
Mmoja wa wamiliki wa hisa kwenye klabu ya Monaco, Alessandro Proto alifichua kwamba alikutana na Bilionea Abramovich jijini London kwa lengo la kumchukua Mourinho, ambaye kwa sasa yupo kwenye wakati mgumu klabuni Chelsea.
Lakini, baada ya kuweka ofa ya Pauni 35 milioni mezani, Abramovich aligoma kupokea na hivyo kumfanya Proto kufichua kwamba Monaco inajipanga upya kuja na kiasi cha Pauni 71 milioni ambazo wanaamini zitatosha kumnasa.
Mourinho yupo kwenye wakati mgumu sana kwa sasa kwenye kikosi chake cha Chelsea baada ya kupoteza mechi sita kwenye Ligi Kuu England. Mwenyewe amesema hawezi kuondoka, lakini taarifa zimefichua kwamba amepewa mechi mbili za kunusuru kibarua chake.
Proto alisema Monaco ina dhamira ya dhati ya kumchukua Mourinho na kwamba hawatajali mapito anayopita Mreno huyo Stamford Bridge kwa sasa.
Miamba hiyo ya Ligi Kuu Ufaransa inataka kuununua mkataba wa Mourinho ambao utafikia tamati mwaka 2019.
Abramovich aligomea ofa ya awali ya Pauni 35 milioni, lakini Proto Enterprises, kampuni inayomiliki hisa kwenye klabu ya Monaco inaamini kama itaongeza dau na kufikia Pauni 71 milioni, Abramovich hawezi kugomea.
Mapema juzi Jumanne, Mourinho alibainisha mipango yake ya kuendelea kubaki Chelsea hadi mkataba wake utakapofika ukingoni.
“Nina mkataba wa miaka minne. Hadi kufika sasa miaka mitatu na miezi saba imebaki. Ndiyo, nafahamu matokeo yamekuwa mabaya, lakini ninachowaambia nitakuwa hapa kwa muda mrefu,” alisema.
Mwanaspoti
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake