Msemaji wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia watoto, Nsachris Mwamwaja
HOSPITALI za serikali na zile za binafsi hazina chanjo ya polio ya mdomoni (OPV) pamoja na ile ya kinga dhidi ya Kifua Kikuu, Bacille Callimete-Guerin ( BCG) ambazo hutolewa kwa watoto wadogo.
Mtoto anapozaliwa hupewa BCG ili kumkinga asipatwe na kifua kikuu kikali wakati OPV hutolewa kwa njia ya matone ya mdomoni kwa ajili ya kumkinga asipatwe na ugonjwa wa kupooza.
Uchunguzi wa Nipashe katika hospitali za serikali pamoja na binafsi umebaini kuwepo kwa tatizo hilo ambalo limedumu mwezi mmoja sasa kwani baadhi ya hospitali zilikuwa zikitoa kinga ambazo hazijakamilika.
Baadhi ya watoto walionekana wakipewa dawa kuwakinga dhidi ya kifua kikuu na kuambiwa kuwa za polio hazipo na wasubiri tangazo la serikali.
Mariamu Said aliyekutwa katika hospitali ya Palestina jijini Dar es Salaam, alisema baada ya kumpeleka mtoto wake mwenye miezi mitatu hospitalini hapo alipewa dawa ya kumkinga mwanaye dhidi ya kifua kikuu na kutakiwa akatafute kwingine dawa ya chanjo ya polio.
Alisema alihangaika kwenye hospitali mbalimbali lakini hakufanikiwa kupata dawa hiyo “Yaani nimezunguka kutafuta kinga mpaka nimechoka, hapa amechomwa sindano za mapaja nesi akaniambia nijaribu kutafuta kinga ya polio hospitali nyingine, nimefika hapa ndipo nikajua ukweli kuwa kuna tatizo hata hizi za mapaja nimebahatika wengine hawajapata,” alisema.
Akizungumza kitaalamu zaidi, daktari wa watoto katika hospitali ya Misheni ya Mikocheni, Kairuki, Salvatory Florence, alisema miili ya watoto wadogo iko katika hatari kubwa kuambukizwa magonjwa hayo kutokana na kukosa kinga hivyo wanapokosa kinga ya dawa hizo wanakuwa kwenye hatari.
Alisema kinga hizo ni muhimu kwa watoto hasa kutokana na miili yao kuwa bado haijakomaa kupambana na magonjwa kama hayo ya polio na kifua kikuu na kwamba mtoto anayekosa chanjo hizo anapougua huwa katika hatari ya kupoteza maisha.
Alisema wataalamu wanawashauri wazazi wahakikishe watoto wanapata chanjo hizo ili kuwalinda na magonjwa kutokana na mazingira hatarishi wanayoishi.
Msemaji wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia watoto, Nsachris Mwamwaja, alikiri kuwepo kwa tatizo hilo na kwamba juhudi za makusudi zimeshafanyika na wanatarajia chanjo hizo kuingia nchini wakati wowote.
“Kweli kuna uhaba wa chanjo za OPV na BCG katika hospitali za Umma, lakini tunawahakikishia Watanzania kuwa, hadi kesho kutwa (Jumapili) tatizo litaisha, chanjo hizi hutoka nje ya nchi na tunatarajia zifike hivi karibuni,” alisema.
Mpango wa Taifa wa Chanjo Tanzana (EPI), unazitaja chanjo muhimu kuwa ni polio, kifua kikuu, pepopunda, donda koo, kifaduro, surua na homa ya ini.
POLIO
Kwa mujibu wa wataalamu mbalimbali huo ni ugonjwa ambao unaweza kuwapata watoto wa rika mbalimbali lakini watoto wa umri wa chini ya miaka 15 ndio waathirika zaidi.
Ugonjwa huo unaelezwa kushambulia mishipa ya fahamu na hatimaye mtoto kupooza misuli ya mwili mzima kama vile miguu na mikono na wakati mwingine husababishwa na virusi vya polio ambavyo huenezwa kwa njia ya kula na kunywa maji yaliyochafuliwa na kinyesi.
Wataalamu wanasema mtoto huanza chanjo hiyo mara tu anapozaliwa na hutolewa mara nne kwa awamu tofauti ndani ya wiki 12.
KIFUA KIKUU
Madaktari wanasema mtoto huchomwa sindano bega la kulia kama chanjo ya Kifua Kikuu ambayo hutolewa mara baada ya kuzaliwa au pale anapofikishwa kliniki kwa mara ya kwanza.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake