
Imesema kama vyama visingesaini maadili ya kukubali matokeo, visingeruhusiwa kusimamisha wagombea wa nafasi mbalimbali, ikiwemo urais. Mwenyekiti wa NEC, Jaji Damian Lubuva alisema hayo jana wakati wa mkutano wa tume hiyo na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari.
Jaji Lubuva alishauri kuwa kama vyama na wagombea wao, wameishiwa sera basi wakae kimya na kusubiri siku ya kupiga kura. Alisema walisaini maadili kwa vyama 22 huku vyama nane vikiwa vimeteua wagombea urais.
Alisema vyama hivyo vilikubali kuwa NEC ndiyo yenye mamlaka ya kutangaza mshindi wa rais na kusaini kukubali matokeo. “Wanachopaswa ni kunadi sera zao ili kuwawezesha wananchi wawachague na siyo kutukana tume na kuwa na wasiwasi nayo katika kutangaza matokeo,” alisema.
Alisisitiza hakuna sababu ya kuwa na wasiwasi kwa masuala mbalimbali, kama vile kufutika kwa wino kama ilivyozushwa hivi karibuni. Alieleza kuwa makamishna wawili wa Tume walioteuliwa hivi karibuni, watasaidia utendaji kazi wa tume hiyo kwa sababu ina shughuli nyingi, tofauti na inavyodaiwa mitaani.
Jaji Lubuva aliwataka wahariri kuepuka kutoa taarifa zisizo sahihi kutoka vyanzo visivyo rasmi, bali kuangalia maslahi mapana ya jamii ya Watanzania. Aliwataka kuepuka upotoshaji katika kazi zao za kila siku.
“Wahariri mnatakiwa kuacha kuegemea upande mmoja katika kutoa taarifa kwani mkiegemea upande mmoja, mtakuwa hamuitendei haki jamii,” alisisitiza. Alitaja baadhi ya mambo ambayo vyombo vya habari, vilikuwa vikipotosha kuwa ni uandikishaji wapiga kura kwa mfumo wa kisasa wa BVR.
Alisema baadhi ya vyombo vya habari, vilidai kuwa uandikishaji huo haukuenda vizuri, lakini kwamba NEC imepongezwa na nchi kadhaa, mfano Ghana na Angola. Alisema kuwa Kenya ilikuwa na idadi ya BVR ambazo ni mara mbili ambazo Tanzania ilikuwa nazo, lakini Kenya iliandikisha watu milioni 14 tu.
Alisema kwa kipindi kilichobaki ni vyema vyombo vya habari, viache kuegemea upande wowote na kuzingatia maadili, jambo litakalosaidia uchaguzi kufanyika kwa amani na utulivu.
Mkurugenzi wa Uchaguzi, Ramadhan Kailima alitaka wahariri kuepuka kutoa taarifa za vitisho, kwani zinaweza kuzuia watu kupiga kura na kusababisha kuvunjika kwa amani. Alisema kalamu inaua kwa umbali mrefu kuliko risasi.
Kailima alisema Oktoba 15 mwaka huu vifaa vya uchaguzi vitakuwa vimewasili katika majimbo yote ya uchaguzi na siku ya kupiga kura wananchi watakaokuwepo kituoni saa 10 jioni askari atasimama nyuma yao.
Pia, alisema wiki ijayo NEC itatoa idadi kamili ya wapigakura baada ya kukamilisha madaftari na siku nane kabla ya uchaguzi, watabandika katika vituo. Katibu wa Jukwaa la Wahariri ambaye ni Mhariri Mtendaji wa gazeti la Tanzania Daima, Neville Meena alisema alitaka utaratibu wa kutolewa vitambulisho kwa ajili ya waandishi kuripoti habari za uchaguzi, unaofanywa na Idara ya Habari (MAELEZO) kwa kuzingatia ‘Press Card’, kubadilishwa kwani waandishi wengi hawana.
Suala hilo liliungwa mkono na wahariri wengine, waliotaka utaratibu wa miaka mingine wa mhariri kuandika barua na kupeleka Tume utumike, jambo ambalo NEC waliahidi kulishughulikia kwa kushirikiana na MAELEZO.
Makamu Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu Hamid Mahmoud Hamid alisema kwa wananchi ambao majina yao hayataonekana kwenye daftari huku wakiwa na vitambulisho, watashughulikiwa ili kupiga kura.
Alisema ingawa tatizo hilo lilijitokeza wakati wa uhakiki wa Daftari, wale wachache watakaobainika kuwa na tatizo hilo, watapiga kura baada ya NEC kujiridhisha. Karipio la NEC juu ya vyama au wanasiasa, limekuja baada ya siku za hivi karibuni baadhi ya viongozi wakuu wa vyama vya upinzani, kuelezea hofu ya kuibiwa kura mara kwa mara.
HABARI LEO
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake