Januari 12, 1964, wananchi wa Visiwa vya Zanzibar waliupindua uongozi wa Sultan wa Oman, na kuanzishwa rasmi kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Aman Abeid Karume akiwa ndiyo rais wake wa kwanza.
Miaka mingi baadaye, bado siku hiyo inaendelea kukumbukwa na kuadhimishwa si visiwani pekee bali hata bara! Naam, ni siku ya Mapinduzi ya Zanzibar ambayo leo, Januari 12, 2017 inaadhimishwa nchini kote.
Hata hivyo, licha ya siku hii muhimu kwa historia ya Zanzibar na Tanzania Bara kuendelea kuadhimishwa miaka mingi baada ya mapinduzi hayo, bado kuna mambo ambayo wengi hawayajui, au kama wanayajua kila mmoja anaelezea tofauti na kuleta mkanganyiko, kuhusu nani hasa aliyekuwa kiongozi wa mapinduzi hayo na jinsi yalivyofanyika.
Vizazi vya sasa, ambavyo havikuwepo wakati wa mapinduzi hayo, vimeendelea kuishi katika mkanganyiko mkubwa kuhusu mapinduzi hayo, na kwa bahati mbaya, hata vitabu vya historia, vinavyotumika mashuleni, havielezi kwa undani kuhusu mapinduzi hayo.
Baadhi ya watu wanaamini kwamba Karume ndiye aliyeongoza mapinduzi hayo na baadaye kuingia madarakani, akiwa ndiye rais wa kwanza wa serikali ya mapinduzi lakini, walioshuhudia mapinduzi hayo, wanaeleza kwamba, kiongozi wa mapinduzi hayo, ambaye ndiye aliyekuwa ‘mastermind’, kuanzia kusuka mipango ya awali mpaka kusimama mstari wa mbele kwenye vita, ni John Okello, Field Marshal ambaye alizaliwa Uganda.
Wakati walioshuhudia mapinduzi hayo wakimtaja Okello kama shujaa namba moja, vitabu vingi vya historia hazimzungumzii kabisa mwanajeshi huyu, zaidi linatajwa jina la Karume, kiasi cha kuwaacha njia panda watu ambao hawakuwepo kipindi hicho, hususan vijana waliozaliwa kuanzia miaka ya sitini kuja mbele.
Baadhi ya vitabu vya historia, vinaeleza kwamba, wakati Okello akishirikiana na wanachama wa Afro Shiraz Party (ASP), chama kilichokuwa kikipigania uhuru visiwani humo, Karume alikuwa akiishi Bara (Tanganyika), baada ya kukorofishana na serikali ya sultani na chama cha ZNP kilichokuwa kikiongozwa na Mohammed Shamte.
Historia ya Mapinduzi ya Zanzibar, inatajwa kuanza Oktoba, 1963 ambapo Zanzibar ilipata uhuru wake wa bendera, kutoka kwa Waingereza lakini bado ikaendelea kukaliwa kimabavu na utawala wa sultani. Miezi michache baada ya Waingereza kuondoka, ndipo vuguvugu la mapinduzi lilipoanza, hatimaye Wazanzibar wakaingia mitaani na kupambana kwa saa 9, kabla ya kufanikiwa kuuangusha utawala wa sultani, Januari 12, 1964.
Miezi mitatu baadaye, Aprili 26, 1964, Tanganyika na Zanzibar viliungana na kuunda Tanzania, muungano ambao umeendelea kudumu hadi leo na kuwa mfano wa kuigwa duniani kote.
JOHN OKELLO NI NANI?
Vitabu vichache vya historia, vinamtaja John Okello, kuwa ni raia wa Uganda, aliyezaliwa katika Wilaya ya Lira, ambaye baadaye aliamua kuikimbia nchi yake kwa sababu za kiuchumi na kisiasa, akahamia Kenya kabla ya kuingia Kisiwani Pemba, Juni 21, 1959, akitafuta ajira.
Muda mfupi baadaye, alijiunga na ASP, ambacho wanachana wake wengi walikuwa ni watu weusi. Sababu ya harakati zake, alifanikiwa kuchaguliwa kuwa katibu wa vijana wa chama hicho, katika eneo la Vitongozi, ambalo baadaye lilikuja kuwa ngome ya vijana wa Pemba.
Ni katika kipindi hicho, ndipo alipoanza harakati za kupigania uhuru na haki za watu weusi ambapo katika hotuba zake mbalimbali, alikuwa akiwahamasisha watu weusi, kuungana na kudai haki zao. Mwanzoni mwa mwaka 1963, alithubutu kuwahamasisha vijana na watu wengi weusi wa Zanzibar, kuingia mitaani na kudai uhuru wao lakini jaribio lake lilizimwa na polisi na askari kanzu.
Okello akaingia kwenye orodha ya wapinga serikali, kama ilivyokuwa kwa Karume ambaye alikuwa akisakamwa sana na utawala wa sultani, kutokana na misimamo yake ya kutetea utu na haki za watu weusi, kama ilivyokuwa kwa Okello.
Ni katika kipindi hicho, Karume aliamua kutafuta hifadhi ya kisiasa Bara (Tanganyika), Okello akaendelea na harakati za kuwafundisha vijana wa Kizanzibari, wengi wakiwa ni waangua nazi, mbinu za kivita kwa sababu yeye (Okello), tayari alikuwa na mafunzo ya kijeshi aliyoyapata nchini Uganda.
Mafunzo ya kijeshi yalifanyika porini na hatimaye, akafanikiwa kupandikiza morali ya ushindi kwa Wazanzibari, ambao siku ya mapinduzi, wanaume zaidi ya 600 wakiwa na silaha za jadi, waliingia mitaani na kuanza kupambana na polisi, wakafanikiwa kupora silaha ambazo ndizo zilizotumika kweye mapinduzi hayo.
Okello aliwaongoza vijana hao ambao kadiri muda ulivyokuwa unasonga mbele ndivyo walivyokuwa wakizidi kuongezeka, mpaka Stone Town, Zanzibar yalipokuwepo makazi ya Sultani Sayyid Jamshid Ibn Abdullah. Kama bahati kwake, sultani na familia yake pamoja na watu wake wa karibu walifanikiwa kutorokea nchini Uingereza, mapinduzi yakawa yametimia.
Hivyo ndivyo mapinduzi yalivyotokea, kwa mujibu wa vitabu mbalimbali vya historia na watu waliokuwepo kipindi hicho.
Bado haifahamiki kwa uwazi, nini kilitokea kwa Okello baada ya mapinduzi hayo kwani hakuonekana tena visiwani humo, wala jina lake halitajwi na mamlaka husika, kuwa ndiye aliyekuwa mstari wa mbele kwenye mapinduzi hayo, jambo linaloleta mkanganyiko kwa wachambuzi wa mambo.
Hashim Aziz/ GPL.
No comments:
Post a Comment