Advertisements

Sunday, October 16, 2016

MTOTO ATESEKA MIAKA 4 MAHENGE

Mtoto Devotha Nagaikaya akiwa amepakatwa na shangazi yake Emma Nagaikaya.(Picha na John Nditi).
MTOTO Devotha Lucanus Nagaikaya (4), anaishi kwa mateso makubwa aliyoyapata akiwa na umri wa miezi mitano tu baada ya kuzaliwa.

Pamoja na mateso mbalimbali, maisha ya Devotha yamemfanya kuishia kulala kitandani, huu ukiwa ni mwaka wake wa nne, kutokana na kushindwa kukaa.

Devotha anaishi na shangazi yake, Emma Nagaikaya, katika mtaa wa Togo, Kata ya Mahenge, Wilaya ya Ulanga, mkoani Morogoro, baada ya mama yake mzazi, Emelda Maumba kupata kichaa baada ya kujifungua mtoto wake huyo na kumkataa kwamba si wake.

Emma akizungumza na HabariLeo Jumapili hivi karibuni nyumbani kwake mtaa wa Togo, alisema amelazimika kuchukua jukumu la kumlea mtoto huyo, ambaye ni wa mdogo wake, Lucanus Nagaikaya, baada ya mama yake mzazi kumkataa akiwa wodini mara tu baada ya kujifungua.

Chanzo chake

Akielezea mkasa uliompata mtoto huyo, Emma alisema Devotha alizaliwa Machi 1, 2012 na alipofikisha umri wa miezi mitano, aliugua homa kali na alipofanyiwa vipimo na madaktari, aligundulika kupata madhara kwenye uti wa mgongo na kulazimika kulazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Ulanga iliyopo mjini Mahenge kwa matibabu.

Kwamba madaktari waliendelea kupigania afya ya Devotha ili aweze kurejea katika afya njema, lakini jitihada hizo ziligonga mwamba, kwani hadi alipofikisha umri wa miezi minane, hakuonesha kupona, badala yake alishindwa kukaa chini, kusema na kushika kitu chochote. Aliishia kulala kitandani muda wote.

Alisema hali hiyo iliwafanya madaktari wa Hospitali ya Mahenge, kumwandikia vipimo kwenda Hospitali ya CCBRT ya jijini Dar es Salaam kwa ajili ya uchunguzi wa kina, ikiwa ni pamoja na kujaribu kumfanyisha mazoezi ya viungo, kuona kama inaweza kumsaidia kumrejesha katika afya ya kawaida.

“Tulikwenda CCBRT lakini kutokana na gharama kubwa ya vipimo, mazoezi na gharama za kuishi Dar es Salaam, nilishauriwa na madaktari nirudi naye Mahenge ili kuendelea na mazoezi ya viungo na tiba nyingine katika Hopitali ya Wilaya ya Ulanga”, alisema.

Hata hivyo, alisema suala hilo nalo lilikabiliwa na changamoto baada ya kubainika kuwa hospitali hiyo, haikuwa na eneo la kufanyia mazoezi maalumu ya viungo kwa watoto na pia kukosekana kwa vifaa na wataalamu wa kada hiyo, hatua iliyosababisha Devotha kushindwa kupata matibabu yaliyotarajiwa.

“Tumeweza kumpeleka CCBRT kupata matibabu na kufanyiwa mazoezi, lakini hilo limefanyika mara tatu tu na sasa tumeshindwa kuendelea nalo kutokana na ukosefu wa fedha za kumudu gharama za matibabu ambazo zipo juu, familia yetu haina uwezo kifedha,” alisema Emma.

Akitoa mfano wa kuelemewa kwa gharama, shangazi huyo alisema mathalani amekuwa analazimika kutumia Sh 17,000 kila wiki ili kumweka Devotha katika hali ya usafi kwa kununua nepi maalumu za kumsitiri kutokana na kulala kitandani muda wote na kushindwa kukaa wala kufanya jambo lolote.

Kutokana na mateso anayokabiliana nayo mtoto huyo, shangazi huyo aliiomba jamii na serikali kuisaidia familia hiyo ili waweze kumpeleka katika hospitali kubwa kwa ajili ya kumfanyia uchunguzi wa kina na kupata tiba, ambazo zitamwezesha kupona maradhi yake na kumrejeshea furaha kama waliyonayo watoto wengine.

Naye Upendo Nagaikaya, ambaye Devotha ni mtoto wa mjomba wake, alisema kutokana na kuzidiwa na maradhi yanayomsumbua, alipofikisha umri wa miezi minane, pamoja na kushindwa kukaa, kushika kitu wala kuongea, lakini pia shingo yake ilianza kulegea na kushindwa kukaza.

Akizungumzia aliko mama mzazi wa Devotha, Upendo alisema mara tu baada ya kujifungua, mama yake Devotha alipatwa na kichaa na alianza kumkataa mtoto wake huku akitishia kumdhuru, hatua iliyomfanya shangazi yake Emma, kumchukua ili kumlea.

Alisema Devotha anakabiliwa na mateso makubwa kutokana na maradhi hayo yanayomsibu, huku uwezo wa familia katika kuokoa maisha yake, kwa kurejesha afya yake kwa kumpatia matibabu na mazoezi ya viungo katika hospitali kubwa, ukiwa ni mdogo.

Upendo aliiomba jamii na serikali kuisaidia familia hiyo kwa hali na mali ili kupata fedha za kugharamia matibabu zaidi kwa mtoto huyo ili aweze kurudi katika hali yake ya kawaida na kumuokoa kutoka katika maisha yake ya sasa ya kulala kitandani au kupakatwa na ndugu muda wote wa saa 24 kwa siku saba.

Alisema endapo atapatiwa matibabu ya kupona, Devotha ataondoka na mateso ya kushindwa kuamka na kulazimika kuangaliwa na mtu maalumu wa kumuangalia na kumsafisha, anapopata haja ndogo na kubwa na kuvishwa nepi maalumu kila mara.

Jamii inaombwa kumsaidia mtoto huyo kupitia simu namba 0712 801864; jina Emma Nagaikaya ambaye ndiye mlezi wa mtoto huyo tangu akiwa na umri wa miezi mitano hadi sasa. Unaweza pia kuwasilisha mchango wako kupitia Mhariri wa gazeti hili kwa simu namba 0766 843382; jina Nicodemus Ikonko.

HABARI LEO

No comments: