Saturday, December 3, 2016

MWENYEKITI WA KATA YA RUNGWA MATATANI KWA KUMTOZA FAINI YA LAKI MBILI MWANAFUNZI WA KIKE.

Mkuu wa mkoa wa Singida, Mhandisi Mathew Mtigumwe ameagiza kukamatwa na kufunguliwa mashtaka mwenyekiti wa baraza la usuluhishi la kata ya Rungwa ambaye pia ni kaimu mwenyekiti wa CCM kata ya Rungwa, iliyoko halmashauri ya Itigi wilayani Manyoni baada ya mwenyekiti huyo kumtoza faini ya shilingi laki mbili mwanafunzi wa kike wa darasa la nne kwa tuhuma za kujihusiha kimapenzi na mkazi mmoja kwenye kata hiyo.

Hayo yamebainika kwenye ziara ya mkuu wa mkoa wa Singida katika halmashauri ya Itigi baada ya Bwana Ally Ramadhani kutoa malalamiko kwenye mkutano wa hadhara yakuwa, mwenyekiti alimtoza faini mwanafunzi huyo na kuacha kumchukulia hatua stahiki mtu anayetuhumiwa kumrubuni mwanafunzi ambaye aliachiwa huru baada ya kulipa faini ya shilingi laki mbili.


Alipotakiwa na mkuu wa mkoa wa Singida kutoa maelezo kwanini wamemtoza faini mwanafunzi huyo wa kike wa darasa la nne, mwenyekiti wa baraza la usuluhishi la kata Bwana Zuberi Manjemi alisema wameamua kumtoza faini binti huyo kwa kosa la kukubali kupokea simu na kukubali kurubuniwa.

Kutokana na hali hiyo mkuu wa mkoa wa Singida Mhandisi Methew Mtigumwe ilimbidi kuchukuwa maamuzi magumu na kuamrisha kuvunjwa kwa baraza hilo na kutoa amri ya kukamatwa mwenyekiti huyo na kufunguliwa mashitaka, kwa sababu haiwezekani binti wa darasa la nne kupigwa faini ya lakimbili na kumwachia huru mtuhumiwa.

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake