Maharusi, James Katagila na Prugensiana Kahandukahao (waliopo katikati) wakipendeza katika pozi na wapambe wao.
HARUSI ya karne Bongo ndilo neno linalopendeza kutamkwa kuelezea bonge la sherehe ya ndoa inayoendelea kuwa gumzo kubwa kwenye vinywa vya wakazi wengi wa Jiji la Dar es Salaam.
Harusi hiyo ilifanyika Jumamosi iliyopita kwenye Ukumbi wa Mlimani City, Dar baada ya ndoa kufungwa kwenye Kanisa la Kristo Mfalme, Tabata kati ya bwana harusi, James Katagila na bibi harusi, Prugensiana Kahanduka.
magari ya maharusi yakitoka kanisani.
TETESI ZA AWALI
Mapema siku hiyo, habari zilitua kwenye dawati la Amani zikieleza kuwa usiku wa siku hiyo, kutakuwa na harusi ya kukata na shoka kwenye ukumbi huo na kwamba watu maarufu watahudhuria.
AMANI LATINGA, LASHINDWA KUINGIA
Mapaparazi wetu walifanikiwa kuwasili kwenye ukumbi huo, saa moja usiku lakini walishindwa kuzama ndani baada ya ulinzi kuwa wa asilimia mia moja.
James Katagila na Prugensiana Kahanduka, enzi wakiwa wachumba.
NJE YA UKUMBI
Hata hivyo, nje ya ukumbi huo, magari ya kifahari kama Range Rover, Toyota Land Cruiser VX na mengineyo mengi yaliegeshwa huku gari la bibi harusi likiwa ni BMW.
MAHARUSI WAENDA KENYA
Dodosadodosa ya Amani ilibaini kuwa, licha ya wageni waalikwa kibao kuwemo ndani ya ukumbi, maharusi walikuwa wakisubiriwa kutoka jijini Nairobi nchini Kenya walikokwenda kupiga picha kama ‘wanavyoendaga’ ufukweni maharusi wengi wa Jiji la Dar.
“Humu kuingia jamani ni kazi kama hamna kadi. Maharusi mnaowaulizia ndiyo wanasubiriwa. Baada ya ndoa, walienda Kenya kupiga picha,” alisema mwanakamati mmoja aliyekataa kutaja jina lake.
Wanandoa wakiingia ukumbi wa Mlimani City.
YALIYOJIRI
Kinachofanya harusi hiyo kuwa ya karne, ni pamoja na mlolongo wake kuonesha tofauti kubwa na harusi nyingine za Kibongo. Ilielezwa kuwa, mshereheshaji wa shughuli hiyo, MC Makena alipatikana baada ya watu tisa kufanyiwa ‘intavyuu’, yeye ndiyo akashinda.
MA-DJ 10
Pia, ma DJ waliokuwa wakitumbuiza kwenye harusi hiyo kwa kuweka CD, walikuwa 10 ambapo kila mmoja alitengewa muda wake wa kupiga muziki na alipomaliza, hakuwa na kazi tena!
WATUMBUIZAJI
Ili kuifanya sherehe inoge, wasanii mbalimbali walilipwa fedha kutumbuiza. Wasanii hao ni pamoja na Josephine kutoka nchini Uganda aliyeimba wimbo wa Kiganda kuhusu harusi tu.
Mwingine ni JMC kutoka Karagwe, Mkoa wa Kagera. Yeye aliimba nyimbo za Kabila la Wanyambo kutoka mkoani humo.
NYIMBO ZA KIDUNIA
Kwenye nyimbo za ‘kidunia’, walikuwepo Malaika Band, Kalunde Band na B Band ya Banana Zorro ambapo wote walitumbuiza kwenye sherehe ya awali kabla ya maharusi kuingia.
INJILI PIA
Pia kulikuwa na waimba Injili, Rose Muhando na Edson Mwasabwite na waimbaji wao ambao walikonga nyoyo za wahudhuriaji.
KAMERA YA KISASA
Licha ya kuwepo kwa wapiga picha wa video na picha za mnato, lakini pia ndani ya ukumbi huo kulikuwa na kamera ya kisasa (drone), inayofanana na helikopta ndogo ambayo ilikuwa ikipiga picha kutokea juu, ikiongozwa na mtu aliyekuwa anatumia rimoti.
WATU WALIJISEVIA
Kabla ya maharusi kuwasili kutoka Kenya, wageni waalikwa walianza kwa kunywa supu kabla ya kupata msosi na baadaye kukawa na matunda na keki kibao ambapo watu walielekezwa kwenda kujisevia na kula watakavyo bila kujali muda maalum.
PETE ZA NDOA
Amani liliambiwa kuwa pete za ndoa za maharusi zilikuwa na mchanganyiko wa madini ghali ya dhahabu na almasi hivyo kutoa mwonekano usiozoeleka vidoleni.
SHELA
Ilitonywa kuwa, bibi harusi alibadili gauni ‘shela’ mara tatu. Alilofunga nalo ndoa silo alilokwenda nalo kupiga picha Nairobi na silo aliloingia nalo ukumbini.
Maharusi waliwasili ukumbini hapo majira ya saa mbili usiku na kupita kwenye zuria jekundu (red carpet) wakiwa wanapigiwa makofi.
SHUGHULI YACHUKUA SAA 12
Mmoja wa wanakamati wa sherehe hiyo alilihakikishia Amani kuwa shughuli hiyo iliombewa kibali cha saa 12 ambapo ilianza saa 10 jioni mpaka saa 10 alfajiri siku ya pili ambapo wageni waliondoka baada ya kunywa supu nzito!
HONEYMOON UGIRIKI
Juzi, Amani lilimtafuta kwa simu bwana harusi lakini hakupatikana hewani huku habari zikisema yeye na bibi harusi wapo nchini Ugiriki kwa ajili ya kula fungate (honeymoon) na wakirudi kuna sherehe kubwa ya kuvunja kamati huku Bendi ya Yamoto ikitarajiwa kutumbuiza.
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake