Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Mbeya Mjini, Saadati Mwambungu pamoja na
wajumbe 19 wa kamati ya utendaji wa wilaya hiyo, wamevuliwa uongozi
baada ya kutuhumiwa kukihujumu chama.
Hatua hiyo ilifikiwa juzi
jioni na uongozi wa Chadema Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, chini ya
mwenyekiti wake, Dk Stephen Kimondo na Mratibu wa Kanda, Frank Mwaisumbe
na kuweka wilaya hiyo chini ya uangalizi wa uongozi wa Mkoa wa Mbeya
ndani ya siku 30 wakati wakiendelea na uchunguzi.
Mratibu wa
Chadema katika Kanda hiyo, Frank Mwaisumbe alisema jana
kuwa baada ya kufanyia kazi tuhuma 17 zilizowasilishwa kwao na
wanachama wa chama hicho wilaya, walibaini kuwa tuhuma saba kati yake
zina ukweli dhidi ya viongozi hao hivyo wakafikia uamuzi wa
kuwasimamisha na kuwataka kurudisha mali zote za chama hicho ndani ya
siku 30.
“Ni kweli jana (juzi) tulifika Kyela na katika kikao
chetu na kamati ya utendaji ya wilaya tulipowahoji ilionekana tuhuma
saba zina ukweli na baadhi ya watuhumiwa walikiri. Miongoni mwa tuhuma
hizo ni matumizi mabaya ya fedha na mali za chama, kutoshiriki vyema
Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana hadi tukapoteza jimbo, hususani siku ya
kuhesabu kura za jumla viongozi walikimbia.
“Siku ile ya
uchaguzi wa mwaka jana kuna vijana wetu walikamatwa wakituhumiwa kuvunja
ofisi pale halmashauri ya Kyela na wakahukumiwa, lakini hakuna kiongozi
yeyote ngazi ya wilaya aliyethubutu hata kwenda kuwaona pale gerezani
hadi walipojinasua wenyewe,” alisema Mwaisumbe.
Alisema kutokana
na mkutano wao wa juzi wajumbe wake kutotimia ili kufikia uamuzi halali
wa kuwachukulia hatua zaidi, uongozi wa Kanda uliamua kuwasimamisha na
chama kuwa chini ya mkoa, huku ukifanyika utaratibu wa kuitisha mkutano
mkuu ambao utawajadili kwa kina na kuona kama watafukuzwa moja kwa moja
au la.
Mwambungu alipoulizwa juu ya kutimuliwa kwao, alikiri
huku akisisitiza kwamba tuhuma zilizotolewa hazina ukweli wowote
kikatiba, na badala yake zimetengenezwa na ‘genge’ la watu wachache kwa
uchu wa madaraka, lakini hana kinyongo kusimamishwa uongozi kwa kuwa ipo
kikatiba ndani ya Chadema.
Alisema; “Kwanza ni heshima kwa kuwa
jambo hili lipo kikatiba. Lakini katika mkutano wa juzi akidi ya
wajumbe haikutimia kwani Chadema Wilaya ya Kyela ina wajumbe 349 wa
mkutano mkuu, lakini kwa juzi wajumbe waliohudhuria walikuwa 120 tu.
“Ndiyo
maana uongozi wa Kanda ulitoa siku 30 za kufanyika mkutano mkuu
utakaowajumuisha wajumbe wote 349 na ndipo itakapofahamika… kama ni
kufukuzwa au kuendelea na uongozi,” alisema.
Mwambungu
alisema kati ya wajumbe 19 wa kamati ya utendaji ya wilaya, wajumbe saba
waliamua kujiuzulu uongozi na baadaye wakaungana na wengine ambao
waliunda tuhuma hizo kwa lengo na kuuangusha uongozi ikiwa ni maandalizi
ya uchaguzi mwaka 2020.
No comments:
Post a Comment