Friday, December 2, 2016

KASESELA KUIOMBA UN KIWANDA CHA KUSINDIKA NYANYA

Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo (UNDP), Alvaro Rodriguez na Ofisa wa Mawasiliano na Ushirikiano NUNV kutoka Ofisi ya Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini, Didi Nafisa wakitazama vibao vya malengo ya maendeleo endelevu (SDGs) walipofika ofisini kwa Mkuu wa wilaya ya Iringa, Richard Kasesela ajili ya kumuaga kabla ya kuelekea jijini Mbeya.(Habari picha na Zainul Mzige wa Modewjiblog)

Mkuu wa wilaya ya Iringa, Richard Kasesela ameuomba Umoja wa Mataifa kusaidia kuanzishwa kwa kiwanda cha kusindika nyanya wilayani humo ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa malengo endelevu ya dunia kipengele cha uondoaji wa umaskini. Alisema anaamini katika kukabili umaskini ni lazima kuwapo na viwanda vinavyowezesha bidhaa ghafi za wakulima kupata soko na kwa wilaya hiyo kuondoa tatizo la soko la nyanya kutawezesha wananchi wake kupiga vita umaskini. Aidha alisema kwamba serikali imejiandaa vyema kutekeleza malengo hayo ya dunia kutokana na hatua mbalimbali inazochukua katika kuhakikisha haki na ustawi wa wananchi wake. Sanjari na kueleza hatua hizo pia alitumia nafasi hiyo kukanusha swali la mwandishi wa habari kwamba serikali ya Tanzania haijawaandaa wananchi kutekeleza malengo hayo. 
Mkuu wa wilaya alisema maandalizi yapo na si kweli kwamba serikali haijafanya maandalizi kwa kuwa moja ya lkengo katika malengo hayo inazungumzia maandalizi ya utekelezaji. Alisema serikali inatambua thamani ya maandalizi katika utekelezaji wa malengo hayo ndiyo maana inashirikiana bega kwa bega na Umoja wa Mataifa katika kuandaa watu kuelewa malengo hayo na kuyatekeleza. “…ili kuondoa umaskini…
hatuwezi kupitisha malengo hayo bila kushirikisha wananchi… suala la ushirikishaji ni lengo la 17, ni lengo ambalo linataka kila mtu ashiriki katika maendeleo” alisema Kasesela ambaye alikumbusha nguzo tano za malengo hayo ili kuyafanikisha. Alisema pamoja na kuondoa umaskini malengo hayo yamesimama katika kuhakikisha kwamba watu wanaishi kwa amani na ustawi, kukiwa na usawa wa kijinsia na kila mtu kunufaika na hali ya rasilimali na uchumi uliopo.
Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo (UNDP), Alvaro Rodriguez akimkabidhi cheti balozi wa malengo ya maendeleo endelevu (SDGs) Mkuu wa wilaya ya Iringa, Richard Kasesela aliposhiriki katika semina ya SDGs iliyofanyika katika Chuo Kikuu cha Iringa.

Aidha alisema kitendo cha mabadiliko yanayozungumzwa ya kuondoa umaskini kutoonekana vijijini kunatokana na ukweli kwamba taifa kwa muda mrefu ilikuwa inakabiliwa na tatizo la rushwa.

Alisema japo serikali imekuwa ikipigana na rushwa kubwa, tatizo la vijijini lilikuwa kukosekana kwa haki kwa wananchi kutokana na rushwa hali iliyokwamisha maendeleo ya watu binafsi na hata serikali za vijijini.

“kutokana na hili unaona mafanikio ya kupiga vita rushwa inasaidia kukabili changamoto za malengo ya dunia ya kuondoa umaskini na kuweza kuwa na nchi yenye staha na kujali wananchi wake” alisema Kasesela.

Kwa mujibu wa mkuu huyo wa wilaya malengo ya dunia yakifanyiwa kazi kwa namna inavyostahili taifa hili litafika mbali.

“kufuta umaskini moja kwa moja ni hatua.. Kufuta umaskini moja kwa moja…kusimamia haki.. semina zimepungua.. safari za hovyo zimepungua na sherehe zisizokuwa na tija zimepungua.. lengo la kuhakikisha afya kwa kila mmoja kwa kuwa na zahanati kila kijiji” anasema Kasesela ni sehemu ya kazi kubwa inayofanywa na serikali ya awamu ya tano katika kufikisha wananchi wake katika ustawi na hivyo kutekeleza malengo ya dunia.
Mkuu wa wilaya ya Iringa, Richard Kasesela akitoa maelezo ya namna atakavyoshirikisha wananchi wake SDGs wanaofika ofisini kwake kupata huduma mbalimbali kwa Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo (UNDP), Alvaro Rodriguez aliyefika ofisini kwa DC Kasesela kwa ajili ya kumuaga kabla ya kuelekea jijini Mbeya.

Aliwaambia waandishi wa habari waliokuwa katika kampeni ya uhamaishaji wa malengo ya maendeleo endelevu ya Umoja wa Mataifa wilayani Iringa, Mkuu huyo wa wilaya alisema kwamba taifa hili limepiga hatua kubwa katika utekelezaji wa malengo ya dunia na kwamba hilo linaanzia vile vile katika elimu kwa watu wake.

Hata hivyo alisema la maana zaidi ni kuhakikisha kwamba mtu mmoja mmoja anatekeleza malengo hayo kuwa ni ya wote na wala si ya serikali pekee.

“Malengo ni yetu sisi sote si ya mtu mmoja ni mimi nitafanya nini kuondoa umaskini na kuondoa njaa” alisema Kasesela huku akitole amfano wa mkoa wenye chakula kingi kama wa Iringa kuwa na tatizo la udumavu.

“mkoa wenye chakula na watoto wamedumaa, ulaji mfumo wa ulaji .. sasa lazima kufundishana watu wale chakula kilichobora…Waweze kula matunda kumi na nne na mboga kila siku.” Alisema.

Alisema amefurahishwa sana kwa Umoja wa Mataifa kuendesha kampeni za kubadili watu fikira kwani wakibadilika utekelezaji wa malengo hayo utakuwa mwepesi zaidi.
Mkuu wa wilaya ya Iringa, Richard Kasesela katika picha ya pamoja na Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo (UNDP), Alvaro Rodriguez aliyemtembelea ofisini kwake mjini Iringa.

Huku akiahidi kuwa championi wa Umoja wa Mataifa katika kuhamaisha utekelezaji wa malengo hayo 17, alisema moja ya kitu cha kwanza katika kuondoa umaskini ni kuhakikisha kwamba wakulima wa nyanya wanapata sehemu ya kuuzia nyanya zao badala ya kuoza. Alisema watauomba Umoja wa Mataifa kusaidia kujenga kiwanda cha kutengeneza rasilimali za nyanya kama walivyowasaidia watu wa Simiyu wa kuanzisha kiwanda chaki na maziwa. Amesema kuwepo kwa kiwanda kutasaidia sana kuwa na soko la uhakika na kwamba wananchi umaskini wao utapigwa vita kwa namna inayofaa zaidi.

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake