Licha ya kupewa uzito mdogo kwenye sekta ya afya, virusi vya ugonjwa wa homa ya ini vinasambaa kwa kasi kuzidi virusi vya Ukimwi (VVU), wataalamu wameeleza.
Wataalamu hao wa afya wameeleza kuwa Tanzania inaongoza kwa kuwa na waathirika wengi wa ugonjwa huo katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Hayo yameelezwa jana katika mkutano maalumu wa madaktari wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) waliokutana kujadili ukubwa wa tatizo hilo na namna ya kukabiliana nalo.
Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) kutoka Marekani, Dk Brian Mcmahon alisema kwenye mkutano huo kuwa waathirika wa ugonjwa huo unaojulikana kitaalamu kwa jina la Hepatitis B ni zaidi ya watu milioni 250 ikilinganishwa na waathirika wa Ukimwi ambao ni milioni 33.
Kadhalika, takwimu hizo zinaonyesha kuwa wanaokufa kwa homa hiyo duniani wamefikia 600,000 kila mwaka.
“Kiwango cha maambukizi ya Hepatitis B ni kikubwa kwa sasa, kwa kuwa tayari kipo katika alama nyekundu ambayo si salama tena. Kinazidi asilimia nane ya tafiti zote zilizowahi kufanyika,” alisema.
Akielezea ukubwa wa tatizo hizo hapa nchini, daktari bingwa wa magonjwa ya mfumo wa chakula na ini kutoka Muhimbili, Dk Edwin Masue alisema Tanzania ina kiwango cha juu cha maambukizi hayo.
Alisema baada ya kufanyika kwa utafiti mdogo kwa kutumia wajawazito, wachangiaji damu na watu wanaoishi na VVU, imegundulika kuwa tatizo hilo ni kubwa.
“Hawa tunapata takwimu zao kwa sababu ni lazima damu zao zipimwe, lakini kiwango cha upimaji wa ugonjwa huu kwa hiari ni kidogo,” alisema.
Alisema ukubwa wa tatizo hilo umezua hofu na taharuki kwa sekta ya afya kwa kuwa wagonjwa wengi wanaogundulika kuwa na homa hiyo huwa wamefikia hatua mbaya.
Alisema wengi wanaoishi na homa ya ini, hawajui hali zao za kiafya kutokana uhaba wa vipimo vya kugundua mapema virusi hivyo hali kadhalika, ukosefu wa elimu.
“Maambukizi ya homa ya ini ni mara 100 zaidi ya VVU, kibaya zaidi ni kuwa hapa Tanzania hatuna bajeti iliyotengwa na Serikali ili tufikie nafasi nzuri. Pia, hatuna sera ambazo zinahusu ugonjwa huu na matibabu,” alisema.
Akizungumzia ugonjwa huo nchini, Dk Masue alisema takwimu zilizopatikana zimetokana na makundi matatu ambayo ni wajawazito, wanaoanza dawa za ARV na wachangiaji kwenye benki ya damu.
Alisema virusi vya Hepatitis B huweza kuambukiza kwa njia ya damu, ute, mbegu za kiume na majimaji mengine ya mwilini au kuchangia vifaa vyenye ncha kali kama wembe, pini na sindano.
“Huko ndiko kuna uwezekano mkubwa wa kupata na mpaka sasa hakuna dawa ambayo ina uwezo wa kumaliza kabisa virusi hivyo, hasa vinapokuwa tayari vimejenga protini zao ndani ya mwili wa binadamu. Iwapo utawahi matibabu, kuna uwezekano wa kupona kwa asilimia 0.5 mpaka mbili, tu,” alisema Dk Masue.
Alisema wagonjwa wengi wanaougua Hepatitis B hawaonyeshi dalili yoyote. Kwa maana hiyo mtu anaweza kuishi na virusi hivyo na kusababisha maambukizi kwa wengine bila kugundulika.
Dalili
Lakini alisema dalili za ugonjwa huo ni pamoja na homa kali, maumivu ya tumbo upande wa ini, macho na ngozi kuwa vya njano, kichefuchefu na udhaifu.
Dalili nyingine ni uchovu, kupoteza hamu ya kula, kupungua uzito na kupata mkojo mweusi.
Athari zake, kwa mujibu wa Dk Masue ni ini kuharibika, kupata saratani ya ini na kifo.
1 comment:
Mbona habari hii haizungumzii kwamba ugonjwa huu una kinga kwa njia ya chanjo?
Ni muhimu kuwaelimisha Wananchi kuhusu chanjo hili watu wajitokeze wapimwe na kwa wale ambao hawana ugonjwa huu wapewe chanjo; au nchi yet haina chanjo ya ugonjwa huu? Na kama haina he serikali inafanya mpango gani kwa kushirikiana na WHO kuweza kutoa chanjo ya homa ya maini kwa wananchi?
Post a Comment