SHIRIKISHO la Wasanii Tanzania linalojumuisha Sanaa za filamu,muziki,utamaduni maonesho na ufundi limempongeza Mhe. Dkt, John Pombe Joseph Magufuli kwa kuchaguliwa kuwa Raisi wa Awamu ya tano wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Makamu wake Mhe. Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza na Waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam kwa niaba ya Shirikisho la wasanii Tanzania Bw. Simon Mwakifwamba ambaye ni Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania, Amesema kuwa, watashirikiana nae katika kufanya kazi kwa bidii ili kuleta maendeleo kwa taifa kwa kuzingatia kauli mbiu yake ya “ HAPA KAZI TU”.
Aliongeza kuwa Rais kupitia Serikali yake atakayoiunda ni vema ikasimamia maslahi yenye tija kutokana na kazi zao kwa kuandaa Sera, Sheria na kanuni zitakazowanufaisha wasanii pamoja na kuwaandalia mazingira bora katika kusambaza kazi zao.
Naye mdau wa muziki hapa nchini Bi. Asha Baraka ambaye pia ni Mkurugenzi wa bendi ya muziki ya African Stars (Twanga pepeta) ameiomba Serikali ya Awamu ya tano kusimamia kwa dhati na kuendeleza yale yaliyotekelezwa katika awamu iliyopita ikiwemo haki miliki za wasanii kwa kuwa imekuwa na tija kwao.
Aidha, mmoja wa wasanii wakongwe nchini Bi. Stara Thomas, ameomba mchango wa wasanii uthaminiwe katika uchumi wa nchi kupitia kazi zao na Katiba itakayoundwa ishirikishe wasanii kwa kutoa nafasi sawa kwa wasanii wa fani zote ili kuweza kusimamia kwa karibu kazi zao ikiwa ni pamoja na kuwa na mwakilishi wao bungeni asiyetokana na chama chochote cha siasa.
Sekta ya Sanaa nchini ina nafasi kubwa ya kutangaza nchi kupitia vivutio mbalimbali vinavyopatikana nchini, hivyo sekta hiyo ichukuliwe kama mkombozi wa ajira kwa watanzania kwa kuwa inatoa matokeo chanya kwa kukuza uchumi binafsi na wa taifa kwa ujumla.
-MWISHO-
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake