ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, November 25, 2015

WANAHARAKATI WA TANZANIA WANATOA WITO KWA JAMII KUCHUKUA HATUA ILI KUMLINDA MTOTO APATE ELIMU BORA NA SALAMA

  Eda Malick kutoka Tanzania Women and Children Welfare center akizungumza na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi wa siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia
 Afande Christina Onyango, Afisa wa Polisi, mkoa wa kipolisi Ilala akielezea namna ambavyo dawati la jinsia wamejipanga kufikisha ujumbe wa siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia.
  Waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali nchini Tanzania wakihudhuria mkutano na waandishi wa habari kuhusu uzinduzi wa siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia.
 Bahati Mandago kutoka shirika la Tanzania Human Rights fountain akielezea mikakati ya shirika lake katika kufikisha ujumbe wa Funguka. Chukua Hatua Mlinde Mtoto apate elimu.

Wadau kutoka katika mashirika mbalimbali wanaoshiriki kikamilifu katika utekelezaji wa maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia wakiwa katika mkutano na waandishi wa habari
 Dr. Judith Odunga Mkurugenzi wa Shirika la WiLDAF akisoma taarifa kwa vyombo vya habari kuhusiana na kuanza kwa siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia.

FUNGUKA! CHUKUA HATUA MLINDE MTOTO APATE ELIMU

Katika kuadhimisha Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia kuanzia tarehe 25 Novemba mpaka 10 Desemba, WiLDAF, Mashirika ya Haki za Binadamu, Wadau wa Maendeleo na Asasi za Kiraia watatoa elimu na kuhamasisha umma kuchukua hatua kumlinda mtoto ili apate elimu bora na salama. Ulinzi wa mtoto ni pamoja na kuzuia vitendo vyote  vya ukatili wa kijinsia.

Maadhismisho ya SIku 16 za kupinga Ukatili wa kijinsia mwaka huu yanalenga zaidi kuzungumzia suala zima la usalama  mashuleni, lengo kuu ikiwa kuhamasisha umma kuhusu ukubwa wa tatizo la ukatili wa kijinsia kwa vijana na watoto wetu mashuleni, kwani vitendo vingi vya ukatili wa kijinsa vimekuwa vikiripotiwa.

Utafiti uliyofanywa na Chuo cha Tiba Cha Muhimbili (MUHAS) kwa kushirikiana na Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Afrika, (WiLDAF) umetambua hatari zinazochangia ukatili wa kijinsia ikiwa ni pamoja na wazazi kutowajali watoto na kutoa adhabu kali kwao na hivyo kuwafanya watoto kuwa na hofu. Wakati mwingine watoto kufanyiwa ukatili bila wao kufahamu. Aidha, adhabu ya viboko inahusishwa kama moja ya aina za ukatili dhidi ya watoto. Hii inaathiri maendeleo ya elimu ya watoto katika taifa letu.

Kukosekana kwa usawa kati ya watoto wa kiume na wa kike hunapelekea kuwajengea hofu watoto wa kike,  na wakati huo kuwajengea watoto wa kiume ujasiri wa kuona kuwa ni sahihi kwao kufanya  vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Aidha, tafiti kuhusu Ukatili Dhidi ya Watoto (VAC) uliofanywa na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia watoto (UNICEF) wa mwaka 2011 ulionesha kwamba watoto 3 wa kike kati ya 10 na mtoto 1 kati ya watoto 7 wa kiume wenye umri kati ya miaka 13-24 wamewahi kufanyiwa ukatili wa kingono. Aidha, asilimia 6 ya watoto wa kike wamelazimishwa kufanya tendo la ngono kabla ya miaka 18. Pia utafiti huo unaonesha kuwa watoto wa kike wanafanyiwa vitendo vya kingono  na wanaume waliowazidi umri wakati watoto wa kiume wanafanyiwa ukatili na watoto wenye umri sawa.

Tafiti pia imeonesha kuwa vitendo hivyo vinafanywa na watu wanaowafahamu wakiwemo majirani, wapenzi wao, watu wenye mamlaka (walimu). Ni  asilimia 32.2 tu ya watoto wa kike na asilimia 16.6 ya watoto wa kiume wamefanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia na watu wasiofahamika na watoto. Vitendo hivi hufanyika maeneo ambayo uangalizi wa watu wazima unahitajika kuwepo kwa mfano mashuleni, njiani, majumbani na wakati mwingine katika vyombo vya usafiri.

Ni dhahiri kwamba kwa mazingira, mila na utamaduni ikijumuisha familia za Kitanzania, vimekuwa vikichangia vitendo vya ukatili wa kijinsia. Vitendo vya ukatili na udhalilishaji vina madhara makubwa ya kiafya kwa watoto kwani hukatisha uwezo wao wa kielimu, mahudhurio ya shule na hivyo kupelekea matokeo mabaya ya  katika ufaulu wao wakati wa mitihani.

Aidha, mazingira yasiyo salama kwa watoto wa shule yana madhara makubwa. Watoto wanapokuwa mashuleni na kufanyiwa ukatili wa kingono wapo katika hatari kubwa zaidi ya kupata maambukizi ya UKIMWI kwa mathlani mara tatu zaidi ya wale ambao hawajawahi kufanyiwa ukatili.

Tunaamini kwamba kuondolewa kwa vikwazo vinavyo chochea ukatili wa kijinsia kwa watoto wa shule kutachangia katika kuleta usawa wa kijinsia kwa watoto wa kiume na wa kike. Pia mazingira mazuri ya shule yatasaidia mahudhurio mazuri ya watoto mashuleni na  kuleta matokeo mazuri katika ufaulu.

Jamii inahaswa kuweka mazingira mazuri ya shule ikiwa ni pamoja na kuwepo miundombinu kama mabweni, vyoo, madawati, uzio kuzunguka mashule na vyombo rafiki vya usafiri. Haya yote yatawezekana tu ikiwa kutakuwa na dhamira ya dhati kwa watunga sera, wazazi, walimu, wanafunzi na jamii kwa ujumla katika kuzuia ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto. Kuna haja ya makusudi kabisakutofumbia macho  masuala ya ukatili kwa ujumla wake ili kujenga jamii imara.

Siku 16 za Kupinga ukatili wa kijinsia  ni tukio la kimataifa la kila mwaka ili kuwa na nguvu ya pamoja  katika kuzuia kuenea kwa janga hili . Ndani ya siku hizi, kuna siku zingine muhimu za kimataifa , mathlani, Novemba 25 ni Siku ya Kimataifa ya Kupinga Ukatili Dhidi ya Wanawake, Novemba 29 ni Siku ya Kimataifa ya Watetezi wa Haki za Binadamu, Desemba 1 ni Siku ya UKIMWI Duniani, Desemba 3 ni Siku ya Kimataifa ya watu wenye Ulemavu, Desemba 6 ni Siku ya Kimataifa ya Kumbukumbu ya Mauaji ya kikatili ya Montreal 1989, ambapo wanawake 14 waliuawa na mtu aliyekuwa anawachukia wanawake. Tarehe hizi zilichaguliwa mahususi ili kuhusianisha kwamba ukatili wa kijinsia unaongeza maambukizi ya UKIMWI na ni Ukiukwaji wa Haki za Binadamu.

Katika kipindi hiki cha Kampeni ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia , mamia ya asasi za kiraia na wadau mbalimbali Tanzania wataifikia jamii kwa kauli mbiu inayosema;
FUNGUKA! CHUKUA HATUA MLINDE MTOTO APATE ELIMU.

Kauli hii inalenga kumshawishi mtu binafsi, kuwashawishi walimu, wanafunzi, wazazi na jamii kwa ujumla, kuwalinda watoto dhidi ya  ukatili wa kijinsia na kuhakikisha kwamba shule ni mahala salama. Ni vema kutafakari kwa kina jinsi vitendo vya ukatili wa kijinsia mashuleni vinavyoathiri maendeleo ya watoto wetu kielimu. Hivyo na haja ya kuwa na taifa linalopiga vita vitendo vyote vya ukatili wa kijinsia. Taifa linalofumbia macho ukatili wa kijinsia  haliwezi kupiga hatua kimaendeleo.

Kampeni ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa kijinsia ina lengo la kushawishi watunga sera, wadau na jamii kwa ujumla, kuchukua hatua dhidi ya ukatili wa kijinsia . Pia ina taka jamii kufichua vitendo vyote vya ukatili wa kijinsia ili kuwa  na jamii isiyovumilia ukatili wa aina yoyote.

Hivyo basi WiLDAF na wadau mbalimbali wanaopinga vitendo vya ukatili wa kijinsia wanaitaka serikali kufanya yafuatayo;
1)    Kufutwa kwa adhabu ya viboko mashuleni na walimu kutafuta mbinu za kutoa adhabu mbadala.
2)    Kutengeneza muongozo wa utekelezaji wa sera  ya elimu ya mwaka 2014 utakaolekeza upatikanaji wa elimu ya msingi iliyo bora na salama.
3)    Kuboresha miundo mbinu rafiki kwa watoto wa shule ikiwa ni pamoja na  kuwepo kwa vyoo bora, mabweni, madawati, usafiri, uzio kuzunguka shule na mengineyo kwa ustawi wa watoto wa shule.
4)    Kuunda mabaraza yatakayokuwa yanasimamia malalamiko ya wanafunzi mashuleni.
5)    Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa kushirikiana na Wizara ya sheria na Katiba zitunge sheria ya kudhibiti Ukatili Majumbani na kubadilisha Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971inayoruhusu mtoto wa kike chini ya miaka 18 kuolewa, ama kwa ridhaa ya wazazi, mlezi au Mahakama.

Katika kipindi hiki cha siku 16, za kupinga ukatili wa kijinsia kutakuwa na shughuli mbalimbali na midahalo ili kuleta mabadiliko katika nchi yetu. Tunatoa wito kwa jamii kwa ujumla kupaza sauti na kukemea vitendo vyote vya ukatili wa kijinsia. Jamii ihamasishe usawa wa kijinsia, mahusiano yasiyo na ukatili na  isibague au kunyanyapaa waathirika wa ukatili wa kijinsia. Tusikae kimya bali tufichue ukatili wa kijinsia na kuchukua hatua kuwalinda watoto wetu iliwapate elimu bora na iliyo salama. Kwa pamoja kupitia kauli mbiu ya mwaka tunasisitiza;
FUNGUKA!  CHUKUA HATUA MLINDE MTOTO APATE ELIMU.

Imefadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Watu wa Marekani (USAID Tanzania)
Imetolewa na;
Dkt. Judith N. Odunga (MKURUGENZI)
Kwa niaba ya:
Shirika la Wanawake Katika Sheria na Maendeleo Barani Afrika (WiLDAF)
S.L.P 76215
DAR ES SALAAM    
 

No comments: