Advertisements

Tuesday, October 13, 2015

Mchina wa meno ya tembo akosa dhamana

Meno ya tembo 

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imekataa maombi ya dhamana ya kesi ya kusafirisha nje ya nchi meno ya tembo yenye thamani ya Sh5.4 bilioni inayowakabili watu watatu, akiwamo raia wa China, Yang Glan.

Akitoa uamuzi huo jana, Hakimu Mkazi Mkuu, Renatus Rutta alisema katika kesi za uhujumu uchumi ambazo kiwango chake ni zaidi ya Sh10 milioni zinasikilizwa na Mahakama Kuu ya Tanzania.

Kutokana uamuzi huo, maombi hayo ya dhamana yaliyowasilishwa na upande wa utetezi hayawezi kuzungumziwa na Mahakama ya Kisutu hadi Mahakama Kuu.

Hakimu Rutta alisema Mahakama ya Kisutu kupitia kesi hiyo ya uhujumu uchumi siyo mahali sahihi pa kuomba dhamana na kwamba, sehemu sahihi ni Mahakama Kuu.

Baada ya kutolewa kwa uamuzi huo, Wakili wa Serikali, Pius Hilla aliiomba mahakama kuiahirisha kesi hiyo wakati wakikamilisha upelelezi hasa wa Glan.

Kutokana na ombi hilo, kesi hiyo iliahirishwa hadi Oktoba 26, 2015 kwa ajili ya kuangalia upelelezi iwapo utakuwa umekamilika au la. Washtakiwa wote walipelekwa rumande.

Watuhumiwa wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo ni wafanyabiashara Salivius Matembo na Philimon Manase, ambao wanadaiwa kujihusisha na biashara ya nyara za serikali, uhujumu uchumi na kutoroka chini ya ulinzi halali wa askari.

Watu hao wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Januari Mosi, 2000 na Mei 22, 2014 jijini Dar es Salaam, walijihusisha kuendesha biashara ya vipande 706 vya meno ya tembo vyenye thamani ya Sh5,435,865,000.

Katika kesi nyingine, mkazi wa Mabibo Makuburi, Israel Wilson (20) alifikishwa mahakamani hapo akikabiliwa na shtaka la kusambaza taarifa za uongo kinyume na sheria ya mtandao. Akisomewa shtaka mbele ya Hakimu Rutta na Wakili wa Serikali, Esterzia Wilson ilidaiwa kuwa kati ya Septemba 10 na Oktoba 5, 2015 jijini Dar es Salaam, Wilson alisambaza taarifa za uongo dhidi ya wafanyakazi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

MWANANCHI

2 comments:

Anonymous said...

Kwani Kinana yupo wapi si dhamana jamani
CCM mbona China marafiki zetu

Anonymous said...

Acha unafiki wa Ukawa wewe. Sheria wala siyo urafiki inafuatwa hapa.