Spika Rebecca Kadaga (Mb) wa Uganda
afunga Warsha ya siku mbili ya Sekretarieti ya Chama cha Mabunge ya Jumuiya ya
Madola Kanda ya Afrika Jijini Dar es Salaam. |
(Picha zote na Benedict
Liwenga)
Na Benedict
Liwenga.
SPIKA
wa Bunge la Uganda, Mhe. Rebecca Kadaga (Mb), ambae pia ni Mwenyekiti wa CWP
Kimataifa amezihasa nchi Wanachama wa Sekretarieti
ya Chama cha Mabunge ya Jumuiya ya Madola Kanda ya Afrika kuendelea kuwathamini
wanawake kwa kuwapa vipaumbele vya ushiriki katika ngazi za maamuzi pamoja na kuwaenzi
wanawake waliotoa mchango wa maendeleo ya nchi zao.
Spika Kadaga
ameyasema hayo leo Jijini Dar es Salaam wakati akifunga rasmi Warsha ya siku
mbili iliyohusu kujadili ushiriki wa wanawake katika ngazi za maamuzi ili
kubuni mbinu na mikakati ya kuongeza idadi ya Wanawake katika ngazi za siasa na
kijamii.
Mhe. Kadaga ameeleza
kuwa, nchi Wanachama hazinabudi kuthamini mchango mkubwa wa wanawake katika
masuala ya kijamii pamoja na kisiasa, hivyo kuna haja ya kuwaenzi kwa kutunza
nyaraka zao muhimu ikiwemo kuwaendeleza wanawake kielimu ili kuweza kuleta
maendeleo katika nchi husika.
“Ni vema tukaaangalia
mchango mkubwa unaotolewa na Wanawake katika nchi zetu hususani katika masuala
ya kijamii pamoja na kisiasa, basi nchi zetu
hazinabudi kuwajali kwa kuwashirikisha katika ngazi zote muhimu ili kuwe na usawa
kati ya wanawake na wanaume, lakini pia kuna haja ya jamii husika kuwaelimisha
wanawake hawa ili waweze kuleta mchango mkubwa katika jamii zetu”, alisema Spika
Kadaga.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Utendaji ya CPA Kanda ya
Afrika, Mhe. Lindiwe Maseko (Mb) kutoka Afrika Kusini, amezidi kuipongeza
Tanzania katika hatua nyingine kwa kujali haki na usawa katika masuala ya
kisiasa ambapo pia ameimwagia sifa kwa uchaguzi uliopita wa mwaka 2015 kuwa wa huru
na haki na kuzitaka nchi nyingine za Afrika kufanya chaguzi zake kuiga mfano
huo.
Kwa upande wao
Wajumbe wa Warsha hiyo wameendelea kujadili masuala mbalimbali ambayo yanaweza
kuleta mabadiliko katika jamii kwa kuhakikisha kuwa wanawake wanapewa fursa
sawa na wanaume katika masuala ya kisiasa na kijamii ambapo msisitizo mkubwa
unaotolewa katika warsha hiyo ni ‘ushiriki wa wanawake katika ngazi za maamuzi’.
Sambasamba
na hilo, suala la kuwashirikisha wanawake kwa njia ya Vyombo vya habari na
mitandao ya kijamii limezungumziwa katika warsha hiyo ambapo msisitizo
umetolewa wa kutumia mitandao hiyo kwa njia ya kuelimisha umma juu ya nafasi ya
mwanamke katika ngazi za maamuzi ambapo endapo ikitumiwa vema inaweza kuleta
usawa katika jamii.
Nchi
zilizoweza kushiriki katika Warsha hiyo ni Tanzania, Uganda, Kenya, Ghana,
Nigeria, Zambia, Mauritus pamoja na Afrika Kusini.
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake