Sunday, January 15, 2017

GLOBAL PEACE FOUNDATION KUPITIA PROGRAMU YA "VIJANA NA AMANI" WAHIMIZA AMANI KWA VIJANA WA BUREZA, MULEBA MKOANI KAGERA

 Mwakilishi wa GPF  Mkoani Kagera  Bw. Benson Daud akizungumza na vijana katika Kongamano hilo
 Baadhi ya wanafunzi wakiwa wakimsikiliza kwa makini Bw. Benson (hayupo pichani) wakati wa Kongamano hilo
Baadhi ya wanafunzi kutoka shule mbalimbali wilayani Muleba wakimsikiliza kwa makini Diwani wa kata ya Bureza Bw.Deores Msinde(hayupo pichani)
  Picha ya pamoja

Diwani wa kata ya Bureza Bw.Deores Msinde akiongoza upandaji miti ambapo walipanda miti 20 katika eneo walilofanyia kongamano.

Na Mwandishi wetu
Zaidi ya Vijana 150 kutoka Shule ya  Sekondari Bureza, Shule za Msingi za Butembo,Higabilo,Kinovelu wakiwa pamoja na Diwani wa Kata ya Bureza na walimu  wilayani Muleba Mkoani Kagera kupitia Programu ya Vijana na amani inayo endeshwa na Global Peace Foundation(GPF), wamekutana katika kongamano  ambalo lengo kubwa ni kuhamasisha na   kudumisha amani kutoka katika ngazi ya Familia na jamii kwa ujumla.

Akizungumza na wanafunzi hao Mwakilishi wa GPF  Mkoani Kagera Bw. Benson Daud alisema kuwa waliamua kuwakutanisha vijana wenye umri kati ya miaka 13-21 kwa kuwa hao ndio wapo katika  kundi ambalo limeathirika zaidi na uvunjifu wa amani.

Alieleza kuwa katika kata ya Bureza kumekuwa  na matatizo mengi yanayowakabili vijana ikiwa ni pamoja na utoro wa shule ambapo wengi wao huenda katika ziwa Victoria kwa ajili ya kuvua samaki na kujifunza tabia zisizo njema ikiwemo kuvuta Bangi na vileo vinginevyo, Mimba za utotoni ambazo nyingi husababishwa na madereva wa bodaboda ambao  hupelekea migogoro mikubwa baina yao na familia pamoja na  familia zenyewe kuchangia uvunjifu wa amani kwa sababu ya wazazi kuwakatalia watoto shule na kuwalazimisha wafanye biashara baada ya masomo.

Benson aliwasihi  wazazi na vijana  kuachana na hayo mambo na vitendo vya uvunjifu wa amani  kwani wakifanya hivyo kutakuwa na amani na wataishi vizuri katika jamii inayowazunguka.

Nae Diwani wa Kata ya Bureza Bw. Deores Msinde aliwahimiza vijana kuwa mfano wa kuigwa katika kudumisha amani, aliyasema hayo kutokana na mambo yanayoendelea katika kata hiyo ambapo vijana ndio wanakuwa mstari wa mbele kuvunja amani, "Naomba nitoe mfano katika kata yetu kumekuwa na mgogoro wa ardhi ambapo wakulima na wafugaji wamekuwa wakitaka sehemu moja kwa ajili ya kilimo na ufugaji  jambo ambalo limepelekea makundi hayo ambao ni vijana kupigana kila wakati huku wazee wakiwa wamekaa pembeni" alisema Diwani Deores na kuwaomba vijana waachane na mambo hayo na kuwa serikali inafanya jitihada za kutatua mgogoro huo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti vijana mbalimbali wamefurahishwa na programu hiyo inayoendeshwa na GPF ya 'VIJANA NA AMANI' na kusema kuwa itawasaidia hata kuwaelimisha wengine umuhimu wa kulinda amani.


No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake