili kwa lengo la kuwawezesha waumini kupiga kura.
“Hata waumini wetu wanaelewa kuhusu utaratibu huo kwa kuwa tulishawatangazia hakuna wasiwasi watapata muda wa kupiga kura,” alisema.
Mchungaji Christosiler Kalata pia alisema Usharika wa Vingunguti wilayani Ilala utakuwa na ibada fupi na akawaomba waumini kwenda majumbani baada ya kupiga kura kumuomba Mungu awape kiongozi bora.
“Tusikae vituoni kusubiri matokeo bali turudi kumwomba Mungu ili upigaji kura uweze kumalizika kwa amani,” alisema.
Juzi, Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) ilisema imetoa uhuru kwa maaskofu kuamua njia rafiki itakayowezesha waumini kupata muda wa kupiga kura siku ya uchaguzi mkuu.
Kwa upande wake, katibu mkuu wa TEC, Raymond Saba alisema maaskofu wa majimbo ndiyo wenye mamlaka ya kupanga utaratibu wa ibada.
Alisema mamlaka kupanga au kubadilisha siku na muda wa ibada si wa TEC bali ni wa maaskofu kwenye majimbo yao.
“Mamlaka ya askofu wa jimbo ni kutoa maelekezo yanayofaa kulingana na sheria na kanuni za kanisa kuhusu siku hiyo ya uchaguzi,” alisema.
Alisema waumini watapata taarifa kutoka kwa maaskofu wao kuhusu utaratibu utakaopangwa kwenye majimbo hayo.
Alisema baraza hilo halijatoa maelekezo yoyote juu ya ibada ya misa takatifu ya terehe 25/10/2015 ambayo ni siku ya uchaguzi.
Katika hatua kama hiyo, Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF), Zachary Kakobe amesema siku ya uchaguzi hakutakuwa na ibada katika makanisa hayo.
Askofu Kakobe pia alichukua uamuzi kama huo mwaka 2010 na makanisa mengine ya kipentekoste yakaungana naye kufuta ibaza za siku hiyo ya Jumapili ili kuwapa waumini wao fursa ya kutumia haki yao ya kidemokrasia.
Badala yake, alisema ibada itafanyika Jumamosi.
Kwa kawaida ibada za makanisa ya kipentekoste huchukua muda mrefu tofauti na makanisa mengine.
No comments:
Post a Comment