Matokeo haya yametolewa na Twaweza kwenye muhutasari wa utafiti wenye jina la Nusu nusu? Maoni ya wananchi kuhusu upatikanaji wa maji safi. Muhutasari huu umetokana na takwimu kutoka Sauti za Wananchi, utafiti wa kwanza barani Afrika wenye uwakilishi wa kitaifa unaofanyika mara kwa mara kwa njia ya simu za mikononi. Matokeo yametokana na takwimu zilizokusanywa kutoka kwa wahojiwa 1,852 wa Tanzania Bara kati ya tarehe 9 Septemba na 26 Septemba 2015 (Zanzibar haikuhusishwa kwenye matokeo haya).
Takribani nusu ya wananchi wote (asilimia 44) hutumia zaidi ya dakika 30 kufuata maji kwa ajili ya mahitaji yao, wakati mwongozo wa serikali unapendekeza kuwa wananchi hawapaswi kutumia zaidi ya nusu saa kufuata maji kwa ajili ya matumizi ya kila siku. Katika maeneo yote ya mijini na vijijini, mwananchi mmoja kati ya watatu wametaja ukosefu wa vyanzo vya maji kama changamoto yao kubwa.
Kwa ujumla, wananchi wanakumbana na masuala kadhaa kwenye kupata maji, huku kukiwa na tofauti kubwa ya upatikanaji wa maji ndani ya jamii za vijijini na mijini. Kwa wakazi wa vijijini, changamoto yao kubwa ni umbali wa vyanzo vya maji (asilimia 47) na uchafu wa maji (asilimia 40). Kwa upande wa mijini, mgao wa maji (asilimia 43) na gharama kubwa za maji (asilimia 40) ndivyo vinavyowatatiza zaidi.
Asilimia 57 waliripoti kutumia njia mojawapo ya kutibu maji yao ili yawe salama. Wengi zaidi walisema walichemsha maji yao (asilimia 85). Idadi kubwa nao waliripoti kuchuja maji (asilimia 69) au kuyaacha yatuwame uchafu ubaki chini (asilimia 38). Hata hivyo, njia hizi kwa viwango vya kimataifa, hazikubaliki kama njia za kuyafanya maji yawe safi na salama.
Licha ya miaka miwili ya Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa, wananchi wengi (asilimia 80) hawakuona mabadiliko yoyote katika sekta ya maji ndani ya kipindi cha miaka miwili iliyopita. Hivyo haishangazi kuona kwamba asilimia 65 ya wananchi wanasema upatikanaji wa maji safi na salama bado ni changamoto kubwa inayoikabili jamii yao.
Katika miezi ya hivi karibuni, kulivuma taarifa nyingi kwenye vyombo vya habari kuhusu mlipuko wa kipindupindu nchini. Kipindupindu huenea kwa njia ya maji machafu, na njia nyingine. Hata hivyo, taarifa za matumaini ni kuwa ni asilimia 6 tu ya wananchi walioripoti kuona au kusikia mtu aliyeugua kipindupindu ndani kipindi cha wiki nne kabla ya utafiti.
Aidan Eyakuze, Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza alisema "Kuna usemi usemao, Maji ni Uhai. Cha kusikitisha kwa Watanzania wengi ni kuwa, maji, na vyanzo vyake mchini, ndivyo vinavyoweza kusababisha maradhi au hata kifo kwao. Takwimu za miaka kadhaa zimetuonesha kuwa kuongeza tu kwa rasilimali hakuboreshi upatikanaji wa maji safi na salama. Hakuna njia ya kukwepa kutoa huduma ya maji kwa kila mwananchi maana huduma hii muhimu sana. Serikali mpya ina fursa ya kipekee ya kupitia upya mikakati yetu kwenye sekta ya maji na kutafuta suluhisho za kudumu. Hivyo basi, hatuna namna nyingine, bali kufikiri haraka na kibunifu kuhakikisha wananchi wanapata maji safi na salama-ambayo ni haki yao ya msingi’’.
---- Mwisho ----
No comments:
Post a Comment