Kaimu Kamishna Mkuu wa TRA, Alphayo Kidata
Dar es Salaam. Mwenendo wa Serikali katika ukusanyaji mapato katika miezi minane ya awali ya mwaka wa fedha unaoishia Juni umetajwa na wataalamu wa uchumi kuwa ni dalili nzuri za Tanzania kujitosheleza kwa bajeti lakini wakieleza kuwa itachukua miaka mitano kufikia lengo la kupunguza utegemezi wa wahisani hadi asilimia tatu.
Maoni ya wataalamu hao yamekuja baada ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutoa ripoti ya mapato yaliyokusanywa kuanzia Julai 2015 hadi Februari mwaka huu kuwa yamefikia Sh8.569 trilioni ikiwa ni asilimia 99 ya malengo.
Kaimu Kamishna Mkuu wa TRA, Alphayo Kidata aliwaambia wanahabari jana kuwa kwa kipindi hicho walipanga kukusanya Sh8.685 trilioni lakini hawakufikia lengo kutokana na kushuka na kupanda kwa kodi na kuahidi kuwa hadi ifikapo Juni, watakuwa wamefikia asilimia 100 ya malengo kwa mwaka wa fedha 2015/16.
Katika mkutano huo uliolenga kutoa mwenendo wa ukusanyaji mapato, matumizi ya mashine za kielektroniki za utoaji risiti (EFD), kusitisha bei elekezi katika ukadiriaji wa kodi na usajili wa vyombo vya moto, Kidata alisema malengo kwa mwaka huu wa fedha ni kukusanya Sh12.3 trilioni katika bajeti ya Sh22.4 trilioni iliyopangwa mwaka 2015/16.
Ripoti hiyo inaonyesha kuwa sehemu kubwa ya mapato hayo ilichangiwa na makusanyo ya kuanzia Desemba 2015 ambayo TRA ilikusanya Sh1.4 trilioni na kufuatiwa na Januari (Sh1.07 trilioni) na mwezi uliopita Sh1.04 trilioni.
Kidata alisema kuongezeka kwa mapato hayo kunatokana na kudhibiti mianya ya ukwepaji kodi na kuweka mazingira rafiki kwa mlipakodi, kurekebishwa kwa misamaha ya kodi iliyokuwa inachangia upotevu wa mapato, kuongezeka kwa watumiaji wa EFD na kudhibiti eneo la forodha.
Profesa wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Humphrey Moshi alisema mwenendo huo ni chanya na unaonyesha iwapo Serikali itaendelea kusimamia mikakati yake ya ukusanyaji mapato, utegemezi “halisi” utapungua kwa asilimia nane.
“Ukifuatilia sehemu kubwa ya mapato hayo ni matokeo ya malimbikizo ya kodi yaliyolipwa miezi miwili iliyopita, hofu ya wafanyabiashara kwa Serikali mpya, kupungua kwa rushwa na wananchi kulipa kodi kwa hiari,” alisema Profesa Moshi.
Alitaka wigo wa ulipaji kodi utanuliwe kwa kuharakisha urasimishaji biashara na kupunguza misamaha ya kodi akisema jitihada hizo zitamsaidia Rais John Magufuli kupunguza utegemezi wa bajeti kwa wahisani hadi asilimia tatu.
Katika mpango wake wa bajeti ya mwaka wa fedha 2016/17, Serikali kupitia Waziri wa Fedha, Dk Philip Mpango ilibainisha mwezi uliopita kuwa utegemezi kwa wahisani utashuka hadi kufikia asilimia tatu kutoka asilimia 6.4 ya mwaka huu, jambo ambalo Profesa Moshi hakubaliani nalo.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Dhamana na Uwekezaji ya Zan Securities, Masumbuko Raphael alisema ufanisi umeongezeka katika ukusanyaji wa mapato kutokana na mabadiliko ya Serikali huku akionya ni mapema kubashiri mafanikio makubwa kwa kutumia viashiria vya makusanyo ya kodi ya miezi mitatu.
“Kama jitihada zilizopo zikiendelea mpaka mwisho wa mwaka na njia mpya za ukusanyaji mapato zikianzishwa, tutakuwa na uhakika mkubwa kuwa sasa tunaweza kujitegemea kwa asilimia 100 ukilinganisha na miaka iliyopita,” alisema Raphael.
Hoja hiyo iliungwa mkono na mtaalamu wa uchumi, Hussein Kamote aliyesema kitendo cha kufikia lengo kwa asilimia 99 kwa miezi minane ya awali ya mwaka huu kinatoa picha nzuri ukilinganisha na hali ya miaka ya nyuma ambako TRA ilikuwa ikifikia lengo hadi asilimia 75 tu.
“Nchi yoyote inajivunia kujitegemea kwa mapato yake ya ndani. Utegemezi wa misaada haufai,” alisema Kamote ambaye pia ni Mkurugenzi wa Sera na Ushawishi wa Shirikisho la wenye Viwanda Tanzania (CTI).
“Naamini hali ikiendelea hivi tutajitegemea lakini Serikali itafute vyanzo vingine vya kodi kama kusimamia VAT na kodi ya mashirika badala ya kutegemea ushuru wa forodha ambao ni rahisi kuyumba siku uingizaji wa bidhaa ukiporomoka.”
EFD 5,700 zanunuliwa
Kamishna wa Kodi za Ndani wa TRA, Yusuph Salum alisema mamlaka hiyo inaendelea kugawa mashine za EFD bure kwa wafanyabiashara wadogo ambao uwezo wa kununua mashine hizo unaweza kuathiri mitaji yao ya biashara na kwamba tayari wameshakamilisha ununuzi wa mashine za uniti 5,700.
Usajili wa magari
Kidata alisema TRA, imefanya ukaguzi na kubaini kuwepo kwa magari ambayo yaliingizwa nchini na kusajiliwa bila kufuata taratibu za forodha hivyo kuyafanya yamilikiwe bila kulipiwa kodi stahiki. Sehemu kubwa ya magari hayo, alisema yaliingizwa kutokana na matumizi mabaya ya misamaha ya kodi.
Kufuta bei elekezi
Katika hatua nyingine, Mamlaka hiyo imefuta bei elekezi katika mchakato wa uthaminishaji wa bidhaa bandarini kwa sababu ni kinyume cha sheria ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na kwamba TRA itaendesha shughuli za forodha kulingana na sheria husika.
“Tumeona bei elekezi haisaidii kwa sababu uingizaji wa bidhaa unatawaliwa na sheria ya Afrika Mashariki ambayo Tanzania ni wanachama, hivyo Mamlaka itadhibiti ukaguzi na uthaminishaji halisi ili kila mfanyabiashara alipe ushuru na kodi kulingana na thamani ya bidhaa husika,” alisema Kidata.
No comments:
Post a Comment