Sasa ni dhahiri kuwa hali si shwari ndani ya CCM baada ya kujitokeza kundi linalomshinikiza mwenyekiti wake, Jakaya Kikwete kusita kukabidhi chama kwa Rais John Magufuli kabla ya muda wake kumalizika.
Habari zilizopatikana jana mjini hapa zimeeleza kuwa kundi hilo limejipenyeza hadi vikao vya juu vya chama hicho na hasa kile cha Kamati Kuu kilichoketi juzi huku ikidaiwa kuwa linataka Kikwete aendelee mpaka Oktoba mwakani wakati muda wake utakapokwisha.
Vyanzo mbalimbali vililidokeza gazeti hili jana kuwa kutokana na msimamo huo mpya wa kundi hilo, Baraza la Ushauri la Wazee wa CCM linaloundwa na marais wastaafu litakutana kwa dharura muda wowote kujadili, lakini likiwa na mtazamo tofauti. Wazee wanataka mchakato wa makabidhiano wa nafasi hiyo ufanyike haraka.
Wanaounda Baraza la Ushauri la Wazee ni marais wastaafu, Ali Hassan Mwinyi ambaye ni mwenyekiti, Benjamin Mkapa, Amani Abeid Karume na Dk Salmin Amour ambao ni wajumbe.
Wajumbe wengine ni Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais mstaafu, John Malecela na Spika mstaafu wa Pius Msekwa ambaye ni katibu.
Msekwa alipoulizwa kuhusu madai hayo, alisema ni uongo na hakuna makundi kama hayo na hata kama yangekuwapo, hakuna mtu wa kuyasikiliza.
“Ni utaratibu wetu tangu enzi za Mzee Mwinyi, ndani ya mwaka mmoja alimkabidhi madaraka Mkapa ambaye naye alifanya hivyo kwa Kikwete. Mimi kama katibu wa wazee wa chama hakuna kundi kama hilo na kwa taarifa yako, mwezi ujao tunamkabidhi Rais Magufuli majukumu ya chama,” alisema.
Baadaye Msekwa alituma ujumbe mfupi akiongezea, “Usiwape wasema uongo heshima wasiyostahili, hakuna kundi ndani ya CCM linalopinga Rais Magufuli kukabidhiwa uenyekiti wa CCM mwaka huu.”
Habari zilizovuja kutoka ndani ya kikao cha Kamati Kuu ya CCM, zimedokeza kuwa kundi hilo linataka Kikwete abadili msimamo, ambao aliutoa kwa mara ya kwanza kwenye sherehe za miaka 39 ya CCM mkoani Singida Februari mwaka huu.
Kabla ya kikao hicho, habari hizo zinasema JK na Rais Magufuli, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan na Katibu Mkuu, Abdulrahman Kinana walikutana kwa faragha, ajenda ya mazungumzo ikiwa maandalizi ya kukabidhi chama kwa Rais wa sasa.
Hata hivyo, mtoa taarifa huyo alidai kuwa ndani ya kikao hicho cha viongozi hao wanne, ilijadiliwa maandalizi ya kumkabidhi chama Magufuli mwezi ujao.
Pia, imedaiwa kuwa katika kikao hicho, Rais Magufuli hakuzungumza chochote zaidi ya kumsikiliza mwenyekiti na baadaye akawataka waende kwenye kikao cha Kamati Kuu.
Ndani ya kikao cha kamati kuu, inadaiwa kuliibuka pia mitazamo tofauti baadhi wakitaka JK akabidhi chama kwa Rais Magufuli na wengine wakitaka amalize kipindi chake, ingawa wengi wanataka akabidhi kwa Magufuli ili kumpa nafasi ya kuendesha chama na nchi kwa pamoja.
Mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo, Jenister Mhagama alipotafutwa nje ya viwanja vya Bunge, alikataa kuzungumza lolote kuhusu kilichojiri ndani ya Kamati Kuu, akisema atafutwe msemaji wa chama, Christopher Ole Sendeka.
“Mtafuteni Sendeka ndiyo msemaji wa chama mumuulize hayo maswali yenu. Akiamua atawaambia nani alichangia nini ndani ya Kamati Kuu. Mie msiniulize hayo maswali,” alisema.
Hata hivyo, Ole Sendeka juzi alikanusha suala hilo kujitokeza akisema miongoni mwa watu wanaotaka vyeo hivyo viwili vishikwe na mtu mmoja ni Kikwete.
“Hakuna jambo kama hilo lililojitokeza wala hakuna mjumbe aliyesimama kupinga. Maandalizi ya kukabidhi chama kwa mwenyekiti mpya yanaendelea vizuri,” alisema.
“Ndani ya siku mbili hizi, lile Baraza la Ushauri la Wazee litakutana kujadili hiyo hali na juu ya jambo hili ambalo limezua sintofahamu,” kilidokeza chanzo cha uhakika ndani ya CCM.
Habari zinadai mpango huo wa kutaka Kikwete kuendelea kukishikilia chama, ni mahsusi kujaribu kumdhibiti Rais Magufuli. “Kwa hiki kilichotokea unaweza kupata picha kuwa kuna hofu kwenye huu mtandao kutokana na kasi ya Magufuli. Sasa wanaona njia ya kumdhibiti ni kubaki na chama,” ilidaiwa.
Mbunge mmoja wa CCM ambaye hakutaka kutajwa jina lake, alisema iko hofu imeanza kujengeka kuwa kama Rais Magufuli atakapokuwa mwenyekiti anaweza kuendeleza fukuzafukuza ndani ya chama.
“Hofu hii imeanza kupata nguvu baada ya Rais Magufuli kuonekana kama anataka kuondoa watu wote wasiofanya kazi, ndiyo maana mtandao huo unajiunda upya,” alidokeza mbunge huyo.
Mbunge mwingine aliyezungumza na gazeti hili nje ya viwanja vya Bunge, alidai kuwa hofu imejengeka baada ya kile kinachodaiwa kuonekana kuvunja sheria katika utumbuaji majipu.
“Sisi tunaunga mkono kuwa kwa hali nchi ilipokuwa imefikia tulihitaji Rais mkali kama Magufuli lakini ugomvi wetu naye ni hilo la kukanyaga sheria katika utendaji wake. Ukimpa na chama itakuwaje?” alihoji. Mbunge huyo alisema aina ya utawala wa Rais Magufuli umetoa nafasi ya wana CCM kuanza kuona ipo haja ya kutenganisha nafasi ya urais na mwenyekiti wa CCM ili iwe rahisi chama kumdhibiti Rais anapopotoka.
Kauli ya JK Singida
Akizungumza katika sherehe za miaka 39 za CCM mjini Singida Februari mwaka huu, JK alisema sherehe hizo ndizo za mwisho kwake akiwa mwenyekiti wa chama hicho.
Kauli hiyo ilimaanisha kuwa huenda ataachia madaraka mapema kabla ya muda wake kama walivyofanya watangulizi wake, Mkapa na Mwinyi.
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake