Dar es Salaam. Zikiwa zimebakia siku sita kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu, Watanzania wameibua mambo matano yanayoweza kuliepusha Taifa na vurugu zinazoweza kutokea baada ya uchaguzi.
Mambo hayo ni pamoja na uwazi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), pande zinazohusika kuheshimu sheria, wagombea kuwa wakweli kwa wafuasi wao, kukaa pamoja kuweka mwafaka wa kitaifa na NEC kuwa huru.
Mambo hayo yametajwa kukiwa na mvutano kati ya vyombo vya dola na viongozi wa vyama vya upinzani kuhusu suala la wananchi kukaa mita 200 au kwenda majumbani baada ya kupiga kura.
Tayari Rais Jakaya Kikwete ameshaagiza vyombo vya dola kuchukua hatua kali dhidi ya watu watakaokaidi agizo la kuondoka kituoni baada ya kupiga kura.
Mbali na mvutano huo, juzi wilayani Tunduma mkoani Mbeya mfuasi mmoja wa CCM alimuua kwa kumchoma kisu mwanachama wa Chadema, kabla ya yeye kuuawa pia.
Viongozi kukutana
Kutokana na hali hiyo, mhadhiri kutoka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Emmanuel Mallya alishauri viongozi wa vyama vyote vinavyoshiriki uchaguzi huo wakutane kujadiliana mambo ya kukubaliana katika kipindi hiki kabla ya kufanyika uchaguzi huo, Jumapili.
Mallya, ambaye ni Mkuu wa Idara ya Sayansi ya Siasa chuoni hapo, alisema kukutana kwa viongozi hao kutasaidia kuwarejesha kwenye tafsiri ya uchaguzi wa demokrasia badala ya kuvutana kwa maslahi yao, hatua inayoweza kuliathiri Taifa.
“Pili, uwazi wa NEC unahitajika zaidi katika kipindi hiki, iwaeleze wagombea kuweka mawakala waaminifu na ijenge uhusiano mzuri na vyama, taasisi za kiraia kwani dhamana ya taifa ipo mikononi mwao na lazima wanasiasa waongoze Taifa likiwa salama na siyo walemavu,” alisema Mallya.
Kufuata sheria
Profesa Gaudence Mpangalla wa Chuo Kikuu cha Ruaha mkoani Iringa alisema ili kuepuka vurugu ni kuhakikisha sheria zinafuatwa.
Alisema ili kufuatwa sheria lazima wanasiasa wajenge utamaduni wa kuwa wakweli kwa wafuasi wao.
“Ushindani siyo vita wala uhasama lakini inaonyesha kundi la vijana limekosa uvumilivu na walitakiwa kuelimishwa ukweli, watambue itikadi zao haziwezi kuwa zaidi ya maslahi au amani ya Taifa,” alisema Profesa Mpangalla.
Uwazi wa NEC
Kwa upande wake, Profesa Mohammed Bakari kutoka Idara ya Sayansi ya Siasa, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM), alitaja jambo jingine linaloweza kunusuru amani ni uwazi wakati wa shughuli za NEC.
Alifafanua kuwa licha ya vyombo vya dola kujitahidi katika ulinzi, wafuasi wa vyama vya siasa wanakosa imani na NEC baada ya kuwazuia wasisubiri matokeo ya uchaguzi mita 200 kutoka vituoni, suala ambalo ni tofauti na maelekezo ya sheria inayowataka kukaa umbali wa mita 200 kutoka kituoni.
“Mwaka 2010 walijikusanya kusubiri kura na waliondoka wakiwa wameridhika na matokeo lakini kwa nini NEC izuie na kauli ya Rais inatumika kama agizo la Amiri Jeshi Mkuu, kwa hivyo dola lazima itekeleze wakati kauli zake nyingine zimeonyesha upendeleo kwa chama chake, hii ni hatari sana,” alisema.
Vijana waepuke kutumika
Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanawake nchini, Profesa Ruth Meena aliwataka vijana kuepuka kutolewa kafara na wanasiasa wenye maslahi yao ya kuelekea Ikulu.
“Burundi ilipochafuka kina mama, watoto na vijana ndiyo walioanza kuumia na machafuko lakini viongozi walikuwa kwenye ulinzi mkali kwa hivyo lazima vijana wajitambue itikadi zao haziwezi kuwa zaidi ya maisha yao,” alisema.
“Lakini pia wanasiasa wote lazima wajiandae kupokea matokeo, hakuna aliyeshinda au aliyeshindwa hadi sasa na uchaguzi ni sawa na mchezo wa soka kwani lazima kuna mmoja atashindwa na mwingine kushinda.”
Vyombo vya habari kutenda haki
Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Rajabu Katimba alisema mbali na tahadhari hiyo, Rais hatakiwi kutoa matamko yanayokinzana na sheria zilizopo huku vyombo vya habari vikitakiwa kutenda haki.
“Kama ni haki ya kisheria kulinda kura umbali wa mita 200 basi Rais Kikwete anatakiwa kuheshimu hilo na wananchi watamwelewa.”
“Lakini pia NEC inatakiwa kuheshimiwa kwa sheria inazosimamia, wafuasi wa vyama na wagombea kujiepusha na kauli zinazovunja sheria za uchaguzi na mwisho kabisa vyombo vya habari vitende haki katika kuripoti habari zake,”alisema Katimba.
No comments:
Post a Comment