Sunday, January 10, 2016

Msimamizi mkuu bomoa bomoa Dar alitekwa nyara, kuteswa jijini

Heche Suguti

Acha kuanguka na kupoteza fahamu akiwa ofisini akitoka kwenye operesheni mwanzoni mwa wiki. Imebainika kuwa Mwanasheria wa Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NECM) anayesimamia zoezi la bomoa bomoa, Heche Suguti, aliwahi kutekwa na kuteswa mwaka 2012.

Nipashe limebaini kuwa Julai, 2012, tukio la kutekwa kwa Suguti liliripotiwa na vyombo vya habari ikielezwa kuwa huenda alifanyiwa kitendo hicho na waliokuwa wamewekewa alama ya X kwenye nyumba zao wakati huo.

Ilielezwa kuwa, Suguti alitekwa wakati akisimamia mpango wa ubomoaji wa mahekalu ya baadhi ya vigogo waliojenga kandokando ya mto Mbezi Beach, Mndubwe na eneo la Hifadhi ya Taifa ya Mikoko ufukweni mwa Bahari ya Hindi, jijini Dar es Salaam.

Aidha, tukio hilo lilitokea wiki chache baada ya kutekwa, kuteswa na kupigwa kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari (MAT), Dk. Steven Ulimboka.

Habari kutoka kwa ndugu wa karibu wa mtumishi huyo wa serikali zilieleza kuwa Suguti alitekwa nyara katika eneo la Leaders Club majira ya saa 4:00 usiku, wakati alipokwenda kupata vinywaji na chakula akiwa na na kuteswawadogo zake wawili.

Ilielezwa kuwa akiwa katika eneo hilo, ghafla liliibuka kundi la watu zaidi ya 10 ambao walimkamata Mwanasheria huyo mithili ya kibaka na kumpeleka eneo la giza na kisha kuanza kumpiga.

Ilielezwa kuwa Suguti aliteswa kwa muda na watu hao hadi alipookolewa na watu waliokuwa karibu na eneo hilo, ambao walishtushwa na kelele za kuomba msaada.

Kwa mujibu wa taarifa hizo ambazo zimethibitishwa na Suguti mwenyewe baada ya kutafutwa na Nipashe, tukio hilo liliripotiwa katika kituo cha polisi cha Oysterbay.

Katika kituo hicho, mwanasheria huyo alipewa PF3 na kwenda kutibiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) ambako alilazwa kwa zaidi ya wiki mbili kutokana na majeraha aliyoyapata.

Ilielezwa kuwa kabla ya tukio hilo, mwanasheria huyo alikuwa akipokea simu na ujumbe wa vitisho kupitia ujumbe mfupi wa mkononi tangu NEMC ilipoanza taratibu za kutaka kubomoa mahekalu ya vigogo wa eneo la Mbezi Beach, jijini Dar es Salaam.

Suguti alianguka ghafla ofisini kwake Jumanne ya wiki hii na kukibimbizwa katika Hospitali moja ya jijini kwa ajili ya matibabu hadi juzi mchana aliporuhusiwa.

Licha ya kufanyiwa matibabu, vipimo vilishindwa kubaini ugonjwa unaomsumbua Suguti mara moja licha ya kuwa katika hali mbaya.

Kwa mujibu wa watu wa karibu na Suguti, mtumishi huyo anaendelea vizuri ingawa afya yake haijahimarika kiasi cha kuendelea na shughuli zake kama kawaida.

NEMC kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, pamoja na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, walianza operesheni ya kuweka alama ya X na kubomoa nyumba zilizoko maeneo hatarishi kuanzia Desemba 17 mwaka jana.

Bomoa bomoa hiyo ilisitishwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, siku sita mbele ili kuruhusu wananchi waweze kuhama kwa hiari yao na pia kushiriki sikukuu ya Krismasi na Mwaka Mpya.

Ingawa serikali juzi ilisema sasa haitabomoa tena nyumba zilizo nje ya eneo la bonde la Mto Msimbazi na mahoteli ya kitalii kwenye fukwe ya bahari ya Hindi:

Hadi juzi zaidi ya nyumba 16,000 zilikuwa zimewekewa alama ya X huku zoezi la kuzibomoa likisitishwa kupisha tathmini ya nyumba 681 zilizowekewa pingamizi Mahakama Kuu ya Ardhi kabla ya kuendelea tena kwa nyumba 16,532.

Uwekaji wa alama ya X umezikumba nyumba kadhaa za watu maarufu akiwemo Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Mikocheni B Assemblies of God, Dk. Getrude Rwakatare, wachezaji wa zamani wa timu za Simba na Yanga, hoteli pamoja na uwanja wa Yanga.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake