Tuesday, November 10, 2015

JK aipa neno Stars, amfagilia Samatta

RAIS mstaafu wa Tanzania, Dk Jakaya Kikwete amesema Taifa Stars kama inahitaji ushindi katika mchezo wa kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Algeria inahitaji kujituma kwa moyo.

Taifa Stars inatarajia kucheza mchezo wa kwanza dhidi ya Algeria Jumamosi ya wiki hii kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.

Akizungumza na kituo kimoja cha redio juzi, Dk Kikwete alisema Taifa Stars inahitaji kuonesha juhudi kwa kujituma kwenye uwanja wa nyumbani ili kupata ushindi.

Dk Kikwete alitaja changamoto nyingine itakayotegemea na ushindi kuwa ni uteuzi wa timu ambao tayari Kocha Mkuu Charles Mkwasa aliteua kikosi kilichokuwa kambini Afrika Kusini kujiandaa na mchezo huo dhidi ya Algeria.

Alisema ana imani Taifa Stars ina uwezo wa kuifunga Algeria kama changamoto hizo zitazingatiwa kwa kuhakikisha wachezaji wanajituma nyumbani.

“Hata bahari kuu huvukwa,” alisema na kuongeza kuwa timu ya Algeria ni bora lakini katika michuano ya Afrika ilifungwa na ikatolewa, hivyo hata Taifa Stars ina uwezo wa kuifunga. Alisema ni muhimu mashabiki wajitokeze kwa wingi kuiunga mkono Taifa Stars katika mchezo huo.

Wakati huo huo, Rais Kikwete amempongeza mshambuliaji wa Tanzania anayechezea TP Mazembe ya Jamhuri wa Kidemokrasia ya Congo (DRC), Mbwana Samatta kwa kuisaidia timu yake kutwaa ubingwa wa Afrika.

Samatta alifunga bao la kwanza katika mchezo huo wa fainali dhidi ya USM Alger ambapo timu yake hiyo ilishinda kwa mabao 2-0 mjini Lubumbashi, DRC Jumapili.

Mchango wa bao hilo la Samatta uliiwezesha timu yake hiyo kuibuka na ushindi wa jumla ya mabao 4-1 baada ya awali kuibuka na ushindi wa 2-1 katika mchezo wa awali uliofanyika Algiers wiki moja iliyopita, ambapo pia Samatta alifunga bao moja.

Dk Kikwete alisema kwa juhudi aliyoonesha Samatta katika timu yake ana imani ataionesha pia Taifa Stars Jumamosi. Pia alisema ana imani kiwango alichoonesha mchezaji huyo hakitaishia hapo bali kucheza soka la kulipwa Ulaya.

Samatta na Mtanzania mwingine wanaochezea TP Mazembe, Thomas Ulimwengu wanajivunia rekodi mpya waliyoweka kuwa Watanzania wa kwanza kucheza fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kutwaa ubingwa huo.

Pia Samatta anajivunia rekodi ya kuwa Mtanzania wa kwanza kufunga bao katika Ligi ya Mabingwa Afrika, baada ya kufunga bao la pili katika ushindi wa 2-1 dhidi ya USM Alger katika fainali ya kwanza mjini Algiers na pia kufunga bao la kwanza juzi katika fainali ya pili iliyoisha kwa ushindi wa mabao 2-0.

Awali Samatta na Ulimwengu walivunja rekodi iliyowekwa na klabu ya Simba SC ya Dar es Salaam mwaka 1974 kwa kucheza nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, walipotolewa na Mehalla El Kubra ya Misri kwa penalti 3-0 baada ya sare ya jumla ya 1-1, kufuatia kila timu kushinda 1-0 nyumbani kwake.

HABARI LEO

2 comments:

  1. Kuweka usiasa kila sehemu, lakini vipi kuhusu Richmond na lowasa?

    ReplyDelete

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake