Dar es Salaam. Wakati viongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano wamefanikiwa kutumbua majipu katika ukwepaji kodi, ushuru wa bandarini na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, bado kazi hiyo ya kuibua ufisadi inaonekana kuwa kubwa zaidi kwa mujibu wa taarifa mbalimbali za ukaguzi na hoja zilizokuwa zinaibuliwa bungeni, kuna majipu uchungu sita yamebaki.
Suala la kampuni ya kufua umeme ya IPTL, kumalizika au kuanza upya kwa mchakato wa Katiba, mtandao wa ujangili unaopukutisha wanyama wa mwituni, mtandao wa biashara ya dawa za kulevya na mikataba mibovu na usiri wake ni majipu uchungu ambayo yanasubiri mtumbuaji baada ya kulalamikiwa kwa muda mrefu na wanaharakati, wabunge pia kubainishwa kwenye ripoti za ukaguzi.
Tangu alipoapishwa Novemba 5, Rais John Magufuli amevunja bodi za taasisi na mashirika ya Serikali, kuwasimamisha kazi na kutengua uteuzi wa vigogo mbalimbali, akiwamo katibu mkuu wa wizara, vigogo wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
Wakati akifanya hayo, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliibua ufisadi mkubwa Bandari ya Dar es Salaam ambako tayari makontena takriban 14,000 yamebainika kupitishwa kinyemela bila ya kulipiwa kodi au ushuru wa bandari. Lakini wanasiasa na wadau wengine wanaona bado kuna majipu mengi ya kutumbua kama kweli Serikali imepania kupambana na ufisadi.
“Suala la IPTL lazima limalizwe,” alisema Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo,Zitto Kabwe alipoulizwa kuhusu mambo ambayo anaona yanaikwamisha Serikali katika jitihada zake za kuwahudumia wananchi.
IPTL ni kampuni ya ufuaji umeme ambayo iliingia mkataba na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) mwaka 1995, lakini ikapingwa vikali na wabunge, Benki ya Dunia na wadau wengine kutokana na gharama na teknolojia yake ya kutumia mafuta mazito.
Tangu kampuni hiyo iingie mkataba huo, imekuwa ikikumbana na tuhuma zinazoibuka kila mara tatizo la umeme linapojitokeza, ikidaiwa kuwa Serikali inalipia fedha nyingi katika mkataba wake na Tanesco.
Hoja ya kila mara ya wabunge kwamba suala hilo lifikishwe mwisho kwa Serikali kutaifisha mitambo hiyo kama ilivyokubaliwa katika mkataba huo wa takriban miaka 20 iliyopita, haijatekelezwa.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, ambaye alisimama kidete kutetea kuwa fedha zilizochotwa kwenye sakata jingine la umeme la Akaunti ya Tegeta Escrow si za Serikali, atalazimika kuibua uozo uliozunguka sakata hilo la IPTL ili kumaliza tatizo hilo. Mbunge wa zamani wa Kigoma Kusini, David Kafulila alisema hadi sasa kuna wahusika hawajachukuliwa hatua stahiki.
Kafulila alisema Rais Magufuli anapaswa kumchukulia hatua katibu mkuu wa Wizara ya Fedha ambaye alimpa ushauri Mwanasheria Mkuu wa Serikali kusamehe kodi ya Sh21 bilioni wakati akijua wazi kuwa mamlaka ya kusamehe kodi ni ya Waziri wa Fedha.
“Hata Gavana wa Benki Kuu naye ni jipu maana alipohojiwa kuhusu suala la escrow alikiri kushauriwa vibaya. Eliakim (Maswi-sasa Kaimu Naibu Kamishna TRA) na Profesa Muhongo nao wanapaswa kuchukuliwa hatua kwa sababu hawajatutajia waliobeba fedha kwenye viroba,” alisema Kafulila.
Mtandao wa majangili
Mbali na suala la IPTL, jipu jingine lililotajwa na wadau ni kuuvunja mtandao wa ujangili. Wakati idadi ya tembo ikiendelea kupungua, nyara za Serikali zimekuwa zikipitishwa mipakani na kukamatwa nje ya nchi, jambo ambalo hata Rais Magufuli alishasema linashangaza kutokana na mamlaka husika nchini kushindwa kubaini mtandao huo.
Februari 14 mwaka jana, Rais mstaafu Jakaya Kikwete wakati akihojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya BBC alisema Serikali imeubaini mtandao wa ujangili unaojumuisha watu 40, akiwamo tajiri maarufu mkoani Arusha lakini mpaka sasa haujawekwa wazi.
Vigogo dawa za kulevya wanajulikana
Jipu jingine ambalo limekuwa gumu kutumbuliwa ni kufichua mtandao wa biashara ya dawa za kulevya, licha ya viongozi kueleza mara kadhaa kuwa wanawafahamu wahusika.
Tanzania imekuwa njia ya kupitishia au kituo cha dawa za kulevya aina ya heroin, cocaine, mandrax na morphine na mara kadhaa mizigo imekamatwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere na kiwango kikubwa kukamatwa nje ya nchi baada ya kupita katika uwanja huo.
Wabunge wamekuwa wakipiga kelele kila mara kutaka Serikali iwafichue wahusika ambao wanatajwa kuwa ni vigogo wa Serikali, wafanyabiashara wakubwa na maofisa wa polisi, lakini hadi sasa wanaokamatwa ni wale wanaobeba na si walio kwenye mtandao.
“Matukio yote haya yametokea katika kipindi cha utawala wa Serikali ya Awamu ya Nne. Kuna viongozi wa juu serikalini ambao waliwahi kusema kuwa wanawajua wanaojishughulisha na biashara haramu ya dawa za kulevya, lakini mpaka sasa hawajawataja na wala hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa,” alisema msemaji wa kambi ya upinzani, Mohamed Mbarouk wakati akitoa hotuba ya kambi hiyo kuhusu muswada wa Sheria ya Udhibiti na Usimamizi wa Dawa za Kulevya ya Mwaka 2014. Aliwataja viongozi waliotoa kauli hiyo kuwa ni Rais wa Serikali ya Awamu ya Nne, Kikwete, Kamishna wa Tume ya Kudhibiti Dawa za Kulevya, mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola na Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP, Reginald Mengi.
Hadi sasa, usafirishaji wa dawa hizo unaendelea huku polisi wakikamata watu wanaoonekana kuwa wanatumwa.
Kitendawili cha mchakato wa Katiba
Wakati Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe akisema amepewa jukumu la kumalizia mchakato wa kuandika Katiba Mpya kwa kuanzia pale ulipoishia, suala hilo linaonekana kuwa jipu jingine kwa Serikali ya Magufuli.
Wanasiasa, wanaharakati na wadau hawakubaliani na jinsi mchakato huo ulivyoendeshwa na wengi wanaona kuwa unatakiwa uanzie kwenye Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na mwenyekiti wa ilivyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji mstaafu Joseph Warioba na liundwe Bunge jipya la Katiba ambalo halitatawaliwa na itikadi za kisiasa.
Lakini CCM inataka Katiba Inayopendekezwa ndiyo ipigiwe kura kumalizia mchakato huo, jambo ambalo limeshaonyesha kuwa litasababisha kutofautiana tena na Jaji mstaafu Warioba ambaye wiki iliyopita alikutana na Rais Magufuli.
Akizungumzia suala la Katiba, mkurugenzi wa utetezi na maboresho wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Harold Sungusia alisema wizara hiyo inatakiwa itunge sheria mpya ili watakaoshiriki katika mchakato wa kupata Katiba Mpya, wasiruhusiwe kujihusisha na masuala ya kisiasa kwa muda wa miaka 10. Alisema kukosekana kwa sheria madhubuti kulisababisha mchakato wa Katiba kutekwa na wanasiasa ambao walikuwa wanachangia hoja, kutoa mawazo kwa matakwa yao ya kisiasa badala ya masilahi ya nchi.
Migogoro ya ardhi
Wakati mchakato wa Katiba ukisumbua, matatizo yanayosababisha mapigano baina ya wakulima na wafugaji na kupoteza uhai wa watu na mifugo, migogoro ya wananchi na wawekezaji na uvamizi wa maeneo yasiyoruhusiwa kwa ujenzi, yanaonekana kutopatiwa ufumbuzi.
Imekuwa ikielezwa kuwa matatizo hayo yamekuwa yakitokana na ardhi kutopimwa na kugawanywa vizuri, lakini jipu linalosababisha mizozo yote hiyo bado halijatumbuliwa.
Maeneo yaliyokithiri kwa migogoro hiyo ni mikoa ya Manyara, Arusha na Morogoro ambako mapigano hutokea mara kwa mara.
Profesa wa uchumi katika kilimo wa Chuo Kikuu cha Sokoine (Sua), Damian Gabagambi alisema tatizo kubwa la migogoro ya wakulima na wafugaji ni nchi kutopima ardhi yake ili kubainishwa matumizi ya kila mahali.
Rais Magufuli alishasema wakati wa kampeni kuwa atahakikisha waziri anayehusika, mkuu wa mkoa na wilaya husika na kamanda wa polisi wa eneo litakalokumbwa na mapigano baina ya wakulima na wafugaji, hatabakia kwenye wadhifa wake.
Mikataba mibovu
Wakati wabunge wamekuwa wakipiga kelele mikataba mibovu na usiri wake, bado suala hilo limekuwa kama kutwanga maji kwenye kinu; hakuna anayefanyia kazi kilio hicho.
Hadi sasa, hakuna aliyeadhibiwa kwa kuiingiza nchi kwenye mikataba mibovu ambayo inapukutisha utajiri wa nchi.
Profesa Abdallah Safari alisema mikataba hiyo imesababisha nchi kupata fedha kidogo kutoka kwenye rasilimali zake.
“Huwezi kusema kila mtu alipe kodi huku mikataba ya madini ikiwaruhusu wawekezaji kuchimba madini na kulipa kodi baada ya miaka mitano, nadhani huko ndiko kuna fedha nyingi inayopotea,” alisema.
No comments:
Post a Comment