Mtoto wa siku moja ameibwa katika mazingira ya kutatanisha katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando, akiwa pembeni mwa mama yake aliyekuwa amelala, mwenye umri wa miaka 16.
Akizungumzia uporaji huo jana, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Justus Kamugisha, amesema aliyepora mtoto huyo aliingia ndani ya wodi ya wazazi ya Hospitali ya Rufaa ya Bugando, akiwa amejifunga ushungi.
“Alipoingia wodini alikuta mama wa mtoto amesinzia akiwa peke yake wodini, ndipo akamuiba mtoto wake wa kike mwenye umri wa siku moja na kuondoka naye kwenda kusikojulikana,” alisema.
Kwa mujibu wa Kamanda Kamugisha, Jeshi la Polisi limeanza uchunguzi wa tukio hilo kwa kuhoji wauguzi, walinzi na wazazi waliokuwa wamelazwa wodini hapo.
Katika hatua nyingine, Kamanda Kamugisha amesema Jeshi la Polisi mkoani humo, litaanza kufanya uhakiki wa silaha kuanzia Aprili mosi hadi Juni 30 mwaka huu, katika ofisi za makamanda wa Polisi wa wilaya zote za Mkoa wa Mwanza.
Amesema uhakiki wa silaha ni wa kitaifa na utahusu wamiliki binafsi, kampuni binafsi na taasisi mbalimbali za Serikali na zisizo za kiserikali zinazomiliki silaha.
“Lengo ni kupata kumbukumbu ya uhalali wa umiliki wa silaha. Watu wote wanaomiliki silaha watii agizo hili bila kulazimishwa, ili tufanikishe uhakiki kwa wakati na tuimarishe usalama katika mkoa wetu,” alisema.
Aliwataka watu wanaomiliki silaha isivyo halali, kusalimisha silaha hizo wenyewe kwenye ofisi za Serikali na kwa wakuu wa Polisi wa wilaya (OCD) kabla ya muda wa uhakiki wa silaha kumalizika.
“Baada ya hapo tutafanya msako kabambe wa watu waliokaidi kuhakiki silaha zao,” alisema.
No comments:
Post a Comment