LEO imetimia miaka 20 tangu itokee ajali ya kuzama kwa meli ya MV Bukoba iliyokuwa ikifanya safari zake kati ya Bandari ya Mwanza na Bukoba.
Kama zilivyo ajali nyingine nyingi, hii ilipoteza maisha ya mamia ya Watanzania na kuwasababishia wengine hasara ya mali.
Umati ulojaa simanzi kwa majonzi na msiba uliosababishwa na ajali hiyo uliahidiwa kwamba Serikali kuanzia wakati huo ingejidhatiti kuchukua hatua za tahadhari za hali ya juu ili kuhakikisha usalama katika vyombo vya usafiri unakuwa si kitu cha kubahatisha, na kwamba hatua madhubuti zitachukuliwa kuhakikisha kuwa ajali zinazozuilika haziwi tena chanzo cha umauti kwa wananchi wa nchi hii.
Sina hakika na maana ya ahadi hiyo, iliyotolewa kupitia Rais wa wakati huo Benjamin Mkapa na kama ilikuwa ya dhati kiasi gani, na sina hakika vile vile kama ilitokana na kile kisemwacho na wanasiasa mara nyingi kwamba ‘husema wasichokiimaanisha na humaanisha wasichokisema’.
Tumekuwa na utaratibu wa kawaida sana kupeana maneno ya faraja na kutafuta visingizo vya harakaharaka kutaka kueleza sababu za kila ajali inayotokea bila kuchukua hatua madhubuti kudhiti ajali hizo, ambazo nyingi zinazuilika.
Kati ya sababu za kuzama kwa MV Bukoba ni kujaza watu kupita uwezo wake, lakini ugonjwa huu umeendelea
kukomaa na kuwa chanzo cha ajali nyingi za majini kama vile hatutajifunza kutoka kwa MV Bukoba.
Matukio ya ajali za karibuni yanadhirisha uzembe na kutojali kama Taifa. Mifano ya kutojali huko ni pamoja na ajali ya meli ya Spice Islander iliyokuwa inatoka Dar es Salaam kwenda Pemba iliyopata ajali mwaka 2011 chanzo cha ajali kikiwa kubeba abiria wengi kuliko uwezo.
Tume iliyochunguza ajali ya meli hiyo ilisema kuwa meli hiyo ilibeba zaidi ya abiria 2000 ingawa maelezo ya nahodha wa meli alidai kuwa melini kulikuwa na watu 500.
Mwaka 2012 Meli ya MV Skagit ilizama japokuwa sababu za kuzama kwa meli hiyo inaelezwa kuwa ni hali mbaya ya hewa katika bahari siku ya tukio kwa sababu ya upepo mkali hivyo meli ya aina hii isingeweza kuhimili mawimbi makali lakini bado meli hiyo iliyokuwa na uwezo wa kubeba abiria 250 tu, ilibeba abiria zaidi ya 400.
Kama hiyo haoitoshi, itakumbukwa kuwa baada ya kupotea na baadaye kuzama kwa meli ya MV Nyamageni, ndani ya Ziwa Victoria, mwaka 2006 , likuja kudhihirika baadaye kuwa meli hiyo ya mizigo mbali na kuwa ilikuwa imebeba abiria, lakini pia ilikuwa na matatizo mengi ya kiufundi, achilia mbali kutokuwa na vifaa muhimu vya kujiokolea.
Lakini katika mshangao wa kila mtu utetezi wa Sumatra ulikuwa ni kwamba meli hiyo ilikuwa imepigwa marufuku isifanye safari zake kwa muda mrefu, mambo yakaishia hapo, watu wakaaandaa taarifa yao ya kujitetea, wenye kupoteza ndugu zao wakenda kuzika na waliopata hasara wakajuta kuzaliwa, siku ikaisha.
Ndani ya Ziwa Victoria boti ya MV Mlinzi ilitoboka na kuzama wakati ikiwasafirisha aliyekuwa waziri wa maendeleoya mifugo Anthony Diallo na wenzake; aliyekuwa Katibu wa CCM Mkoa wa Mwanza Alhaji Mwangi Kundya, Katibu wa CCM Uenezi Mkoa wa Mwanza, John Mangelepa, Mbunge wa CCM Viti Maalumu, Maria Hewa walionusurika kufa baada ya boti waliyokuwa wakisafiria kwenda katika mazishi ya Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ukerewe, kuzama, mwaka 2008.
Kama ambavyo ingetarajiwa kwa mtu yeyote anayetafuta kisingizio, Sumatra hawakukawia kutoa taarifa na taarifa ya safari hii pia ikaja kwa mfumo ule ule wa MV Nyamageni kwamba boti hiyo inayomilikiwa na idara ya maliasili Mkoani Mwanza ilipigwa marufuku kusafiri tangu mwaka 2005.
Kuna mambo mengine yanayotokea nchi hii kwa hakika wakati mwingine unashindwa kuelewa kama yanatokea kwa bahati mbaya au ni kutokuelewa au ni kusudi.
Mtu makini unajiuliza marufuku hizi za Sumatra huwa zina maana gani hasa? Kwamba chombo kimezuiwa kufanya safari zake lakini kinaendelea tu na safari zake kwa muda usiojulikana au mpaka kipate ajali ndipo wanakumbuka kwamba meli au boti fulani haikupaswa kusafiri hii inatusaidia nini sisi kama abiria na usalama wetu hapa unahakikishwaje? Haidhuru hiyo ni historia.
Sisi ni taifa la namna gani lisilotaka kujifunza kutokana na makosa? Waswahili wanasema kosa ni kurudia kosa, kwanini tunapoteza maisha na mali kwa makosa yale yale ambayo tunapaswa tujifunze kwayo na kuchukua hatua ya kutoyapa nafasi kujirudia?
Yanayotokea majini ndiyo hayo hayo tunayoyashuhudia barabarani. Kila mara tunajifunza mazoea mabaya ya kuzoea kufanya makosa?
Wakati tunawakumbuka wapendwa wetu waliotangulia mbele za haki na wakati tunazidi kuwaombea makao ya milele na wapate pumziko la amani, tunapaswa pia kujiangalia sisi wenyewe na kuona kama kweli kuna somo tulilojifunza kutokana na ajali hiyo ili kuepusha kupoteza maisha mengine ya wapendwa wetu kwa uzembe tu.
Inawezekana tunakaribia kuchelewa lakini bado nafasi ya kujisahihisha tunayo, uwezo wa kurekebisha hali ya usafiri wetu pia tunao, na sababu za msingi kabisa kuchukua hatua za haraka kurekebisha hali ya sasa na kufanya safari zetu kuwa ni sehemu ya amani na si chanzo cha mauti tunazo.
Lakini nina wasi wasi kama nia kweli ya kufanya hivyo tunayo, kwa hakika kama tungekuwa na nia ya kuufanya usafiri wa majini na kwingineko kuwa salama tungeshafanikiwa siku nyingi sana, kwa kuwa hata kama tusingekuwa na uwezo kama nia ingekuwepo ya dhati, tungepata njia.
Tunapoadhimisha kumbukumbu miaka 18 ya ajali ya MV Bukoba, turejeshe nia zetu, ziwe za dhati na zidhamirie kwa moyo mmoja kabisa kupunguza na kukomesha ajali zinazozuilika. Inawezekana kabisa tutimize tu wajibu wetu.
Mungu awapumzishe pema peponi wale wote waliotutoka katika ajali ya MV Bukoba na ajali nyingine na awape faraja na matumaini wale wote walioondokewa na wapendwa wao katika ajali hizo.
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake