Sunday, December 6, 2015

Uganda kidume Chalenji 2015

By Julius Kihampa

Addis Ababa,Ethiopia. Timu ya Uganda imethibitisha ubora wake unaoifanya iwe kinara wa soka kwa nchi za Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kulingana na viwango vya Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) inakoshika nafasi ya 68 duniani baada ya kutwaa Kombe la Chalenji mwaka 2015.

Katika fainali hiyo ya 38 ya mashindano hayo ya Chalenji, Uganda ilicheza kwa kiwango bora na kutwaa ubingwa huo kwa kuifunga Amavubi ya Rwanda bao 1-0 la Caesar Okhuti, (pichani) dakika ya 13 na kuzawadiwa Dola 30,000 (Sh62 milioni) huku Rwanda ikijifariji na Dola 20,0000.

Uganda Cranes inayonolewa na kocha Milutin Srejedovi ‘Micho’ imetwaa taji hilo kwa mara ya 14, ikiwa ni mara ya nne kufanya hivyo dhidi ya Rwanda.

Watoto hao wa Rais Paul Kagame wameshika nafasi ya pili ya mashindano hayo kwa mara ya sita katika miaka hivi ya karibuni.

Mchezo huo uliokuwa mkali na uliotawaliwa na ubabe wa kila aina kutoka kwa wachezaji wa timu zote mbili ulimlazimisha mwamuzi kutoka Somalia kuwa katika wakati mgumu, kila wakati akiamulia ugomvi wa wachezaji wa timu hizo mbili na kutoa kadi kadhaa za njano.

Ubabe katika mchezo huo ulisabababisha mshambuliaji hatari na nahodha wa Uganda, Farouq Miya mwenye umri wa miaka 19, ambaye jana aliichezea nchi yake mechi ya 19, kuzimia dakika ya 60 ya mchezo huo baada ya kugongana na mabeki wa Rwanda wakati wakigombea mpira.

Hata hivyo, Uganda ndiyo iliyokuwa na bahati na kadi hizo kwani wachezaji wawili, beki wa Simba, Juuko Murshid na Bernard Muwanga walionyeshwa kadi hizo kutokana na utovu wa nidhamu pamoja na Jean Claude Iranzi wa Rwanda.

Katika mchezo huo uliotawaliwa kwa muda mwingi na Uganda kipindi cha kwanza, Okhuti alipata bao hilo pekee akipokea krosi safi ya Farouk Miya.

Licha ya Rwanda kuzinduka kipindi cha pili kutaka kusawazisha bao, mambo yalikuwa magumu kwao kutokana na ukuta wa Uganda ukiongozwa na Murshid na wenzake kuwa mgumu, kutopitika kirahisi.

Rwanda ikiongozwa na viungo, Haruna Niyonzima wa Yanga na mwenzake wa Azam, Jean Baptiste Mugiraneza ilifanya mashambulizi kadhaa, dakika ya 46 na 57, lakini safu yao ya ushambuliaji haikuwa makini katika umaliziaji.

Niyonzima alipiga faulo safi dakika ya 13 iliyokuwa ikielekea golini, lakini hata hivyo mabeki wa Uganda walikuwa makini kuondoa hatari hiyo.

Katika mechi ya mapema, mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu, wenyeji Ethiopia, ‘Walia Antelopes’ ambao hawakupewa nafasi yoyote ya kufanya vyema kwenye mashindano hayo waliibuka na ushindi wa penalti 5-4 dhidi ya Sudan na kutwaa Dola 10,000.

Mchezo huo ulimaliza dakika 90 kwa timu hizo kwenda sare ya bao 1-1 na hivyo kuamuliwa kwa mikwaju ya penalti, ambayo imetawala michezo mingi tangu robo fainali.

Kauli za makocha Micho

“Ni matokeo mazuri kwa upande wetu kwa sababu wachezaji walionyesha ari tangu mwanzoni mwa mashindano. Kombe hili ni zawadi kwa Lawrence Mulindwa, ambaye ni rais wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) akichukua nafasi ya Leodegar Tenga aliyeshika nafasi hiyo kwa vipinjdi viwili.

“Najivunia timu yangu na ninaweza kusema kuwa ilikuwa bora zaidi kwenye mashindano haya kwa sababu nilikuja na asilimia kubwa ya wachezaji wenye umri chini ya miaka 20,” alisema kocha Micho

Kocha wa Rwanda

“Nampongeza kocha Micho kwa kuweza kutwaa ubingwa kwani timu nyake iliweza kutumia vyema nafasi ilizozipata. Tulipata nafasi mbili ambazo zingeweza kubadili matokeo ,lakini hazikuzaa matunda.

“Timu yangu imefanya kazi nzuri na kwa kuzitoa timu kama vile wenyeji Ethiopia na Sudan, imedhihirisha kuwa sasa tuna uwezo wa kupambana na timu kubwa Afrika,” alisema kocha Johnathan Mckinstry raia wa Irelend Kaskazini aliyewahi kuinoa Sierra Leone.
Mwananchi

2 comments:

Anonymous said...

Hongera sana the Cranes,Uganda.Mpira wenu Upo Juu Sana.viwango vyenu ni vya hali ya juu.nje ya uwanja yaani magazetini,redioni,katika television na kwenye mitandao mpo cool sana yaani kama vile wajinga-wajinga.ni watu wa kuigwa,ni timu ya kuigwa.mmeshinda challenge mara 14,si jambo dogo.Kivumbi mpira wa Tanzania,Watu wa tanzania,Magazeti ya tanzania,Redio za tanzania.kilichosheheni ni ufundi wa maneno.kiswahili-mingi,uongo,unafiki,majungu,ujanja wa midomo,ukuwadi,ushambenga,ufala-ufala,hayo yote ni kwa wale wanaojiita Wasimamizi, washabiki na wapenzi wa mpira.tukija kwa wachezaji wenyewe,mama yangu,miserable.uwezo wao wa miundo mbinu ya mpira wawapo viwanjani ni mdogo mno wa kufedhehesha na kuchekesha.vichwa vimedumaa kupokea maelekezo ya ushindi,wepesi wa kuishiwa mbinu wawapo uwanjani,wanaendekeza uchawi zaidi,nidhamu yao ndani na nje ya uwanja ni ndogo mno,wengi wao niwavuta bangi,elimu za darasani ndogo,hawajitambui yaani kwa ujumla wake UWEZO MDOGO MNO,HAWAFUNDISHIKI,WANAHESHIMU BANGI NA UJINGA TELE.WAMETUIBIA SANA WATANZANIA,NI ZERO-SIFURI,RUSHA ROHO,BLOOD-FOOL,TO HELL,WAANGAMIZWE.

Anonymous said...

kweli kabisa,tanzania si nchi ya soka la mafanikio.angalia utulivu wetu,amani yetu,upendeleo mkubwa kupita kiasi ambao umetolewa na serikali na taasisi zake kwa malezi ya hali ya juu ya timu yetu ya taifa yaani mabillion yameteketea.hapa mkwasa,hapa kibadeni kule barthez,huyu canavalo,yupo mvuta bangi yondani,nikwambie nini.hakuna mpira tanzania.kilichojaa ni wizi,ubabaishaji,uwezo mdogo,kudumaa kama mtindikio wa akili mbadala za mchezaji kujituma na kusaka ushindi.ni kheri pesa hii ingepelekwa kwenye kuimarisha shule,hospitali,barabara,kilimo,na vipaumbele vingine.hakuna mpira tanzania,hautokuwepo in the near future.kimpira sisi ni mazezeta wa kila tunayecheza naye.awe burundi,kenya,somalia,sudan,malawi,botswana,lesotho,msumbiji,commoro.hapa kwa makusudi nimewaogopa sikuwataja kabisa uganda,kongo,rwanda,zambia.nchi gani hii,kisoka nchi hii Tanzania!