Friday, February 19, 2016

Mshindi wa kwanza, pili na tatu waeleza siri ya mafanikio yao

Baada ya Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) kutangaza matokeo ya kidato cha nne 2015, mshindi wa kwanza, pili na wa tatu kitaifa wameeleza siri ya mafanikio yao.

BUTOGWA: NILITARAJIA ILI KUSHIKANA MKONO NA MAGUFULI
Mshindi wa kwanza kitaifa, ambaye ni mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Canossa ya jijini Dar es Salaam, Butogwa Shija (17), amesema matokeo hayo aliyatarajia ili kutimiza ndoto yake ya kushikana mkono na Rais John Magufuli.

Akizungumza na Nipashe nyumbani kwao Kipunguni B, kata ya Kiluvya, jijini Dar es Salaam jana, Butogwa alisema kuwa, siri ya ushindi huo imetokana na utaratibu uliowekwa na shule yao wa kujisomea kila mara ikiwa ni pamoja na kufanya mazoezi ya masomo husika.

Butogwa ambaye kimwonekano ni mtoto anayejiamini kimasomo na mwenye uwezo wa kujenga hoja na kuitetea, alisema kusoma kila wakati bila kubweteka ndiko kulikomfanya afanye vizuri katika masomo yake tangu aanze shule ya awali.

Mwanafunzi huyo ambaye ndoto yake ni kusoma taaluma ya udaktari katika Chuo Kikuu cha Harvard cha nchini Marekani, alisema mara zote amekuwa akiwahimiza wazazi wake wamlipie ada ili afanye vizuri kimasomo na baadaye aweze kupata udhamini akiwa chuoni.

“Nataka kusoma udaktari, napenda kuwatumikia watu, naamini kupitia taaluma hii nitatimiza ndoto yangu, tayari nilishaanza kuifanyia kazi, shuleni wanafunzi wenzangu walikuwa wakiniamini wakiumwa walikuwa wanakuja kwangu kuomba ushauri na kuwapa dawa za kutuliza maumivu,” alisema na kuongeza:

“Nimemaliza shule lakini nimekuwa nikifanya kazi ya kujitolea kupitia shirika lisilo la kiserikali la kujitolea la Friends of Children, huko tumekuwa tukienda Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kukutana na watoto wenye matatizo ya vichwa vikubwa na wanaotakiwa kunyooshwa viungo vyao, huwa tunacheza nao na kuwafundisha.”

“Huwa tunakutana na watoto tunaongea nao na kucheza nao, yupo mtoto Abasi ambaye akiwa Muhimbili wodini nilikuwa namfundisha somo la hesabu kwa sababu analipenda, sitaki akose masomo yake eti kwa sababu yupo hospitali anamumwa,” alisema.

Aidha, alisema mara baada ya kumaliza mtihani wake wa kuhitimu kidato cha nne, alikuwa akimtania baba yake anunue suti ambayo siku ambayo atakwenda kumshika mkono Rais Magufuli aivae.

RATIBA YAKE NA MASOMO ANAYOPENDA
Butogwa alisema anapenda masomo yote, lakini hesabu ni somo ambalo mara zote amekuwa akilifanyia mazoezi.
Mshindi huyo kitaifa, ambaye anapenda kula ugali na maharage, alisema walikuwa wakikutana kimakundi kujadili mada mbalimbali za masomo na baadaye walimu huwaunganisha wawili wawili, anayejua sana na anayehitaji msaada.

“Hii ya kutugawa wawili wawili imenijenga zaidi kwa sababu unapofanya majadiliano na mtu asiyejua zaidi yako anakuwa na maswali mengi ambayo yanakufanya usome kwa bidii ili umuelewezeshe, kwa hiyo, Martha Ng’omu, ambaye tulikuwa tukishirikiana naye, maswali yake mengi ndiyo yaliyonisaidia, namshukuru Mungu naye amefaulu,” alisema.

HISTORIA YAKE YA UFAULU
Mshindi huyo alisema tangu alipoanza elimu ya awali ijulikanayo ya Faith kwa sasa Remnant Academy, alikuwa akiongoza lakini alipofika darasa la sita akiwa Shule ya Msingi Masaka iliyopo Kipunguni, alishuka na kushika nafasi ya sita.
“Nisidanganye nilikwazika kwa sababu hata wenzangu walikuwa wakinicheka kwa maana walizoea kuona nikiongoza, hii ilinipa ari ya kusoma zaidi kwa bidii hadi namaliza nimekuwa nikishika nafasi za juu," alisema na kuongeza:

“Mitihani yangu yote kutoka kidato cha kwanza hadi cha nne nilikuwa naongoza, lakini ipo ambayo tulikuwa tukiifanya inajulikana kama Tahosa kwa shule zao lakini ni Moku, nilishika nafasi pili kishule, mtihani mwingine wa 'Joint Exam Catholic Schools (JECS)' tulishika nafasi ya kwanza wanafunzi wawili, mwenzangu ni mshindi wa pili kitaifa katika mtihani huu,” alisema.

Alisema hadi anamaliza ametunukiwa zaidi ya vyeti vya ushindi 18 ambavyo vilikuwa vikimtia moyo katika masomo yake.
Alisema katika mtihani wa kumaliza kidato cha nne alipata daraja la juu la 1.7 na kwamba alifanya masomo kumi ambayo kati yake, tisa alipata alama ya A na moja uraia alipata B.

Masomo aliyopata A ni hesabu, kiingereza, kiswahili, jografia, historia, kemia, biolojia, fizikia na hisabati.
MCHANGO WA WAZAZI NA WALIMU
Alisema wamekuwa mstari wa mbele kwa kumhimiza kila mara asome kwa bidii na pale anaposhika daraja B, wazazi wamekuwa wakienda shule kuhoji, kitendo ambacho kimemjenga.

Pia, alisema walimu wamewajenga vizuri kwani mwanafunzi akifanya vibaya wamekuwa wakimuita kumuhoji, kitendo ambacho kiliwatia moyo kuwa wapo watu nyuma yao wanawafuatilia na wanataka wafanikiwe.

MARAFIKI
Mwanafunzi huyo ambaye ni wa pili katika familia hiyo yenye watoto wawili, aliwashukuru marafiki zake kwa mchango wao katika elimu yake kwa sababu wiki ya mwisho kabla ya mtihani huo aliugua malaria, lakini walikuwa wakisoma pamoja na yeye kuwasikiliza ili asipitwe.

Mama mzazi wa mtoto huyo, Angela Shija, ambaye kitaaluma ni mtafiti katika Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (Nimr), alisema mtoto wake ni mtu asiyependa kushindwa mara zote na husoma kwa malengo.

Alisema mtoto wake anafuraha za aina mbili ambazo ni ushindi wa jumla wa mtihani huo pamoja na Februari 21, mwaka huu (Jumapili) atasherehekea siku yake ya kuzaliwa na atatimiza miaka 17.

MSHINDI WA PILI
Kwa upande wake, mwanafunzi aliyeshika nafasi ya pili kitaifa kutoka Shule ya Sekondari Feza Girls, mbaye ni raia wa China, Congcong Wang (16), alisema sababu ya kufanya vizuri katika masomo yake ni kujiamini, jitihada za kuuliza maswali na kumuomba Mungu.

Alisema alipenda kujichanganya na wenzake raia wa Tanzania na kuwauliza maswali juu ya mambo asiyoyafahamu, kudadisi na kujifunza hata muda ambao siyo wa masomo.

Alisema alitamani kufaulu somo la kiswahili hali ambayo ilimlazimu kujifunza lugha hiyo kwa bidii na kwamba masomo yote alipata A, lakini somo la kiswahili pekee ndio amepata B.

“Kikubwa sikuwa najitenga kwa sababu ya uria wangu, nilishirikiana na wenzangu, kujifunza kwa bidii na kuwauliza mambo mbalimbali na mara zote nilipenda kujifunza hata wakati nikiwa likizo, jambo kubwa pia ni kuwaheshimu walimu na kuwasikiliza kwa makini wanapokuwa darasani,” alisema.

Congcon ambaye alianza kushi nchini 2006, baba yake ni mhandisi na mama yake meneja masoko, alisema muda mwingi alishiriki majadiliano katika makundi ya kujisomea na kutumia fursa hiyo kujifunza mambo asiyoyafahamu.

Alisema alikuwa na rafiki yake, Mese Boniface, ambaye alikuwa akishindana naye katika masomo na muda mwingi walijitahidi kutoachia nafasi ya kwanza na ya pili katika matokeo.

Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Sabahattin Varol, alisema sababu ya shule hiyo kutoa mwanafunzi bora pamoja na kufaulisha wanafunzi wote 44 ni kutokana na kuwaandalia wanafunzi mazingira rafiki ya kusomea na ushirikiano kati ya mwalimu, mwanafunzi na mzazi.

“Walimu na wazazi wanaweza kutembeleana wakati wote, tumekuwa kama familia, wanafunzi wana mazingira rafiki ya kuwafanya wawaze kusoma kwa utulivu,” alisema.

Naye Mwalimu wa Taaluma wa shule hiyo, Zakia Irembe, alisema Congcong amefanikiwa kushika nafasi hiyo kwa sababu hakujiona tofauti kwa sababu ya uraia wake na alipenda kujichanganya ili kujifunza mambo mengi kutoka kwa wanafunzi wenzake.
INNOCENT
Mwanafunzi aliyeshika nafasi ya tatu kutoka Shule ya Sekondari Feza Boys, Innocent Lawrence, alieleza sababu za kufaulu masomo yake ni jitihada binafsi na kujisomea kwa kujiwekea ratiba ambayo hakuwahi kuivunja.

Innocent ambaye alishika nafasi ya kwanza kitaifa katika matokeo ya darasa la saba mwaka 2011, alisema alikuwa akifanya jitihada binafsi za kusoma mara baada ya kufundishwa na mwalimu.

“Nilikuwa na mzigo wa kutaka kuwalipa fadhila wazazi wangu ambao wananisomesha kwa kuhakikisha nafauli vyema mitihani yangu. Nilijiwekea ratiba ambayo sikuwahi kuivunja zaidi ya kubadili muda wa kusoma, nilihakikisha naifuata,” alisema.

Alisema sababu nyingine ni kuwaheshimu wazazi na walimu, ambao wamemuwezesha kupata elimu na kumuomba Mungu wakati wote.

“Darasani nilikuwa naongoza kila mara na nilikuwa na rafiki yangu Mohamed Omary ambaye nilishirikiana naye kila mara kufundishana masomo na amefaulu alama kama zangu za 1.7, hali ambayo inanipa furaha sana,” alisema.

Aliwataka wanafunzi wengine kutumia fursa na muda walionao wa kusoma kufanya hivyo ili kuwatia moyo na kuwalipa fadhila wazazi na walimu wao wanaowapatia elimu.

“Unaweza kuwa na walimu wazuri lakini usifaulu, lakini kama ukijitambua na kuamua kuwalipa fadhila wazazi wako unaweza kufanya vizuri hasa kwa shule ambazo mazingira yake ni mabaya,” alisema.

Rafiki yake, Mohamed Omary alisema, Innocent alikuwa na uwezo wa kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja na hasa uwezo wa kufikiri kwa haraka.

“Nilishirikiana naye lakini sikiwahi kumpita zaidi ya kuwa nyuma yake, sanasana nilikuwa nikimpita somo moja tu na hata matokeo haya tumepata alama sawa ni jambo la kufurahia,” alisema Mohamed.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake