Friday, January 8, 2016

Mke afia 'gesti' akiwa na mchepuko

Mwanamke mmoja (jina linahifadhiwa) anayedaiwa ni mke wa mtu, amefariki dunia katika nyumba ya kulala wageni katika Manispaa ya Bukoba, akiwa na mwanaume mwingine inayesemekana ni hawara yake.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Augustine Ollomi, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa, watu hao walienda katika nyumba hiyo ya kulala wageni iliyopo eneo la Hamugembe Januari 3, mwaka huu na kuchukua chumba namba nane.

Alisema siku iliyofuata saa 6:00 mchana, polisi walipokea taarifa kutoka kwa wahudumu wa nyumba hiyo ya kulala wageni kuwa katika chumba hicho kuna watu waliingia jana yake lakini hadi muda huo mlango wa chumba ulikuwa haujafunguliwa na kuna ukimya uliowatia hofu.

Alisema wahudumu hao waliambatana na polisi na walipofika eneo la nyumba hiyo walimkuta mmiliki wake ambaye alitoa funguo za akiba na kufungua chumba hicho.

“Polisi walipofungua chumba walikuta godoro liko chini lakini kitandani lilipopaswa kuwa kulikuwa na mwili wa mwanamke ukiwa umefunikwa shuka na kuuchukua kwenda kuuhifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera,” alisema.

Kamanda huyo wa polisi mkoa wa Kagera, alisema mtu aliyekuwa pamoja na mwanamke huyo (jina linahifadhiwa) ambaye ni dereva wa basi la abiria linalofanya safari zake kati ya Bukoba na Mwanza, hakukutwa katika chumba hicho na alifunga mlango kwa nje na kuondoka na funguo.Hata hiyo, alisema chanzo cha kifo hicho hakijajulikana lakini kutokana na taarifa walizopata kutoka kwa msaidizi wa dereva huyo wamefanikiwa kumpata mtu aliyejitambulisha kuwa ni mume wa marehemu.

Kamanda Ollomi aliongeza kusema kuwa, mume wa marehemu mkazi wa Butimba, jijini Mwanza, amepatikana na kukabidhiwa mwili wa mkewe, huku uchunguzi wa tukio hilo ukiendelea na kwamba wafanyakazi wawili wa nyumba hiyo ya kulala wageni wanashikiliwa na polisi kwa upelelezi zaidi lakini pia kwa kitendo cha kuficha taarifa za wageni wanaolala katika nyumba hiyo.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake