ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, October 15, 2015

MH. OTHMAN MASSOUD APONGEZWA NA ZADIA

Na Mwandishi wetu Washington DC
Jumuiya ya Wazanzibari waishio nchini Marekani (ZADIA), imeunga mkono matamshi ya aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Zaznibar Mh. Othman Massoud Othman aliyoyatoa hivi karibuni mjini Unguja.
Aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Othman Masoud Othman
Katika taarifa yake fupi kwa umma ambayo Swahilivilla imepata nakala yake, ZADIA ilimnukulu Bwana Othman akisema kuwa Katiba ya Zanzibar inampa kila Mzanzibari wajibu wa kulinda, kuhifadhi na kudumisha Uhuru wa Zanzibar, Mamlaka ya Zanzibar, Ardhi ya Zanzibar na Umoja wa Zanzibar.
"Maelezo hayo ya Mheshimwia Othman, yanakwenda sambamba na malengo makuu ya Jumuiya ya Wazanzibari waishio nchini Marekani (ZADIA)", ilisema taarifa hiyo, na kusisitiza "Kwa hivyo, ZADIA inapenda kuchukua fursa hii kumpongeza na kumuunga mkono Mheshimiwa Othman Massoud Othman kwa kauli zake hizo za kizalendo"
Taarifa ya ZADIA iliyosainiwa na mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Bwana Omar Haji Ali, imeendelea kuelezea juu ya Bwana Othman alivyowakumbusha Wazanzibari jinsi alivyotekeleza wajibu wake huo wa kikatiba kivitendo kwa kupiga kura "kama alivyopiga" kwenye Bunge Maalum la Katiba mjini Dodoma.
Aidha taarifa hiyo imemkariri msomi huyo wa Sheria akizifafanua kasoro zilizomo kwenye Katiba pendekezwa ya Tanzania ambayo aliielezea kuwa haina maslahi kwa Zanzibar.
"Kitendo hicho cha kijasiri, na maelezo hayo, vinatoa changamoto kwa Kila Mzanzibari kuiga mfano huo. Nasi Wanadiaspora tumezipokea kwa moyo wote changamoto hizo na kuzifanyia kazi kama ambavyo imekuwa kawaida yetu. Na tutafanya juhudi zote na tutashirikiana na wadau wote, ili kuhakikisha kuwa Zanzibar inapata hadhi yake na haki zake ndani ya Muungano wa Tanzania", imemalizia taarifa ya ZADIA.
Itakumbukwa kuwa Mheshimiwa Othman Massoud Othman, alikuwa ni miongoni mwa Wazanzibari waliopiga kura za wazi za "hapana" kwenye Bunge Maalum La Katiba mjini Dodoma kupinga rasimu ya Katiba mpya ya Jamhuri a Muungano wa Tanzania kwa vile ilikuwa inaikandamiza Zanzibar.
Kitendo hicho kilizingatiwa na Wazanzibari wengi kuwa ni cha kijasiri na kizalendo, lakini wachambuzi wanaona kuwa ilikuwa ndiyo sababu ya kuvuliwa wadhifa wake kama Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar.
Hii ilikuwa ni mara ya mwanzo kwa Bwana Othman kuzungumza hadharani tangu kuvuliwa cheo hicho, na kumekuweko na tetesi kadhaa wa kdhaa katika mitandao ya kijamii zikimpa nyadhifa mbalimbali zikiwemo za Kimataifa.

No comments: