ANGALIA LIVE NEWS

Monday, November 30, 2015

Azma ya kuwa na kizazi kisicho na UKIMWI, muda wa vitendo ni sasa

Mark B. Childress, Balozi wa Marekani katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ubalozi wa Marekani
Dar es Salaam
TANZANIA
MAONI YA BALOZI

Azma ya kuwa na kizazi kisicho na UKIMWI, muda wa vitendo ni sasa
Na Mark B. Childress, Balozi wa Marekani katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
1 Disemba 2015

Mwaka mmoja uliopita wakati wa maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani, niliandika makala kuhusu jitihada za kuwa na kizazi kisicho na UKIMWI nchini Tanzania.  Toka wakati huo, kwa pamoja tumepiga hatua muhimu kuelekea katika kufikia azma hiyo, tukielekeza rasilimali na shughuli zetu kwenye maeneo yenye mahitaji zaidi nchini kote. Hata hivyo, bado tunahitajika kuongeza nguvu na kufanya zaidi. Bila ya kuongeza kasi yetu katika mwelekeo huu, maambukizi mapya yataongezeka, jambo litakaloongeza idadi ya Watanzania watakaokuwa wakiishi na VVU hivyo kuathiri maendeleo na ukuaji wa uchumi wa Tanzania.

Kipindi cha miaka mitano ijayo ni kipindi muhimu sana katika kufikia lengo la kutokomeza kabisa UKIMWI duniani ifikapo mwaka 2030. Rais Obama ameweka malengo makubwa kwa Mpango wa Rais wa Marekani wa Kudhibiti UKIMWI (PEPFAR), akitangaza kuwa hadi ifikapo mwishoni mwa mwaka 2017, PEPFAR itakuwa inawasaidia watu milioni 12.9 kupata matibabu yanayookoa maisha ya  kufubaza VVU na kuwawezesha wanaume milioni 13 duniani kote kupata tohara.  Aidha, kwa kushirikiana na wadau wa kiserikali, asasi za kiraia na sekta binafsi, PEPFAR itajielekeza katika kupunguza maambukizi ya VVU kwa asilimia 40 miongoni mwa wanawake vijana na wasichana katika nchi zilizoathiriwa zaidi  zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara.


Tunatarajia kuwa nchini Tanzania, katika kipindi cha miaka mitano ijayo tutakuwa tumeweza kuwapatia dawa za kufubaza VVU zaidi ya watu 840,000 wake kwa waume na watoto na tutakuwa tumechangia zaidi ya Dola za Kimarekani milioni 430 kwa ajili ya miradi ya kukabiliana na VVU ambayo itasaidia shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuzuia maambukizi, kutoa matunzo na matibabu kwa wagonjwa, kupunguza athari zitokanazo na janga hili, kuimarisha mifumo ya utoaji huduma za afya na utafiti.  Tutaendelea kufanya kazi hii kwa ushirikiano na Mfuko wa Kimataifa wa Kukabiliana na UKIMWI (Global Fund), Shirika la Umoja wa Mataifa la Kupambana na UKIMWI (UNAIDS), wabia wengine wa maendeleo na sekta binafsi ili hatimaye tuweke kulitokomeza janga hili.

Kuwasaidia watu wa Tanzania wanaoishi na VVU na wale waliokatika hatari kubwa ya kuambukizwa virusi hivyo, kunahitaji kuchukuliwa kwa hatua za haraka na kuwa na dhamira ya dhati iliyoendelevu. Watanzania wanastahili kuwa na mfumo wa afya wanaoweza kuuamini kwa muda mrefu. Hii itahitaji Serikali ya Tanzania kuongeza uwekezaji wa fedha kutoka vyanzo vyake vya ndani, vya umma na kutoka sekta binafsi ili kuboresha mfumo wake wa afya na kuelekeza zaidi rasilimali kwa watu na maeneo yenye uhitaji zaidi.  Kwa hali hii, napenda kumpongeza Rais Magufuli kwa hotuba yake ya tarehe 20 Novemba kwa Bunge na taifa ambapo alisisitiza azma ya serikali ya kuongeza bajeti inayotengwa kwa ajili ya madawa na mfumo wa usambazaji wake.

Mwaka 2015, Serikali ya Tanzania ilichukua hatua muhimu pale ilipoanzisha Mfuko wa Taifa wa Kukabiliana na UKIMWI (AIDS Trust Fund). Hata hivyo hii bado ni hatua ya mwanzo tu na bado kiwango kilichotengwa kwa mfuko huu cha dola milioni 1.5 ni kidogo mno.

Mchango mkubwa zaidi na endelevu wa serikali ya Tanzania kwa mfuko huu ni muhimu sana, sio tu kwa lengo la kuwezesha kushughulikia mahitaji ya sasa bali pia kuwezesha upatikanaji wa kuaminika na endelevu wa fedha za kutosha kuwahudumia watu wanaoishi na VVU na hatimaye kuweza kulidhibiti kabisa janga hili. Aidha, upatikanaji endelevu wa rasilimali za kutosha kukabiliana na janga hili utahitaji ushiriki mkubwa zaidi wa jamii zikishirikiana na asasi za kiraia na viongozi wa maeneo yao pamoja na ubia imara zaidi na sekta binafsi.

Serikali ya Marekani bado imedhamiria kuendelea kushirikiana na wabia wetu katika kufikia azma ya kuwa na kizazi kisicho na UKIMWI. Siku ya UKIMWI Duniani inatoa fursa ya kumualika na kumchagiza kila mmoja wetu – viongozi wa serikali, wadau wa maendeleo kutoka nchi mbalimbali na wale wanaowakilisha taasisi za kimataifa,  asasi za kiraia, sekta binafsi na wadau wengine wote, kuungana pamoja na kushikamana katika kuhakikisha kuwa hakuna mmoja wetu anayeachwa nyuma.  Haitakuwa rahisi kufikia malengo yetu. Lakini ili tuweze kuyafikia ni lazima sasa tugawane majukumu na kudhamiria kwa dhati kuimarisha jitihada zetu. Muda wa kuchukua hatua kwa vitendo ni sasa.


686 Old Bagamoyo Road, Msasani, P.O. Box 9123, Dar es Salaam
Telephone +255-22-229-4000, Fax +255-22-229-4722

No comments: