Maofisa watano wa Mamlaka ya Hifadhi ya
Ngorongoro (NCAA) wanaotuhumiwa kushiriki kumwondoa faru John kutoka
katika Creta hiyo walikamatwa juzi kwa mahojiano ili kujua ukweli kuhusu
mazingira ya kupotea kwake.
Hatua ya maofisa hao kukamatwa imekuja
siku tatu baada ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuituhumu menejimenti,
wafanyakazi wa NCAA na Baraza la Wafugaji (NPC) kuwa imejaa vitendo vya
rushwa na wizi na asingeweza kuvumilia sakata la faru John ambaye
alisema kuwa aliuzwa kwa Sh200 milioni kwenye Hoteli ya Grumet iliyo
Hifadhi ya Serengeti na kuwa walipokea fedha za awali Sh100 milioni.
Waziri Mkuu alisema anataka kumwona faru huyo, nyaraka za kumhamisha na
kama amekufa basi apelekewe hata pembe ofisini kwa kuwa anajua pa
kuzipeleka.
Habari za uhakika kutoka Ngorongoro, ambazo zimethibitishwa na Jeshi la
Polisi zinasema kuwa maofisa hao watano wanashikiliwa katika kituo chao
cha Ngorongoro kutokana na ushiriki wao kwa njia moja au nyingine.
Wanaoshikiliwa ni pamoja na Israel Naman ambaye alikuwa Kaimu mkuu wa
idara ya uhifadhi wakati faru huyo akiondolewa.
Wengine ni Cuthbert
Lemanya, ambaye alikuwa Mkuu wa Kanda ya Creta, Dk Athanas Nyaki ambaye
anadaiwa kumdunga sindano ya usingizi ili aweze kubebwa.
Maofisa wengine
waliokamatwa ni aliyekuwa Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii wa
Mamlaka ya Ngorongoro, Kuya Sayaleli na aliyekuwa Kaimu Mkuu wa Idara ya
Ikolojia, Patrice Mattey.
Ofisa mmoja
wa NCAA, ambaye aliomba kuhifadhiwa jina lake jana alisema maofisa hao
walikamatwa juzi jioni na jana walikuwa wanaendelea kuhojiwa.
“Tuiache
serikali ifanye kazi kwani ni muhimu sana kujulikana ukweli wa tukio
hili,” alisema ofisa huyo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles
Mkumbo hakupatikana jana kuelezea tukio la kukamatwa maofisa hao, baada
ya simu yake kupokelewa na msaidizi wake ambaye alieleza yupo kwenye
kikao.
Lakini, ofisa wa mmoja wa polisi, ambaye aliomba kuhifadhiwa
jina kwa kuwa si msemaji alikiri kukamatwa maofisa hao kwa mahojiano.
Chanzo cha sakata
Akiwa katika ziara ya kikazi Ngorongoro, Waziri
Majaliwa aliibua sakata la kuhamishwa kinyemela faru huyo na kudaiwa
kupelekwa Grumet.
Waziri mkuu alitaka ukweli kuhusu upotevu wa John
aliyeondolewa Creta na kupelekwa Grumet na kudaiwa kufa huku taarifa za
kifo hicho zikifanywa siri.
Waziri Mkuu alitaka kupewa nyaraka zote
zilizotumika kujadili kumuondoa faru na kuamua kumpeleka Grumet.
Waziri
Mkuu alitoa hadi Desemba 8 (jana) awe amepata taarifa zote, ikiwamo ya
daktari inayothibitisha kifo hicho na kwamba pembe za faru huyo
zifikishwe ofisini kwake. Pia, Majaliwa alisema ikibainika wapo
waliokiuka taratibu watawajibika.
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake