Advertisements

Sunday, October 16, 2016

Atembea Siku 21 Kwenda Dodoma Kumfuata Waziri Mkuu

Angela Basso, akiwa na watoto wake wawili Happy(7) na Janeth Peter(9).

MKAZI wa Kilindi mkoani Tanga, Angela Basso, akiwa na watoto wake wawili Happy(7) na Janeth Peter(9), amelazimika kutembea kwa mikuu kwa siku 21 hadi mkoani Dodoma kwa lengo la kumuona Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ili amsaidie kurudishiwa hekari 30 za mashamba yake aliyozoporwa.

Basso alifika mjini Dodoma akiwa na watoto wake hao, ambapo alisema aliona ni vyema kwenda Dodoma kuonana na Waziri Mkuu kutokana na kuporwa mashamba na kuchomewa nyumba yake katika kijiji cha Kwendigole wilayani Kilindi na wanaume wawili ambao waliojitokeza kwa nyakati tofauti wakidai ni maeneo yao.


Alisema alipita hatua zote zinazotakiwa kuomba mashamba, ambapo awali alipatiwa hekari 10 na kijiji na akazifanyia shughuli za kilimo na kujenga nyumba yake ya kuishi, lakini baada ya kwenda kujifungua alikuta mazao yamefyekwa na yeye kutakiwa kuondoka kwenye eneo hilo.

Mwanamke huyo alisema baada ya kunyang’anywa alifikisha malalamiko yake kuanzia uongozi wa kijiji hadi wilayani na baadaye akapatiwa eneo jingine la hekari 20, lakini alijitokeza mtu mwingine na kudai eneo hilo ni mali ya kanisa, licha ya kumiliki kihalali eneo la Hembekali.

“Nilikwenda kushtaki kwa serikali ya kijiji, kata na baadaye kwenda kwa mkuu wa wilaya ambako iliamuliwa nirudishiwe mashamba yangu, lakini hawakufanya hivyo mwisho wa siku nikafukuzwa kabisa kuishi kwenye eneo hilo,” alisema Basso

Mwanamke huyo alisema baada ya kutimuliwa alianza kuishi maisha yake kituo cha mabasi Muheza na baadaye alifukuzwa kituoni hapo kwa madai watu hawaruhusu kulala ama kuishi hapo na ndipo akaamua kuanza safari ya Dodoma baada ya kusikia Waziri Mkuu amehamia Dodoma.

Akisimulia machungu ya safari yake, Basso alisema akiwa njiani walikuwa wakila mahindi ya kukaanga na maji ya kunywa na kulala porini muda mwingine giza linapowakuta katikati ya pori.“Naomba kusaidiwa jamani nimeanza kufuatilia tangu mwaka 2012 lakini bila mafanikio jambo ambalo limechangia familia yake kusambaratika kutokana na kukosa pa kuishi huku watoto wangu hawa wakikosa elimu kwa kutangatanga,”alisema Mwanamke huyo.

Basso aliomba Serikali itende haki ili yeye aweze kupata haki yake ya kurejeshewa mashamba yake na kurudi katika eneo hilo ili watoto wake wawili wapate nafasi ya kusoma. Mwanamke huyo alisema kwasasa amekuwa kama mkimbizi kutokana na kukosa hana mahali pa kuishi huku mumewe naye akiikimbia familia yake baada ya kuporwa ardhi hiyo ambayo ilikuwa kama kitega uchumi chao.

CREDIT: MICHUZI ISSA.

No comments: