ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, March 24, 2016

Mtego wa ufisadi unaoisubiri Ukawa.

Baada ya vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kushinda nafasi ya Meya wa Jiji la Dar es Salaam na ile ya Manisapaa ya Kinondoni na Ilala, wananchi wengi wanataka kuona mabadiliko kati yao na wakati wa uongozi uliopita chini ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Mbali na matarajio hayo ya wananchi, kauli za viongozi wa Ukawa kusema kuwa kuna ufisadi kwenye mikataba mbalimbali ukiwamo ule wa Shirika la Usafirishaji Dar es Salaam (Uda), zabuni mbalimbali zikiwamo za kusomba taka, upangishaji nyumba za Jiji na kuuza maeneo ya wazi, ni kati ya mambo ambayo yanatarajiwa kupatiwa ufumbuzi.

Kadhalika, baadhi ya vitu ambavyo vimekuwa vikizua maswali mengi juu ya uhalisia wake ni pamoja na makusanyo ya mapato mbalimbali kama ya Soko la Kariakoo.

Licha ya soko hilo kuwa na wafanyabiashara wengi, imeelezwa kuwa linakusanya wastani wa Sh. milioni 180 kwa mwezi kutoka kwa wazabuni wanaokusanya mapato, hali inayoonyesha kuwa bado soko hilo linakusanya fedha kidogo kinyume cha matarajio ya serikali.

Pia, fedha zitokanazo na mabango, ni kitendawili kingine ambacho licha ya kuwapo kwa mabango ya matangazo, inaelezwa kuwa fedha nyingi huingia kwenye mifuko ya wajanja.

Meya wa Kinondoni, Boniface Jacob, Februari 16, mwaka huu, aliwaleeza waandishi wa habari kwamba Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni imekuwa ikipoteza Sh. bilioni 11 kila mwaka kutoka katika vyanzo vya mapato vya mabango makubwa ya matangazo.

Alisema upotevu wa fedha hizo ulikuwa ukitokea kila mwaka kupitia kampuni 12 za matangazo makubwa ambazo hushirikiana na watumishi wa manispaa hiyo.

Alisema tangu alipoingia katika uongozi wa manispaa hiyo, wamebaini udanganyifu mkubwa uliokuwa unafanywa na walipa ushuru, jambo lililosababisha kufanya utafiti.

“Hapo awali Manispaa katika vyanzo vyake vya mapato kupitia ushuru wa mabango, tulikuwa tukikusanya Sh. bilioni 2.5 kwa mwaka, lakini tulikuwa tukilaumiwa kwa kukusanya kiasi kidogo, ila kwa sasa tumegundua katika ukusanyaji huo hata robo tulikuwa hatufikii,” alisema na kuongeza:

“Hayo mabango mnayoyaona barabarani yalikuwa na udanganyifu wa vipimo pamoja na idadi kwa kila kampuni, tumepitia mabango yote katika manispaa hii na idadi yote tunayo na tumeyapima upana pamoja na urefu, tumegundua tulikuwa tukipoteza zaidi ya Sh. bilioni 11.5 kwa mabango makubwa na kwa kampuni za mabango madogo tulikuwa tunapoteza Sh. milioni 662.”

Wakati danadana za kumpata Meya wa Jiji zikiendelea, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, aliwahi kunukuliwa na vyombo vya habari akisema:

“Hii ni mikakati ya makusudi ya wenzetu wa CCM na serikali kuficha ufisadi ambao umefanyika ndani ya Jiji la Dar es Salaam. Wanaogopa viongozi kutoka upinzani watakwenda kuyatibua.

“Kuna ufisadi mkubwa wa (Uda), viwanja vya Jiji na kuna wizi mkubwa wa kandarasi jijini. “Tuna taarifa juu ya maandalizi ya kuvunja baraza la madiwani ili kuundwa tume itakayoongoza Jiji la Dar es Salaam. Mpaka sasa umefanyika mkakati wa makusudi wa kuigawa Manispaa ya Ilala na Kinondoni ili kuvunja nguvu ya Ukawa.”

Mbali na Mbowe, Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Jacob, naye alinukuliwa akisema: “Katika halmashauri hizi, CCM wana maslahi mapana, kuna mikataba hewa ambayo ilikuwa ikiwanufaisha wao siyo manispaa. Wanajua tukiingia tutaweka wazi kila kitu pamoja na kufuta mikataba hiyo.”

Kashfa ya uuzwaji wa Uda ambayo inahusishwa na vigogo wa CCM, imewahi kufikishwa katika Bunge la 10 ingawa iliyeyuka katika mazingira ya kutatanisha.

Kashfa hiyo pia iliyokuwa imeshikiwa bango na wabunge wa CCM, ilifanya wa chama hicho na madiwani kukosoana, hatua iliyofanya aliyekuwa Meya wa Jiji, Dk. Didas Massaburi, kuwaambia wanafikiria kwa kutumia 'makalio'.

Jana, Meya wa Kinondoni, Jacob aliliambia gazeti hili kuwa kuna madudu mengi ambayo wameyagundua tangu waingie madarakani, lakini kwa sasa ni mapema kuyasema.

“Huwezi ukaweka kila kitu hadharani sasa hivi, muda ukifika kila kitu kitakuwa hadharani, lakini ni madudu mengi tumeyagundua na tutayatumbua tu,” alisema Jacob.

Juzi baada ya kuchaguliwa, Meya wa Jiji Isaya Mwita, alisema baadhi ya mambo atakayoshughulikia kwenye uongozi wake ni changamoto ya foleni.

Pia, uchafu ambao alisema Jiji la Dar es Salaam likilinganishwa na mengine ya Afrika Mashariki, linaongoza kwa uchafu, ambalo nalo atalishughulikia.

“Kuna tatizo la bodaboda, nafahamu kilio chao, mama ntilie hawana maeneo, lakini wale wanaoishi mabondeni nitaangalia namna gani ya kuwezesha waendelee kuishi Dar es Salaam,” alisema.

Alisisitiza kuwa Jiji halitaendelea endapo migogoro ya muda mrefu ya kiitikadi haitaisha.

“Nataka kuona si CCM, Chadema au CUF, bila kujali itikadi za vyama vyao, wote tunafanya kazi kwa pamoja ili kuwaletea wananchi maendeleo. Hii ni mara ya kwanza Jiji hili linashikiliwa na upinzani, kwa hiyo kazi kubwa niliyonayo ni kuhakikisha miaka mitano ijayo maendeleo yanapatikana. Nawaomba wananchi watupe ushirikiano,” alisema.
SOURCE: NIPASHE

1 comment:

Anonymous said...

Asante Mameya wa Jiji letu. Sio hayontuu tunaomba mshirikiane na Serikali kuona jinsi gani haya maegesho ya magari yaliyo mengi sana hizo hela zinaenda wapi ni mkononinmwa mtu mmoja na analipa kodi kiasi gani kwani hata mishahara ya wahudumu wanaopigwa jua kila leo mvua, vumbi ni mdogo kupindukia na manyanyaso mengi. Maegesho ya magari na maliponyake yanaweza kuendesha jiji sana na kwa ukamilifu. Mabasina malori yanayoingia jijini pande zote bora wawekewe kiwango maalumu hiyo ni hela pia ya kuendeleza jiji. Msisubiri Rais kulisemea hili fanyeni kazi. Tunapenda pia kuwe na vyoo maalumu na safi kwa wateja sio kujisaidia pembezoni na akikutwa yeyote ni faini. Wafanya biashara kila kona kama mnavyozungumzia Kariakoo tuna masoko kibao. Kama mfanyabiashara ana duka analolipia kodi ni kwa nini basi atoe biashara yake nje kwenye njia za kupita watu?? Maeneo ya mbele ya maduka yasiwe ya kufanyia biashara na akifanya hivyo alipishwe faini ili iache. Tunahitaji wananchibwatembea kwa mguu wawe huru hata ukidondosha shilingi uione na kuichukua.!! Kazi mtindo mmoja. Mradi wa mabasi ya kasi iwe marufuku mtu kuweka biashara kwenye vituo au barabarani. Mabadiliko yawepo usiwe mtego! Kwanininkutegeana.