ANGALIA LIVE NEWS

Monday, March 14, 2016

Watanzania nje waanzisha kampeni serikali kutolipa mabilioni Uingereza

Wakati Benki Kuu (BoT) ikiwa bado haijasema kama itaitoza faini Benki ya Stanbic Tanzania kutokana na kashfa ya Sh, bilioni 12, zilizotokana na mkopo wa dola za Marekani milioni 600 zilizokopwa benki ya Standard ya Uingerea, Watanzania waishio nje ya nchi wameanzisha kampeni ya kutaka uchunguzi ufanywe upya na Taasisi ya Kuchunguza Rushwa Kubwa ya Uingereza (SFO), ili ikibidi Tanzania isilipe mkopo huo.

Mpaka sasa, Watanzania 850 wametia saini waraka maalumu wa kutaka SFO ifanye tena uchunguzi wa suala hilo kati ya 10,000 wanaotakiwa.

Kati ya waliotia saini ni Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe, Mbunge wa Mbinga Mjini, Sixtus Mapunda na Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, Makongoro Nyerere.

Katika kuhamasisha Watanzania wengi zaidi kutia saini waraka huo, Zitto alisema deni la nje la taifa limefika Sh. trilion 30 na kwamba kila mwaka kutokana na ukubwa wa deni hilo, taifa kila mwaka hulipa takribani Sh. trilioni 2.2.

“Kati ya madeni hayo kuna ambayo yamepatikana kwa rushwa na mengine yamechukuliwa kwa matumizi ya anasa tu. “Moja ya madeni ya ovyo ni la dola 600, ambalo Tanzania ilikopa kutoka Benki ya Standard ya Uingereza kupitia hati fungani,” ilieleza taarifa hiyo.

Taarifa hiyo ya Zitto ilisema SFO imeonyesha kuwa mkopo huu ulipatikana kwa rushwa na kwa mujibu wa taasisi ya Corruption Watch ya Uingereza, Tanzania imepata hasara ya takriban dola milioni 80 (zaidi ya Sh. bilioni 160) kwa kuchukua mkopo huo.

Iwapo uchunguzi ungegundua kuwa Benki ya Standard ilihusika moja Kwa moja na hongo hiyoi, Tanzania ingefutiwa deni lote na kuokoa fedha nyingi ambazo zingewekezwa kwenye sekta za elimu, afya na maji.

“Tunataka Benki ya Standard ichunguzwe upya na SFO kuhusu tuhuma za rushwa ili kupata biashara Tanzania hati fungani ya dola milioni 600,” ilieleza taarifa hiyo.

Zitto alibainisha kuwa ikigundulika kuwa mabosi hao walishiriki, Tanzania itafutiwa deni lote kwa sababu benki hiyo itawajibika kurudisha fedha za watu kwa kuwa hati fungani itaonekana ni batili.

Alisema Tanzania itaanza kulipa deni hilo kuanzia Aprili, mwaka huu, na iwapo deni hilo litalipwa, juhudi za Rais John Magufuli kupata mapato zitaathiriwa na sekta nyeti kama elimu, afya na maji zitakosa bajeti ya kutosha.

Katika ukurasa huo, alisisitiza kuwa: “Ewe Mtanzania ungana na Watanzania wenzako duniani kutaka SFO ifungue uchunguzi kwa kuzingatia ushahidi mpya dhidi ya Benki ya Standard ambayo sasa inaitwa ICBC plc.”

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Ashatu Kijaji, akitolea ufafanuzi wa azma ya BoT kuitoza faini Benki ya Stanbic Tanzania kutokana na kashfa hiyo, katika kikao cha 10 cha bunge la 11, alisema sheria inaitaka benki ya Stanbic kutoa utetezi katika kipindi cha siku 20 ambazo zimeisha tagu wapewe kusudio hilo.

Alisema endapo BoT haitaridhika na utetezi wa Stanbic, italazimika kulipa faini hiyo.

Novemba 30, mwaka jana, Mahakama ya Crown Southwark ya jijini London, Uingereza, iliamuru serikali ya Tanzania irejeshewe dola za milioni sita (sawa na Sh. bilioni 12.6) kutokana na kubainika kuwapo kwa udanganyifu baada ya kesi hiyo kufunguliwa kwenye mahakama ya kwamba asilimia moja ya mkopo huo ambayo ni dola milioni sita zililipwa kwa Kampuni ya EGMA.

EGMA ni kampuni ya Kitanzania iliyohusika na uwezeshaji wa upatikanaji wa mkopo wa serikali wa Sh. trilioni 1.3 na inatuhumiwa kupokea kiasi cha Sh. bilioni 12 kama rushwa kwa kuwezesha upatikanaji wa mkopo huo.

Wanaotuhumiwa katika sakata hilo ni mmiliki wa EGMA ambaye alikuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Harry Kitillya; Ofisa Mtendaji Mkuu wa zamani wa Stanbic Tanzania, Bashir Awale; aliyekuwa Mkuu wa Uwekezaji wa benki hiyo, Shose Sinare; baadhi ya vigogo wa serikali ya Tanzania na maofisa wa Benki ya Standard ya Uingereza.

Kashfa yenyewe ilitokana na Benki ya Standard kukubali kuikopesha serikali ya Tanzania dola milioni 600 (Sh. trilioni 1.3) mwaka 2012 kwa masharti ya kulipwa riba ya asilimia 1.4, lakini Benki ya Stanbic Tanzania iliongeza asilimia moja, hivyo kufanya serikali kutakiwa kulipa riba ya asilimia 2.4.

Benki ya Stanbic iliyokuwa ikishughulikia suala hilo ikishirikiana na maofisa wa serikali ya Tanzania, ilidai nyongeza hiyo ilikuwa kwa ajili ya malipo kwa wakala, ambaye ni EGMA iliyopewa kazi ya kushauri mauzo ya hati fungani ingawa zilitumika kuhonga maofisa wa serikali.
SOURCE: NIPASHE

No comments: