Siku ya hali ya hewa duniani huadhimishwa kwa utamaduni wa kuchagua kauli mbiu. Kwa mwaka huu wa 2016, kauli mbiu ni ‘ Joto kali, Ukame, Mafuriko; Kabiliana na mabadiliko”-“Hotter, Drier, Wetter - Face the future’. Kauli mbiu hii inahusiana na mabadiliko ya hali ya hewa na inaweka msisitizo wa kukabiliana na changamoto zinazotokana na mabadiliko ya hali ya hewa siku za mbeleni.
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inatekeleza majukumu yake ya kitaalamu kwa kufuata miongozo ya Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO). TMA inatekeleza jukumu hilo kwa niaba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. TMA huwa katika mstari wa mbele katika kuadhimisha siku ya hali ya hewa Duniani – World Meteorological Day (WMD). Hii ni pamoja na kuhamasisha matumizi ya taarifa za hali ya hewa nchini na pia kuadhimisha mafanikio ya Shirika la Hali ya hewa Duniani ambayo yanapatikana kupitia taasisi za hali ya hewa kote Duniani ikiwemo TMA. Aidha ni siku pia ya kuadhimisha mafanikio ya Mamlaka ya Hali ya Hewa na kuhamasisha utekelezaji wa majukumu muhimu ya kuiwezesha Mamlaka kuongeza ubora wa huduma za hali ya hewa zitolewazo kwa jamii. Mamlaka ya Hali ya Hewa ina jukumu kubwa la kusimamia masuala yote yanayohusiana na hali ya hewa hapa nchini ikiwa ni pamoja upimaji wa hali ya hewa, ukusanyaji na uhifadhi wa taarifa za hali ya hewa pamoja na kuzisambaza kwa watuamiaji mbalimbali.
Mamlaka inatoa huduma za hali ya hewa kwa sekta na wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na sekta za kilimo, nishati,maji,afya, usafiri wa nchi kavu, usafiri wa baharini,mito na maziwa, usafiri wa anga ndani na nje ya nchi na kushiriki katika kubadilishana taarifa za hali ya hewa kimataifa kwa usalama wa wananchi na mali zao na kuboresha uelewa wa hali ya anga la dunia.
Katika kutimiza lengo la kutoa huduma bora kwa jamii, Mamlaka inashirikiana na mashirika na taasisi nyingine za ndani na nje ya nchi katika utekelezaji wa shughuli pamoja na program za mashirika mbalimbali ya kimataifa hususan Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) na Shirika la Usafiri wa Anga (ICAO).
Hali ya hewa itaendelea kubadilika kwa miongo ijayo kwa kadri ambavyo shughuli za kibinadamu zitaendelea kufanyika na kusababisha ongezeko la gesi joto katika anga.
Kwa miongo kadhaa iliyopita joto la wastani la kila mwaka limekuwa likiongezeka zaidi ikilinganishwa na mwaka uliotangulia. Taarifa za nchi mbalimbali ikiwemo Tanzania zimekuwa zikionyesha kuwa viwango vya juu na vya chini vya joto vimekuwa vikiongezeka. Matukio ya hali mbaya ya hewa kama vile ukame na mafuriko yamekuwa yakitokea katika sehemu mbalimbali duniani. Mabadiliko haya ya hali ya hewa yamekuwa yakibadilisha mifumo ya asili ya misimu na ongezeko la ukubwa wa matukio ya hali mbaya ya hewa. Kama vile joto kali, ukame na mvua nyingi. Mabadiliko haya yanaendelea kuchangia kuwepo kwa Joto kali, Ukame, Mafuriko katika nyakati zijazo. Kwa upande wa nchi yetu, El NiƱo iliyojitokeza mwaka 2015 na kuendelea hadi mwaka huu 2016 ilisababisha ongezeko kubwa la joto hapa nchini. Viwango vya joto vilivyojitokeza vilifikia hadi nyuzi joto 36 hususan katika maeneo ya ukanda wa Pwani na yale ya Nyanda za juu Kaskazini Mashariki, kiwango ambacho ni cha juu ya wastani kwa takribani nyuzi joto 1.7 hadi 2.0. Tofauti hiyo ya hali ya joto ni kubwa ikilinganishwa na viwango vilivyowahi kupimwa katika miaka mingi iliyopita katika kipindi hicho. Kwa mujibu wa taarifa za Shirika la Hali ya Hewa duniani (WMO) ongezeko la joto pia limejitokeza katika maeneo mengine duniani.
Katika kuadhimisha siku hii ya hali ya hewa Duniani mwaka huu, TMA inaitumia siku hii kwa kuuhamasisha umma kutembelea vituo vya hali ya hewa vilivyopo nchi nzima ili kufahamu huduma zitolewazo, kujifunza na kuona ni jinsi gani wanavyoweza kufaidika na huduma hizi katika maisha yao na shughuli za kila siku kwa maendeleo endelevu ya Taifa letu. Aidha, watumishi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa watapanda miti katika siku hii kuonyesha umuhimu wa kutunza mazingira kama njia mojawapo ya kukabiliana na mabadiliko. Leo Jumuiya ya kimataifa ya hali ya hewa duniani kote inaadhimisha Siku ya Hali ya Hewa Duniani. Siku hii ni kumbukumbu ya kuanzishwa kwa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) tarehe 23 Machi 1950. Tanzania pamoja na wanachama wengine 190 wa Shirika hili inaungana na jumuiya ya kimataifa kusherehekea siku hii kwa kuonesha mchango wa huduma za hali ya hewa katika kulinda usalama wa jamii.
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ilianzishwa mnamo Desemba, 1999 baada ya Serikali kuchukua uamuzi wa kuboresha utoaji wa huduma kwa sekta mbali mbali muhimu chini ya sheria ya Wakala wa Serikali No. 30 ya 1997. Kabla ya TMA huduma hizi zilikuwa zikitolewa na iliyokuwa Idara Kuu ya Hali ya Hewa (DoM) chini ya iliyokuwa Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi.
Katika kusherehekea Siku ya Hali ya Hewa Duniani ni desturi kuwa na kaulimbiu ya maadhimisho ya kila mwaka, hivyo kwa mwaka huu kaulimbiu ya maadhimisho haya ni “ Joto kali, Ukame, Mafuriko; Kabiliana na Mabadiliko”-“Hotter, Drier, Wetter - Face the Future’. Kaulimbiu hii ni ya muhimu kwa kipindi hiki ambacho jamii nyingi nchini Tanzania na kwingineko duniani wanakabiliana na matukio ya hali mbaya ya hewa ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa joto kupita wastani na kubadilika kwa mifumo na misimu ya mvua. Hali hii ni dhahiri kwani jamii zetu nyingi zimeathirika kwa namna moja au nyingine kutokana na matukio haya ya hali mbaya ya hewa ambayo tafiti za kisayansi zimeyahusisha na mabadiliko ya hali ya hewa na tabia nchi.
Katika miongo ya hivi karibuni, mabadiliko ya hali ya hewa yameathiri mifumo ya asili na ya kibinadamu katika nchi nyingi. Mabadiliko ya matukio ya hali mbaya ya hewa ya muda mfupi na mrefu nidhahiri na hali hii inakaribia kuzoeleka na kuwa kama wastani mpya wa hali ya hewa katika nchi nyingi ikiwa pamoja na Tanzania. Katika miaka ya hivi karibuni Tanzania imeshuhudia athari za maafa yanayosababishwa na mabadiliko haya ya hali ya hewa yakiwa na sura mbalimbali. Mfano, tokea maadhimisho ya siku ya hali ya hewa ya mwaka uliopita tumeshuhudia matukio yaliyosababisha maafa yaliyotokana na mafuriko kwa mfano Mikoa ya kati ya nchi ambapo baadhi ya watu walipoteza maisha pamoja na mifugo na uharibifu wa mali. Tafiti za kisayansi na upimaji wa hali ya hewa zinaonyesha kuwa mabadiliko ya hali ya hewa yameendelea kuwa changamoto kubwa na inapasa kuangaliwa kwa makini na nchi zote. Joto la anga na bahari linaendelea kuongezeka, kuyeyuka kwa barafu kwa maeneo ya milima mirefu na yale ya ncha za dunia, kuongezeka kwa kina cha bahari na matukio ya hali mbaya ya hewa yamekuwa yakirudia mara kwa mara na kuongezeka makali. Kwa upande wa Tanzania, madhara yaliyokwisha kujitokeza kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa kwa uchache ni pamoja na ongezeko la joto, mafuriko ya mara kwa mara, ukame, mabadiliko ya misimu ya mvua, kuzama kwa baadhi ya visiwa vidogo vidogo, mmomonyoko wa kingo za bahari kutokana na kuongezeka kwa kina cha bahari, kupungua kwa barafu katika mlima Kilimanjaro, kupotea kwa baadhi ya viumbe hai, kuongezeka kwa magonjwa yanayohusiana na hali ya hewa kama vile malaria hata kwa maeneo ambayo hayakuwahi kuwa na matukio ya magonjwa haya.
Ripoti za Jopo la Kimataifa la Tafiti za Kisayansi za Mabadiliko ya Hali ya Hewa “Intergovernmental Panel on Climate Change (IPCC)” zinaonyesha kuwa kwa kiwango kikubwa kabisa shughuli za kila siku za binadamu zimechangia katika mabadiliko ya hali ya hewa na kuwa gesi joto kama vile “Carbon Dioxide- CO2” zimeendelea kuongezeka kufikia viwango vya juu kabisa katika historia ya mwanadamu. Kuendelea kutegemea vyanzo vya nishati vinavyozalisha kwa wingi gesi joto hizi kama ilivyo sasa kutasababisha joto la dunia kuendelea kupanda zaidi na ifikapo mwishoni mwa karne hii hali ya joto inaweza kuongezeka kufikia digrii 4 kwa kipimo cha Celsius juu ya wastani kulinganisha na joto wakati wa kabla ya mapinduzi ya viwanda. Kuzuia ongezeko la joto kuwa chini ya digrii 2 bado ni jambo linalowezekana ila inahitaji upunguzaji wa haraka wa gesi joto hizi. Hali ilivyo sasa wastani wa joto wa kila muongo mmoja umekuwa na joto zaidi kulinganisha na uliopita.
Takwimu za hali ya joto la wastani la dunia zinaonyesha kuwa, kipindi cha mwaka 2011 hadi 2015 kimekuwa na joto kali zaidi kulinganisha na vipindi vingine tokea kuanza kwa vipimo hivyo katika miaka ya 1800. Kwa ujumla ongezeko la joto linahusishwa na kuongezeka kwa gesi joto. Mwezi Disemba 2015 wakati wa Mkutano wa kimataifa wa ishirini na moja (21) ambazo zilijadili mabadiliko ya hali ya hewa na namna ya kukabiliana nayo “(Twenty First Conference of Parties (COP 21))” uliofanyika Jijini Paris, Ufaransa, nchi za dunia kwa kauli moja walikubaliana kupitisha makubaliano ya Paris “ Paris Agreement”. Makubaliano haya yanalenga kupunguza uzalishaji wa gesi joto kwa kiasi kikubwa. Haya ni makubaliano ya kihistoria ambayo yanazilazimu nchi zote za dunia kuwa na mpango na juhudi mahsusi kupambana na janga la mabadiliko ya hali ya hewa kwa pamoja kulingana pia na kiwango cha uzalishaji wa gesi joto wa kila nchi, yaani “common but differentiated responsibilities”.
Tunapojiandaa kukabiliana na hali ya baadae ya mabadiliko haya ya hali ya hewa, kila mmoja wetu ana mchango na jukumu la kufuatilia kwa karibu, kuelewa na kukabiliana na hali ya hewa ilivyo leo na itakavyokuwa siku zijazo. Tuendelee kuelimishana kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa na namna ya kukabiliana nayo wakati huo huo tukiendelea kutekeleza sera ambazo zitatusaidia sasa na siku zijazo. Sambamba na jitihada hizi jumuiya ya hali ya hewa ya kimataifa kupitia Shirika la Hali ya Hewa Duniani (World Meteorologica Organization-WMO) inatekeleza programu kama ile ya Global Framework for Climate Services (GFCS) yenye lengo la kuwezesha jamii kukabiliana vilivyo na kuchangamkia fursa zinazotokana na mabadiliko ya hali ya hewa hususani kwa zile jamii zilizo katika hatari ya kuathirika zaidi.
Serikali yetu inaendelea kujenga uwezo wa kufuatilia kwa karibu mifumo ya utabiri wa hali ya hewa ya muda mfupi na mrefu ambapo taarifa hizi zitasaidia katika kutoa maamuzi mbalimbali na kuandaa sera kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa. Taarifa na huduma zinazotokana na utabiri wa muda mrefu wa hali ya hewa utaongeza uwezo wa kumaliza au kukabiliana na mabadiliko haya pamoja na kuleta maendeleo endelevu, hivyo kutufanya kuwa mahali pazuri zaidi katika juhudi za kukabiliana na madhara yatokanayo na mabadiliko ya hali ya hewa kama vile mvua nyingi kupita wastani, mafuriko na ukame; pia itasaidia wakulima kupanga vema shughuli zao za kilimo; kuongeza usalama wa usafiri wa maji na anga.
Kwa kuzingatia maendeleo haya, ni rai yangu kwa kila mwananchi kutimiza wajibu wake katika kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa na athari zake na hivyo tutakuwa tumetoa mchango mkubwa katika kuleta usalama na ustawi wa kila mwananchi wa Taifa letu.
Mabadiliko ya hali ya hewa yanatufanya tushindwe kuwa na uhakika wa mustakabali wetu, hata hivyo jambo moja ni dhahiri kuwa jamii yetu inalo jukumu la kugeuza hali hii, si kwa ajili yetu pekee bali kwa vizazi vijavyo pia. Maamuzi tunayofanya sasa yana matokeo makubwa na yanaweza kubadilisha hali ya baadae ya dunia tunamoishi. Changamoto hizi ni kubwa ila fursa zilizopo za kubadilisha hali ya mambo ni nyingi pia.
Wakati tunaadhimisha siku hii, nawasihi wadau wote wa hali ya hewa katika sekta mbalimbali kujihusisha zaidi katika kuelewa na kufuatilia masuala ya hali ya hewa na mabadiliko yake ili kuweza kuchukua hatua stahiki za kujikinga na kukabiliana na athari zitokanazo na mabadiliko ya hali ya hewa. Kwa kufanya hivyo tutasababisha mazingira tunayoishi yaendelee kubaki katika asili yake na yenye kuvutia kwa shughuli za kiuchumi na kijamii kwa kizazi hiki na vizazi vijavyo.
Nawatakia madhimisho mema na yenye mafanikio ya siku ya Hali ya Hewa Duniani
“Joto kali, Ukame, Mafuriko; Kabiliana na Mabadiliko
No comments:
Post a Comment