WAKAZI wa Mtaa wa Igoma A, Kata ya Isanga Halmashauri ya Jiji la Mbeya, juzi walipata taharuki baada ya kuukuta mwili wa marehemu Harun Kyando (9) aliyefariki dunia na kutoka kumzika ukiwa umebaki chumbani msibani.
Ilielezwa kuwa mtoto huyo alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa kifafa na kwamba alikutwa na wazazi wake asubuhi akiwa amefariki, huku akiwa amelala na mdogo wake ambaye jina lake halikutajwa.
Akizungumza na Nipashe kuhusu mkasa huo jana, rafiki wa baba wa marehemu Ben Chikwamba alisema maiti hiyo ilisahaulika chumbani ilimokuwa ikihifadhiwa baada ya kuoshwa kwa sababu waliopewa jukumu la kwenda kutoa jeneza walikuwa watu tofauti na waliosafisha mwili huo.
Chikwamba alisema maiti hiyo iliwekwa sakafuni kwenye godoro baada ya kuoshwa wakati jeneza lilikuwa juu kitandani.
"Tukiwa tunaelekea makaburini, tuligundua kuwa mkeka umesahaulika ndipo tukamtuma mtu aurudie, lakini katika namna ya ajabu naye alisema hakuona maiti hiyo ilipokuwa imelazwa licha ya kuingia chumbani humo," alisema Chikwamba.
Chikwamba alisema mkeka huo ulitumika kufunika jeneza baada ya kushushwa kaburini na kabla ya kulifukia kwa udongo.
Watu waliohudhuria msiba huo walisema iliamuliwa mwili wa mtoto huyo ukazikwe katika makaburi ya zamani ya Isanga, waombolezaji wakabeba jeneza kwenda kuzika, lakini muda mfupi baada ya kurejea nyumbani wakakuta mwili upo ndani.
Baada ya mwili huo kukutwa ndani, walisema, ndipo yakaibuka malumbano ambapo majirani walihusisha tukio hilo na imani za kishirikina na kutaka kuwapiga wazazi wa mtoto huyo, Jailo Kyando (36) na mkewe Anna Elieza (32) kwa tuhuma hizo.
SIMU POLISI
Hali hiyo, walieleza mashuhuda hao, ilimfanya Mwenyekiti wa Mtaa, Stephano Mwakapeso, kupiga simu Polisi na ndipo maaskari walifika na kuuchukua mwili kuupeleka Hospitali ya Kanda ya Rufani Mbeya kwa ajili ya kuhifadhiwa na kuwachukua wazazi hao kwa ajili ya mahojiano juzi jioni.
Ndipo baadhi ya wakazi wa mtaa huo waliporudi eneo la makaburi hayo kwa lengo la kufukua kaburi la Harun.
Hali hiyo ilipelekea Jeshi la Polisi kuwatawanya kwa kutumia mabomu ya machozi na kutoa taarifa kuwa lingefukuliwa jana baada ya kupata kibali cha mahakama, ili kuthibitisha kilichozikwa.
Jana asubuhi Polisi ilifika eneo la makaburi na kwa kushirikiana na viongozi wa mtaa huo, walisimamia ufukuaji wa kaburi hilo mbele ya mamia ya wananchi wa Kata ya Isanga.
Baada ya vijana wafukuaji kulifikia sanduku hilo, waliamuriwa na askari waliokuwepo kulipandisha juu na kisha kufunua.
Ndipo ilipobainika kuwa hakukuwa na chochote ndani yake.
Hata hivyo licha ya wananchi kuhakikishiwa na Polisi kuwa ni kweli mwili ulikuwa umesahaulika na kutakiwa kwenda kuuchukua kwa ajili ya kuuzika upya, risasi zilifyatuliwa juu baada ya baadhi yao kupiga kelele na kulizonga gari la wana usalama hao lililokuwa limebeba sanduku na wazazi wa marehemu.
Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufani Kanda ya Mbeya, Thomas Isdory ambaye ni Muuguzi Mkuu wa Hospitali hiyo, alikiri kupokea mwili wa mtoto huyo na kukanusha baadhi ya taarifa zilizokuwa zinadai kuwa mtoto huyo alipelekwa akiwa hai.
Alisema kuwa baada ya mwili huo kupokelewa ulipimwa na kuthibitisha kuwa mtoto huyo alikuwa amefariki.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Emmanuel Lukula alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.
Alisema uchunguzi unaendelea ili kubaini endapo mwili huo ulisahaulika kwa uzembe au kuna hujuma zilifanyika dhidi ya familia hiyo.
Ilielezwa msibani hapo kuwa marehemu huyo hakuwahi kupelekwa shule licha ya umri kuruhusu, wazazi wakidai ni kwa sababu ya tatizo la kifafa lililokuwa linamsumbua.
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake