ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, March 9, 2016

Hospitali za rufani, mikoa ni majanga.

Wakati Rais John Magufuli akiwa ameanza kazi kwa kuelekeza nguvu kuhakikisha huduma za afya zinaimarika katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, huduma katika hospitali za rufaa na za mikoani hali ni mbaya zaidi, imefahamika.

Katika kitengo cha afya, Rais Magufuli alianza kwa kuhakikisha mashine ya ST-Scan, MRI, vitanda, magodoro pamoja na mashuka vinapatikana katika Hospitali ya Muhimbili.

Kadhalika, aliagiza kuhamishwa kwa Ofisi ya Wizara ya Afya iliyokuwapo Muhimbili na kuligeuza eneo hilo kuwa wodi ya wazazi ambao walikuwa wakilala wawili wawili na wengine chini.

Mbali na hilo, pia huduma ya maduka ya madaka chini ya Mamlaka ya Chakula na Dawa (MSD), yalifunguliwa hospitalini hapo ikiwa ni mkakati wa kuhakikisha wagonjwa wanapata dawa kwa urahisi na bei halali.

Hata hivyo, wakati Rais Magufuli akiendelea na juhudi hizo, uchunguzi wa kina uliofanywa Nipashe katika hospitali kubwa za mikoa na zile za rufaa, hali ni mbaya kutokana na kukosekana kwa huduma ya vipimo muhimu, wauguzi, madaktari na madaktari bingwa wa magonjwa mbalimbali.

Hospitali ya RUFAA Bombo
Katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga ya Bombo, ambayo ndiyo tegemezi na kimbilio la wakazi wa mkoa huo hasa kwa magonjwa ambayo yameshindikana kupatiwa matibabu hospitali za wilaya ama vituo vya afya, upatikanaji wa huduma si wa kuridhisha kutokana tatizo kubwa la ukosefu wa watumishi na vipimo muhimu.

Kwa upande wa daktari bingwa wa magonjwa ya akina mama, aliyepo ni mmoja tu huku kukiwa na upungufu mkubwa wa wauguzi wakunga zaidi ya 40.

Batrice Rimoyi ni Muuguzi Mfawidhi wa Hospitali ya Bombo, ambaye anasema kutokana na uhaba wa watumishi hasa kila muuguzi mkunga mmoja anaweza kuwa na wastani wa kuhudumia akina mama zaidi ya 24 kwa akiwa zamu ya saa nane.

Kwa mujibu wa Rimoyi ni kwamba kwa zamu moja takribani akina mama 48 wanapokelewa kwa ajili ya kujifungua ambao hudumiwa na wauguzi wawili tu wakati wastani wa kawaida ni kila muuguzi ama mkunga mmoja kumhudumia mama mmoja, jambo ambalo huwaweka katika wakati mgumu kwani baadhi hujifungua kwa njia ya upasuaji.

Kwa upande wao akina mama wajawazito wakizungumzia hali halisi ya upatikanaji wa huduma hospitalini hapo wanasema bado wanapata mashaka na usalama wa maisha yao hasa kwa kuzingatia kuwa daktari bingwa wa wanawake anayetegemewa ni hospitali nzima ni mmoja tu.

“Huko tunakotoka kuna vituo vya afya pia lakini tumepewa masharti kwamba mimba ya kwanza lazima uje Bombo au kama wewe huwa unajifungua kwa njia ya upasuaji unalazimika kuja huku sasa Daktari ni mmoja tu atuhudumia wote kimsingi tatizo lipo pale pale kuna watakaopona na kuna watakaopata madhara kutokana na hilo,” anasema Mariam Hamisi mmoja wa akina mama anayepata huduma hospitalini hapo.

Kadhalika changamoto kubwa iliyopo kwa sasa ni uhaba wa wauguzi na vitanda kutokana na wingi wa akina mama wanaopokelewa kupata huduma kwa siku hivyo hulazimika kulala hata watatu kitanda kimoja.

“Kulala bado mtindo ni ule ule watatu kitanda kimoja na vitoto vyenu labda wale waliopasuliwa siku ya kwanza utalala peke yako kesho yake wanaletwa wengine hili ni tatizo kwa sababu hata maradhi ni rahisi kuambukizwa,”alieleza Tumaini Hilali mmoja wa akina mama hao.

Kwa upande wa Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mwantumu Mahiza, akitoa taarifa ya hali ya Hospitali hiyo kwa Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, aliyekuwa katika ziara ya kikazi mkoani humo alisema hospitali hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo upungufu wa watumishi wa afya vitendea kazi na uchakavu wa majengo hatua ambayo inakosesha ufanisi wa kiutendaji na utoaji wa huduma bora za afya kwa wananchi.

Mahiza alitaja miongoni mwa vifaa vinavyokosekana hospitalini hapo na hivyo kuwakosesha wananchi kupata huduma bora za afya kwamba ni pamoja na vifaa maalum vya uchunguzi ikiwamo CT-Scan, Echo na vitendanishi vya maabara sambamba na uhaba wa wafanyakazi hasa wenye fani za ENT, upasuaji wa mifupa, macho na mionzi.
Mkuu huyo wa mkoa.

Akizungumzia hali hiyo na changamoto za jumla za utoaji wa huduma za afya kwa wajawazito Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dk. Asha Mahita anasema katika kukabiliana na hali hiyo wanaendelea kuboresha hospitali za wilaya na vituo vya afya ili kuhakikisha wanaweza kupunguza mlundikano wa wagonjwa katika hospitali hiyo ya rufaa.

HOSPITALI YA RUFAA Kitete
Katika Hospitali ya Rufaa Kitete mkoani Tabora, wajawazito walimpokea mwandishi wetu kwa kilio cha kusikitishwa na huduma duni hospitalini hapo hasa ukosefu wa dawa na vifaa tiba.

Akizungumza na Nipashe jana kwa niaba ya akina mama wenzake, Rukia Ally, alisema katika wodi yao wanalazimika kulala wawili kwenye kitanda kimoja pamoja na watoto wao baada ya kujifungua na wengine kulazimika kujifungulia chini.

Rukia alisema kutokana na hali hiyo na msongamamo uliopo katika wodi hiyo, kunasababisha kuambukizana magonjwa mbalimbali kwao na watoto.

''Sisi akina mama tunaolazwa hospitalini hapa inafikia wakati mwingine unatandika kanga na kulala chini ili kujiepusha na mbanano katika kitanda na mashuka kutoa harufu mbaya,” alisema Rukia.

Aidha, akina mama hao walimuomba Rais Magufuli majipu anayotumbua ya pesa kwa mafisadi akumbuke kununua vifaa katika hospitali ya Rufaa Kitete na kukarabati majengo.

Mganga Mkuu wa Mkoa katika Hospitali ya Kitete, Dk. Gunini Kamba, alithibitisha kutokuwapo kwa madawa ya kutosha, vifaa tiba na kuwapo kwa uchakavu wa majengo.

Alizungumzia wodi ya wazazi kuwa ni kweli kuna mrundikano wa akina mama, lakini jengo hilo lina miaka mingi na idadi ya wazazi inaongezeka siku hadi siku kutokana na kutokuwapo kwa hospitali za wilaya.

Katika wodi ya wazazi haiwezekani kuongeza vitanda kutokana na kutokuwa na nafasi ya kutosha na mlundikano unatokana na zahanati nyingi zilizopo mkoani kutokufanya kazi kwa saa 24, hivyo kusababisha wote kukimbilia hospitali ya mkoa.

Aidha, Dk. Kamba alisema vifaa ambavyo vipo lakini vingine ‘vimekufa’ ni x-ray ambazo zipo mbili lakini inayofanya kazi ni moja hali inayosababisha mrundikano wa wagonjwa wa vipimo hivyo.

Alisema kifaa kingine cha magonjwa ya ubongo cha CT-Scan ni muhimu kuwapo katika hospitali hiyo lakini hakipo.

HOSPITALI YA RUFAA DODOMA
Kipimo cha cha X-Ray katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, ni moja ya changamoto kubwa kutokana na kuharibika tangu Januari mwaka huu hali inayowalazimu wagonjwa kwenda Hospitali ya Mirembe.

Mmoja wa wagonjwa hospitalini hapo, Aisha Ramadhani, aliliambia Nipashe kuwa alimpeleka mwanawe ambaye amevunjika mguu lakini imewalazimu kwenda Hospitali ya Mirembe kupiga X–Ray, umbali takribani kilomita tano.

Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk. Zainab Chaula, alikiri wagonjwa wanaohitaji huduma ya X-ray kufuata nje ya hospitali hiyo huku akidai imetokana na kipimo hicho kuharibika tangu Januari 13, mwaka huu.

Alisema taarifa za kuharibika mashine hiyo tayari zipo mamlaka husika na kifaa hicho kimeagizwa nje ya nchi.

“Inayotakiwa kuleta X-ray ni Wizara ya Afya na ni mpango wa serikali kuzitengeneza zinapoharibika, na vifaa vyake havipatikani nchini hadi nje ya nchi, tunasubiri wizara ituletee,”alisema Dk. Chaula huku akiongeza kuwa pia hakuna vipimo vya MRI na CT-Scan.

Kadhalika Dk. Chaula alisema kuna upungufu wa watumishi 108 wa fani mbalimbali ikiwa ni pamoja na madaktari bingwa saba, madaktari wasaidizi tisa, maafisa wauguzi 15, wauguzi wa daraja la pili 22.

Hospitali ya Kanda ya Rufaa Mbeya

Katika Hospitali ya Kanda ya Rufaa Mbeya baadhi ya vipimo havipo zikiwamo mashine za CT-Scan na MRI hali ambayo inawafanya wagonjwa kukosa huduma inayohusu vipimo hivyo.

Akizungumza hali halisi, Kaimu Mkurugenzi wa hospitali hiyo, Thomas Isdory, alisema kati ya vipimo hivyo vikubwa, hospitali hiyo inayo mashine ya X-Ray pekee na kwambavingine viko katika mchakato.

Alisema kwa sasa wanafanya juhudi za kuhakikisha wanapata mashine ya CT-Scan kwa mkopo kutoka katika Shirika la Bima la Taifa ambalo alidai kuwa tayari wameshajaza fomu ya kuomba mkopo huo na kuipeleka wizarani kwa ajili ya kuidhinishwa.

Kwa upande mwingine, Isdory alisema tatizo kubwa linaloikumba hospitali hiyo ni upungufu wa madaktari bingwa pamoja na wafanya kazi wengine.

HOSPITALI YA RUFAA KCMC
Hospitali ya Rufaa ya KCMC ya Moshi, inakabiliwa na changamoto lukuki katika utoaji wa huduma bora za afya kwa wagonjwa wanaofikishwa katika hospitali hiyo, ikiwamo kukosa mashine ya MRI.

Mbali na kukosa huduma hiyo, mashine nyingine za uchunguzi za CT-Scan na mtambo wa upigaji picha za mionzi ya X-Ray zinafanya kazi kwa kiwango kidogo kutokana na kuzeeka.

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya KCMC, Dk. Gilliard Massenga aliliambia Nipashe kwamba kipimo hicho cha MRI kinapatikana peke yake katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MHN) na Hospitali nyingine za Rufaa za KCMC na Bugando hazina mashine hiyo.

“Tunasubiri ahadi ya serikali, maana walitueleza watatuletea, lakini sisi kimsingi hatuna mashine ya MRI, ila huwa tunawaandikia wagonjwa waende Muhimbili. Na kuhusu CT-Scan na X Ray, mitambo hiyo inafanya kazi taratibu mno.

Hiyo CT-Scan yenyewe ilinunuliwa kama mtumba mwaka 2006, kwa hiyo ina umri mkubwa na maisha yake siyo marefu kwa sasa,”alisema Dk. Massenga.

Mbali na changomoto hiyo, KCMC kwa sasa ina vitanda 585 tu, ambavyo kimsingi havitoshelezi mahitaji ya wagonjwa, ikilinganishwa na idadi ya wagonjwa wanaofika kupata matibabu.

Kwa mujibu wa Dk. Massenga, hospitali hiyo yenye jumla ya wauguzi 242, inakabiliwa na upungufu wa wauguzi 230 ili kukidhi mahitaji ya kuwa na wauguzi 472.

Aidha, kwa upande wa waganga wanaohitajika kukabiliana na changamoto ya wingi wa wagonjwa wanaofikishwa KCMC, walistahili kuwa na madaktari 164, lakini waliopo kwa sasa ni 62.

HOSPITALI YA RUFAA BUGANDO
Mkurugezi Mkuu wa Hosptali hiyo, Kieni Mteta, aliliambia Nipashe hospitali hiyo haijawai kuwa na mashine ya MRI huku ST-Scan tatu zipo ambazo zimeisha kwa kuwa uwezo wa kufanya kazi ni miaka 10 na zilizopo zina miaka 15, na kwamba katika bajeti yao ya 2016/2017 wameingiza mpango wa manunuzi wa mashine hizo zikiwemo za X Ray ambazo nazo zimeshachakaa.

Hospitali TEULE ya Tumbi
Hosptali Teule ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani, Tumbi ni kati ya hosptali zinazotegemewa sana hapa nchini kutokana na umuhimu wake wa kuhudumia wagonjwa mbalimbali hasa majeruhi wa ajali zinazotokea mara kwa mara katika Barabara ya Morogoro.

Hata hivyo hosptali hiyo iliyojengwa na shirika la Elimu Kibaha mwaka 1967 anakabiliwa na matatizo lukuki ikiwa ni pamoja na tatizo la chumba cha maiti.

Licha ya maiti nyingi zinazotokana na ajali kupelekwa hospitalini hapo, kuna tatizo la majokufu kwani lililopo ni moja tu ambalo linafanya kazi chumba kimoja chenye uwezo wa kubeba maiti nane.

Mkurugenzi wa Shirika la Elimu Kibaha, Cyprian Mpemba, anasema licha ya hosptali hiyo kupanda hadhi hadi kuteuliwa kuwa ya mkoa bado miundo mbinu yake ni ya kizamani na ina matatizo ya vifaa tiba, madawa na mashine mbalimbali za kumuhudumia majeruhi wa ajali.

Mganga Mkuu wa hosptali hiyo, Peter Dattani, kwa upande wake anasema kuna upungufu wa wauguzi na madaktari na pia vyoo vilivyopo havikidhi mahitaji ya sasa na kuwa hata chumba cha mapokezi hakitoshelezi mahitaji ya wingi wa idadi ya watu 500 kwa siku wanaofika kutibiwa katika hosptali hiyo.

Anasema upungufu wa mashuka nao ni changamoto nyingine inayoikabili hospitali hiyo.

Hospitali YA rufaa ya Mnazi mmoja Zanzibar
Kama ilivyo katika hospitali baadhi ya Tanzania Bara, matatizo hayo yanalandana na yanayoikabili ya ile ya Rufaa ya Mnazi Mmoja Zanzibar.

Licha ya Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein, tangu kuingia madarakani kufanya juhudi ili kuifanya hospitali hiyo ifikie kiwango cha kimataifa, bado upungufu wa dawa dawa, vifaa tiba, bajeti ndogo na kuchakaa kwa lifti ni tatizo linaloiandama hospitali hiyo.

Kwa mujibu wa Katibu wa Hospitali hiyo, Hassan Makame Mcha, alisema changamoto zinazoikabili hospitali hiyo ni mashine ya mionzi (X-ray) ambayo iliharibika muda mrefu.

“Wagonjwa wanaohitaji mashine ya X-ray kwa ajili ya kuchunguzwa maradhi yao inabidi wakafanye kipimo hicho katika hospitali nyingine binafsi,”alisema katibu huyo.

Aidha, alisema changamoto nyingine ni uhaba wa waunguzi jambo ambalo husababisha wauguzi waliopo kutokidhi haja ya kuwahudumia wagonjwa kutokana na idadi kubwa ya wagonjwa wanaofika hospitalini hapo.

Kadhalika, alisema chumba cha kuhifadhia maiti ni kidogo na jengo hilo ni la muda mrefu na halina barafu ya kutosha ya kuweza kumhifadhia maiti zaidi ya siku mbili.

Alisema changamoto nyingine ni uhaba wa madawa na vitanda vya kuwalaza wagonjwa na hufika wakati kitanda kimoja hulaza wagonjwa zaidi ya wawili.

Imeandaliwa na Lulu George,Tanga, Augusta Njoji, Dodoma, Nebart Msokwa, Mbeya, Godfrey Mushi, Moshi, Rose Jacob, Mwanza, Halima Ikunji, Tabora, Margaret Malisa, Pwani na Rahma Suleiman, Zanzibar
CHANZO: NIPASHE

No comments: