Saturday, December 5, 2015

RC amsihi Yussuf Manji akubali kuachia Coco Beach

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecky Sadiki amemuomba mmiliki wa Kampuni ya Q Consult inayomilikiwa na mfanyabiashara Yussuf Manji kutumia busara kukubali kuuachia ufukwe wa Coco jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Sadiki alisema Mahakama Kuu ya Tanzania, Kitengo cha Ardhi katika uamuzi wake imeiamuru Manispaa ya Kinondoni, kutekeleza mkataba wake na kampuni ya Q Consult kwa ajili ya kampuni hiyo kuendeleza ufukwe huo hata hivyo Manispaa ya Kinondoni imekata rufaa.

“Kampuni ya Q Consult kwa busara tu iachane na kesi, ikubali kurudisha ufukwe huo chini ya mamlaka ya Kinondoni ili iweze kuuendeleza ufukwe huo kwa manufaa ya wakazi wa jiji la Dar es Salaam na sio kwa manufaa ya mtu mmoja kama anavyotaka mtu huyo,” alisema Sadiki.

Alisema wananchi wafahamu kuwa ufukwe huo wa Coco haujauzwa, kama watu wanavyodai na kwamba kesi hiyo iko mahakamani, ambapo Ofisi ya Manispaa ya Kinondoni kupitia Mwanasheria Mkuu wa Serikali wamekata rufaa.

Akielezea sakata hilo, Sadiki alisema kampuni ya Q Consult inayomilikiwa na Manji mwaka 2007 iliingia mkataba na Manispaa ya Kinondoni kuendeleza ufukwe huo.

Alisema, hata hivyo, baadaye Manispaa ya hiyo ilivunja mkataba huo baada ya Kampuni ya Q Consult kushindwa kutimiza masharti, jambo ambalo liliifanya kampuni hiyo kwenda mahakamani.

Mahakama Kuu ya Tanzania Kitengo cha Ardhi iliamuru Manispaa ya Kinondoni, kutekeleza mkataba wake na kampuni hiyo kwa ajili ya kuendeleza ufukwe huo.

“Kama nilivyosema kupitia mwanasheria mkuu wa Serikali tumekata rufaa katika uamuzi huo kwasababu tunaamini haukuwa sahihi, hata hivyo mwekezaji huyo namshauri tu anaweza kufanya maamuzi akaachana na kesi hiyo na kuamua kurudisha ufukwe huo uendelee kutumiwa na Watanzania wote,” alisema Sadiki.

Kwa kampuni hiyo kushinda kesi hiyo, inamaanisha kuwa mwekezaji huyo endapo ataendeleza eneo hilo, wananchi hawatakuwa na fursa hiyo tena, kama wanavyoutumia sasa.

Sadiki alisema tayari serikali imefanya mazungumzo na moja na benki hapa nchini kwa ajili ya kupata mkopo, ambao utasaidia kuendeleza eneo hilo ili liendelee kubaki chini ya Manispaa ya Kinondoni na kutumiwa na watu wote.

HABARI LEO

4 comments:

Unknown said...

Ni jambo la busara sana kuachana na Coco Beach...Kuwanyima wananchi sehemu ya kupunga upepo ...?

Anonymous said...

Inaelekea wapo watu ambao hawamjui Yusuph Manji vizuri.Yusuph manji ni diwani mwenye nguvu sana wa ccm wa mbagala kuu.wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu alizunguka dar-es-salaam yote kuwapiga tough wagombea wa ccm akiahidi visima vya maji,barabara,zahanati,shule.manji ana hela si mchezo.anajitolea kwa pesa zake si mchezo. manji kamati ya siasa ya mkoa wa dar ilivyokata jina lake kugombea udiwani,alimwandikia mwenyekiti wa ccm taifa jakaya kikwete,kamati kuu ikarudisha jina.yusuph manji ni mwenyekiti wa timu ya Yanga yenye Mamillion ya wafuasi tanzania yote.turudi kwenye somo la coco beach.ilikuwaje uongozi wa manispaa ya kinondoni kumpatia manji eneo hilo kwa mkataba wa ubia LEO HII WAMKANE?tafuteni chanzo.sisi tunaomheshimu Yusuph manji kwa ukweli wa Mungu wa uongozi na misaada yake kwa Yanga na wananchi wa mbagala tunaapa kusimama nyuma yake.DHURUMA,VITISHO SI KWA MANJI,LABDA AWE MWINGINE.

Anonymous said...

MANJI NI DIWANI WANGU MBAGALA,ANATUSAIDIA SANA.TAJIRI WA ROHO NA FEDHA,TUNAMPENDA MANJI.WAPO MATAJIRI BAHILI,HATUUONI MSAADA WAO KWETU RAIA.MHE.MANJI TUPO PAMOJA IWE YANGA UNAKOWALIPA MAKOCHA NA WACHEZAJI WETU POSHO NA MISHAHARA,AU URAIANI MBAGALA,TUNACHIMBIWA VISIMA,TUNAJENGEWA ZAHANATI.ATAKAYETHUBUTU KUMNYANYASA TUTAMCHONGEA CCM TAIFA.

Anonymous said...

Tatizo si kuwasaidia ninyi huko Mbagala, wala tatizo siyo kuwa na pesa nyingi au kuwalipa Yanga sijui yenye wafuasi wangapi, tatizo siyo nguvu za Manji. Tatizo ni kuwa hiyo Coco beach haikutakiwa kubinafsishwa, je ibinafsishwe kwa faida ya nani? Je wananchi walio wengi wanafaidikaje na hiyo beach? Haijalishi alielewana vipi na manispaa ya Kinondoni kwani tunaamini hiyo ni kati ya ile mikataba ya kifisadi inayoendelea kuua nchi yetu ambayo CCM iliendeleza huku ikiwa haiwajali wananchi wake. Inasikitisha hizo comment mbili hapo juu inaonesha jinsi gani sisi waafrika akili zetu bado zinaendelea kutawaliwa kwa vizawadi vidogo vidogo, hiyo inaturejesha enzi za ukoloni wakati utu wetu uliponunuliwa kwa shanga, vitambaa vya nguo na bunduki, inasikitisha sana kuwa bado akili za watanzania wengi bado tegemezi zikitegemea TOKEN badala ya kufanya kazi kujitegemea....wanasubiri matajiri wawalishe na kuwavisha na kuwapa misaada ambayo wangefanya kazi wangepata wanachohitaji hivyo wasingeweza kununuliwa kwa bei ndogo. Kweli bado katika karne hii bado kuna watu wana mawazo ya kitumwa?