ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, February 24, 2016

Sumaye: Ningefuta sheria ya kubadili Katiba



Waziri Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye
By Joyce Mmasi, Mwananchi jmmasi@mwananchi.com

Waziri Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye ameishauri Serikali ya Awamu ya Tano kufuta Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na kutunga ambayo itaunda timu ndogo ya wataalamu badala ya Bunge la katiba lenye watu zaidi ya 600 ambao hawana ujuzi.

Sumaye amesema Bunge la Katiba lenye watu 630 lisingeweza kuandika Katiba nzuri na hivyo akashauri kuundwa kwa timu ndogo ya wataalamu ambayo itachambua Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyokuwa chini ya Jaji Joseph Warioba kwa kulinganisha na Katiba ya mwaka 1977.

Akizungumza na gazeti hili kwenye mahojiano maalumu ofisini kwake, Sumaye alisema utaratibu mzima wa kuendesha mchakato ule ulikuwa mbovu na kamwe usingeweza kufanikisha malengo yaliyokusudiwa.

Sumaye, ambaye mwaka jana alihamia kambi ya upinzani akitokea CCM, alisema kilichovuruga mchakato mzima ni kitendo cha kuwa na wajumbe wengi ambao wasingeweza kujadili vizuri na kutoka na Katiba bora, na kushauri kuundwa kwa timu ya wataalamu kati ya 20 na 30 kufanya kazi hiyo.

“Kwanza ni lazima Katiba ishughulikiwe. Hilo ni la msingi kabisa kwa sababu hatuwezi kuendelea na hii Katiba. Ukiendelea na hii Katiba, huwezi ukapata demokrasia ya kweli,” alisema alipoulizwa angemshauri nini Rais John Magufuli kuhusu kuendelea na mchakato wa Katiba.

“Mimi nina tatizo na katiba zote; ile ya (Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph) Warioba, na ile nyingine (ya mwaka 1977).”

Mchakato wa kuandika Katiba mpya ulikwama kwenye hatua ya kupiga kura ya maoni kuridhia Katiba Inayopendekezwa baada ya Tume ya Uchaguzi (NEC) kushindwa kukamilisha utoaji vitambulisho kwa wapigakura.

Bunge hilo lililoundwa na wabunge wote wa Jamhuri ya Muungano pamoja na wawakilishi kutoka makundi mbalimbali, liliingia dosari baada ya vyama vinne na baadhi ya wajumbe kujitoa kwa maelezo kuwa liliacha hoja za wananchi zilizokuwa kwenye Rasimu ya Katiba iliyoandikwa na Tume ya Warioba.

Kuhusu kukwama kwa mchakato huo, Sumaye alisema kama Bunge lingekuwa halijatunga Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2013, angetafuta kikundi cha watu wachache wataalamu ambao wangechambua Katiba ya zamani kwa kulinganisha na Rasimu ya Katiba kuona kama hoja za wananchi zinajibiwa, na pia kulinganisha na katiba za nchi nyingine kabla ya kupendekeza mpya.

“Haiwezekani ukapata katiba nzuri una watu 630 (kwenye Bunge), utapata vipi? Ndio maana nasema wale waliopitisha ile sheria, ambao ni Bunge lililopita, hawakuangalia mbele zaidi,” alisema.

“Katiba inatengenezwa na watu wachache wataalamu. Kina Warioba ni watu waliozunguka kupata maoni ya wananchi. Tunayo Katiba (ya zamani). Sasa ilitakiwa kundi la wataalamu wachambue Katiba iliyopo, kasoro zilizopo kama zinajibiwa na hoja za wananchi.

“Hoja nyingine za wananchi kwa zilikuwa na jazba kwa kiasi fulani. Mtu anasema wanaume wasitupige. Sasa hilo unaweza kuweka kwenye katiba? Kwa hiyo ilitakiwa wataalamu wachache, very sober people (watu makini), very experienced (wazoefu).”

Alisema Bunge la Katiba lenye uwakilishi mpana linatakiwa lifanye kazi ya kuhalalisha kile ambacho kitakuwa kimechambuliwa kwa kiasi kikubwa na kupendekeza kitu ambacho kitakuwa kizuri.

“(Bunge la Katiba) Si la kwenda kutengeneza Katiba. Bunge la watu zaidi ya 600 na umewapata kutoka kwa wafugaji, sijui makundi gani mengine, nani anajua Katiba?” alihoji. Alisema Bunge la Katiba linatakiwa likutane kwa siku zisizozidi tano kwa kuwa kazi kubwa inakuwa imeshamalizwa.

“Ingekuwa ni mimi, kwa kweli hii process (huu mchakato), kama unataka kuiendeleza, basi iendelee kwa utaratibu mzuri zaidi. Ninge-repeal (ningefuta) ile sheria, nilete sheria mpya ambayo ingesema sasa process iwe hivi, hivi, hivi,” alisema na kuongeza:

“That money is not completely sunk (fedha zilizotumika kwenye Bunge la Katiba hazijapotea zote). Kwa sababu tutatumia zile modules (Rasimu ya katiba na Katiba ya 1977), ingawaje kweli kipindi kile Bunge la Katiba fedha nyingi zilizopotea kuliko kama ingetumika kwa utaratibu huu.”

Alisema ni kwa sababu hiyo anashauri mchakato wa kupata Katiba mpya uanze kwa kufuta Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ili kuunda timu ndogo ya wataalamu itakayochambua katiba na rasimu.

No comments: