Advertisements

Sunday, November 20, 2016

WAZIRI MKUU ATOA SIKU 18 UMEME UKAMILIKE MLANDIZI

 Waziri Mkuu, Kassim  Majaliwa akizungumza baada ya kukagua  maendeleo ya ujenzi wa kiwanda cha Kiluwa Still Group cha Mlandizi mkoani Pwani  Novemba 19, 2016.  Kushoto ni  Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa 

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa siku 18 kwa Mkandarasi wa umeme kwenye kiwanda cha Kiluwa Steel Group awe amemaliza kazi ya kuweka umeme mkubwa ili kiwanda hicho kianze kazi. 

Ametoa agizo hilo jana (Jumamosi, Novemba 19, 2016) wakati akizungumza na wananchi na viongozi mbalimbali wa Serikali na wa Mkoa wa Pwani waliofika kiwandani hapo eneo la Mlandizi wakati akikagua utekelezaji wa maagizo aliyoyatoa Julai 12, mwaka huu alipozuru kiwanda kwa mara ya kwanza.

“Nilipokuwa hapa mara ya kwanza niliagiza itengenezwe njia ya reli kutoka njia panda ya reli ya kati, lakini pia niliagiwa uwekwe umeme wa msongo mkubwa ili kiwanda kiweze kuanza uzalishaji mapema mwakani. Nimefarijika kukuta maagizo haya yametekelezwa kwa kiasi kikubwa isipokuwa hili la umeme,” alisema.


“Mkandarasi ameomba siku 14, nimempa hadi tarehe 7 Desemba ahakikishe umeme unafanya kazi kwa kiwango kinachotakiwa. Sasa hivi wameanza test lakini muda ili transforma iweze kuhimili mzigo mkubwa… hili ni suala la kitaalamu kwa hiyo tuwape muda.”

Waziri Mkuu pia alisema amefarijika kusikia kwa orodha ya watu wanaodai fidia sababu ya kuoisha njia ya reli ijengwe, imeshawasilishwa kwa Mkuu wa Mkoa na mwenye kiwanda yuko tayari kuwalipa maa taratibu zitakapokamilika.

Mapema, akiwasilisha taarifa fupi, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Eng. Evarist Ndikilo alisema haelewi ni kwa nini mkandarasi huyo anazidi kuomba siku 14 ili kukamilisha wakati aliahidi kuwa 14 za awali zingetosha kukamilisha kazi hiyo.

Kuhusu fidia kwa wananchi na Halmashauri ya Wilaya hiyo, Mkuu huyo wa Mkoa alisema wananchi waliopisha njia wanadai fidia ya sh. milioni 95.76 na Halmashauri inadai sh. milioni 307.26 na kwamba jumla yote inafikia sh. milioni 403.

Alipopewa nafasi na Mkuu wa Mkoa huo ajieleze mbele ya Waziri Mkuu, Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Dekan Group Ltd, Eng. Desderius Luhaga ambaye amepewa kazi ya kuweka umeme na transforma Mlandizi alisema anahitaji apewe siku 14 ili aweze kukamilisha kazi hiyo.

“Kazi kubwa ya umeme tumeshaifanya na hii ni ya umeme wa msongo wa kilovoti 132, na tumeanza kutest umeme katika baadhi ya mitambo hapa kiwandani, lakini tunahitaji siku karibu tano ili transforma ipoe tangu tulipoifunga ndipo iweze kupokea mzigo mkubwa. Kisha tutaanza kuunganisha katika maeneo mengine madogo madogo humu ndani,” alisema.

Katika hatua nyingine, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Reli Tanzania (TRL), Bw. Masanja Kadogosa  alisema shirika hilo limetumia sh. milioni 863 kukamilisha ujenzi wa reli ya km.5 kutoka njia panda hadi kwenye kiwanda hicho ambapo kati ya hizo km.1.5 zimo ndani ya kiwanda.

Alisema hadi sasa wameshaweka njia nne za reli, moja ikiwa ni mahsusi kwa ajili ya kubeba makaa ya mawe. 

“Tulilazimika pia kujenga culvert katika eneo moja kwa sababu pailikuwa na shimo kubwa. Tumetumia fedha kidogo kwa sababu tumetumia mafundi wetu badala ya wakandarasi,” aliongeza.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Kiluwa Steel Group, Bw. Mohammed Kiluwa alimweleza Waziri Mkuu kuwa anatarajia kuanza uzalishaji Januari, mwakani na kwamba ataajiri wafanyakazi wapatao 200.

“Tunataraji kuanza uzalishaji Janruari, mwakani na uzalishaji utakuwa tani 2,000 kwa siku. Ila tumekubaliana na wawekezaji wenzangu tuweke pia viwanda vingine vitatu kwa sababu kutakuwa na umeme wa kutosha.”

“Tunatarajia kufungua viwanda vine vya kutengeneza gypsum powder, pikipiki, nguzo na vifaa vya kufungia nyaya za umeme mkubwa pamoja na tissue. Tuna eneo lingine Mkuranga lakini kule hakuna umeme, kwa hiyo tumepanga kuweka hivyo viwanda hapa kwa sababu tuna eneo la kutosha.”

Hata hivyo, Bw. Kiluwa alitumia fursa hiyo kumweleza Waziri Mkuu kwamba wanapata taabu ya makaa ya mawe kwa sababu wanaletewa makaa yenye ukubwa wa milimita 10 hadi 15 badala ya milimita 35 – 40 ambazo wanahitaji kwa ajili ya kiwanda chao.

“Tukiagiza tani 30, tunachambua mawe ya saizi inayotufaa na kujikuta tunabakia na tani saba tu. Kiasi kilichobakia ni vumbi tupu,” alisema.

Waziri Mkuu alimwagiza Naibu Katibu Mkuu wa Viwanda na Biashara, Eng. John Malongo awasiliane na Wizara ya Nishati na Madini ili afuatilie ni kwa nini watengenezaji wa makaa ya mawe hawafuati vipimo halisi vinavyotolewa na wawekezaji.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,

No comments: