Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa
jana alikamatwa na polisi mkoani Geita akituhumiwa kufanya mkutano bila
kibali.
Lowassa, ambaye ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, alikuwa
njiani akitokea mkoani Kagera, ikiwa ni mwendelezo wa ziara za viongozi
wa chama hicho katika kanda zake kutekeleza Operesheni Kata Funua
inayohusisha mikutano ya ndani. Hata hivyo, aliachiwa jana jioni.
Akiwa
ameongozana na viongozi na makada wa Chadema, Lowassa aliingia Geita saa
9:30 alasiri na kupokewa na umati wa wananchi waliojitokeza eneo la
Nyankumbu, tayari kwa safari ya kwenda kwenye mkutano wa hadhara wa
kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani Kata ya Nkome.
Viongozi wengine
waliokuwamo kwenye msafara huo ni Profesa Mwesiga Baregu, ambaye pia ni
mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema na Hamis Mgeja, ambaye ni kada wa chama
hicho.
Msafara huo uliokuwa wa magari matano, ukisindikizwa na pikipiki
na wafuasi kadhaa wa chama hicho, ulipitia makutano ya barabara mjini
Geita na kukutana na magari ya polisi yaliyosheheni askari wakiongozwa
na Kamanda wa Polisi wa Wilaya (OCD), Ally Kitumbo.
Bila kuingilia
msafara huo, magari ya polisi yaliufuatilia kwa nyuma ulipokuwa
ukielekea Kata ya Nkome.
Hali ya hewa ilichafuka baada ya msafara kufika
eneo la Soko Kuu wakati wananchi walipouzuia wakitaka kumsalimia
Lowassa, ambaye aligombea urais katika uchaguzi mkuu uliopita.
Kiongozi
huyo alilazimika kujitokeza juu ya gari lake kuwapungia na baada ya
kelele za ‘njaa, njaa, njaa’ kusikika eneo hilo, Lowassa alitumia kipaza
sauti kuwaomba wananchi wawe watulivu na wawaruhusu waendelee na safari
yao kuwahi mkutano wa kampeni.
“Ndugu zangu wana-Geita, natamani
kuzungumza nanyi lakini sheria inanibana. Naomba muwe watulivu na
mturuhusu tuendelee na msafara kuwahi mkutano wa kampeni Nkome,” alisema
Lowassa.
Askari hao wakiongozwa na OCD, walimfuata Lowassa na
kumuamuru yeye na msafara wake kwenda Kituo Kikuu cha Polisi kwa
mahojiano. Wakati wa kuelekea kituoni, gari lake lilitanguliwa mbele na
la polisi na nyuma kulikuwa na jingine la jeshi hilo.
Kitendo hicho
kiliwafanya wananchi waliokuwa na hamu ya kumsikiliza kiongozi huyo
kuongozana kwenda kituoni, jambo lililoibua taharuki na polisi
kuwatawanya kwa kufyatua mabomu ya machozi.
Waandishi wapigwa
Pamoja na kuwatawanya wananchi kwa mabomu, askari hao pia
waliwapiga kwa mikanda na fimbo waandishi wa habari waliokuwa wakifanya
kazi yao eneo hilo.
Hali ilivyokuwa kituoni
Baada ya kuwasili kituoni
huku polisi wakiendelea kuwazuia wananchi, Lowassa alisalia ndani ya
gari lake hadi hali ilipotulia na kutakiwa kuingia kituoni.
Ni magari
mawili pekee; la Lowassa na la Profesa Baregu, yaliyoruhusiwa kuingia
eneo la polisi huku viongozi wengine kama Singo Benson ambaye ni
Mkurugenzi wa Oganaizesheni na Mafunzo wa Chadema, na Upendo Peneza
(Mbunge wa Viti Maalumu), wakitakiwa kusubiri nje.
Kitendo cha wananchi
kuzidi kufurika kituoni hapo, kiliwafanya polisi kuimarisha ulinzi,
wakizuia mtu yeyote kukatiza wala kusogelea eneo hilo. Licha ya
kuzingira kituo cha polisi, askari walitanda barabara inayoelekea
ofisini kwa Mkuu wa Mkoa wa Geita ambako pia wananchi walizuiwa
kukatiza.
Lowassa apitishwa uani
Baada ya kuona wananchi wanazidi kujaa
kituoni, polisi waliamua kumtoa Lowassa kupitia mlango wa nyuma na
kumhamishia ofisini kwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Mponjoli Mwabulambo.
Kama ilivyokuwa Kituo cha Kikuu cha Polisi, ulinzi pia uliimarishwa
eneo lote la ofisi ya RPC baada ya Lowassa kuhamishiwa huko na wananchi
kupata taarifa.
Kiongozi huyo aliyehamia Chadema akitokea CCM mwaka 2015
aliachiwa jana jioni. Kamanda Mwabulambo alisema hawakumkamata bali
walizuia msafara huo kwa ajili ya usalama wake.
Akizungumzia suala hilo,
Peneza alisema huo ni muendelezo wa ukandamizaji dhidi ya viongozi wa
Chadema unaofanywa na polisi mkoani Geita, akitoa mfano kitendo cha
yeye kuhojiwa kwa saa kadhaa mwishoni mwa wiki iliyopita kwa madai ya
uchochezi alipohutubia mkutano wa hadhara na kusema nchi inakabiliwa na
njaa.
Katiba ya nchi iheshimiwe.
ReplyDelete