Thursday, May 5, 2016

YANGA BINGWA, MFUNGAJI BORA AMIS TAMBWE ‘MR. HAT-TRICK’ VPL 2015/16


YANGA BINGWA, MFUNGAJI BORA AMIS TAMBWE ‘MR. HAT-TRICK’ VPL 2015/16

Na Baraka Mbolembole

Mshambuliazi wa kimataifa raia wa Burundi, Amis Tambwe amefanikiwa kuvunja rekodi yake mwenyewe ya magoli katika historia ya wachezaji wa kulipwa katika ligi kuu Tanzania bara (VPL).

Mrundi huyo kwa mara ya kwanza alitua Tanzania na kujiunga na Simba SC akitokea Vitalo’O ya kwao Burundi msimu wa 2013/14 na kufanikiwa kushinda tuzo binafsi ya mfungaji bora baada ya kufunga jumla ya magoli 19.

Awali kabla ya ujio wa Tambwe mshambuliaji wa kimataifa wa Kenya, Boniface Ambani alikuwa akishikilia rekodi ya mfungaji wa magoli mengi zaidi kwa msimu kwa wachezaji wa kigeni, si hivyo tu, Ambani aliweka rekodi ya mshambulizi aliyefunga magoli mengi zaidi (17) akicheza msimu wake wa kwanza VPL.

Lakini huyu Tambwe ‘Mr. hat-trick’ ni balaa. Ni mfano bora zaidi wa kulipwa na bila shaka vijana wengi washambuliaji wa baadaye watakuwa wakijifunza namna mchezaji huyo alivyo stadi kiufungaji. Utulivu wake, ufuatiliaji wake wa ‘move’ za mchezo, uwezo wake wa kujipanga, kutumia nafasi, kujitengenezea nafasi yeye mwenyewe na kutengeneza nafasi za kufunga kwa wachezaji wenzake.

Tambwe alifunga jumla ya magoli 15 msimu uliopita akichezea Simba hadi nusu ya msimu kisha kujiunga na Yanga baada ya kutemwa na timu yake hiyo ya kwanza Tanzania kwa madai ya kuporomoka kwa kiwango chake chini ya mkufunzi Mzambia, Patrick Phiri.

Yanga ilifanya usajili wa Tambwe muda mfupi baada ya kumtimua aliyekuwa kocha wao Mbrazil, Marcio Maximo mwezi Disemba, 2014. Chini ya Mholland. Hans Van der Pluijm, Tambwe amefanikiwa kufunga jumla ya magoli 35 katika VPL pekee katika kipindi cha miezi 14 waliyofanya kazi pamoja klabuni Yanga.

Jumanne hii, Mrundi huyo amefanikiwa kufunga goli lake la 20 msimu huu huku zikiwa zimesalia game nne kabla ya kumalizika kwa msimu. Tambwe ni mtulivu licha ya siku za karibuni baadhi ya watu kudai kwamba kiwango chake kimeshuka jambo ambolo si la kweli.

“Nina cheza vizuri na kuisaidia timu yangu kupata ushindi. Watu wanataka kuniona nikifunga kila mara na inapotokea sifungi wanasema nimeshuka kiwango. Wanatakiwa kutazama na mchango wangu kwa wachezaji wengine, si lazima nifunge mimi lakini nachukia kumaliza mechi bila kufunga”.

Anasema mshambulizi huyo wakati nilipofanya nae mahojiano mafupi kwa njia ya mtandao baada ya kufunga goli lake la 20 msimu huu na kuisaidia Yanga kushinda 3-1 ugenini dhidi ya Stand United katika game ambayo ilishuhudiwa mshambulizi-pacha wake, Donald Ngoma akizamisha magoli mawili, goli moja kwa usaidizi wa Tambwe.

Goli lake hilo limemfanya kumpiku mshambulizi Mganda, Hamis Kizza ambaye hadi kufikia mchezo wa 22 wa timu yake ya Simba alikuwa amefunga magoli 19 ambayo amesimamia hapo hadi sasa. Wakati timu yake ikihitaji pointi tatu tu baada ya game ya Azam FC siku ya Jumatano, Tambwe amefunga magoli 20 kati ya 61 ya timu yake ambayo katika michezo 26 ya msimu uliopita ilifanikiwa kufunga jumla ya magoli 52 kwa msimu wote. Yanga imefunga jumla ya magoli 61 katika michezo 26 ya msimu huu (magoli 9 zaidi ya msimu uliopita).

Wakati msimu uliopita katika ligi iliyokuwa na michezo 26, Yanga waliruhusu nyavu zao mara 18 msimu huu wamepelekwa nyavuni mara 15 (magoli matatu pungufu ya yale ya msimu uliopita.

Bila shaka ubingwa utaenda tena Yanga msimu huu, na Tambwe atatetea tuzo binafsi ya ufungaji bora ambayo alishuhudia ikienda kwa mchezaji mwenzake wa Yanga, Saimon Msuva msimu uliopita baada ya kufunga jumla ya magoli 17 (magoli mawili zaidi yake).

Tambwe amefunga jumla ya magoli 54 katika msimu wake wa tatu VPL. Hakuna mkali wa nyavu kama Mrundi huyu. Mfalme wa magoli ya kichwa.
Credit:Shaffihdauda

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake