Wanadai kuwa ukaidi wa askofu juu ya uamuzi wa askofu mkuu kumwondoa madarakani ni kukubali athari za kisheria, ambazo zinaweza kutokea kwa Dayosisi na yeye mwenyewe binafsi kwa kuendelea kujipa mamlaka ya askofu wakati akifahamu kuwa mamlaka hayo yameondolewa kwake.
“Sisi waumini wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dayosisi ya Dar es Salaam tunamuunga mkono askofu wetu mkuu kwa uamuzi aliochukua wa kumvua uaskofu Dk Mokiwa na hivyo, tunamwomba mkristo mwenzetu huyu aheshimu uamuzi wa mamlaka yake ya juu ili na wengine waweze kujifunza kwake kama kiongozi,” linasema tamko hilo ambalo lilisomwa jana na Kiongozi wa Walei wa Dayosisi ya Dar es Salaam, Sylvester Haule katika Kanisa la Magomeni.
Haule alisema vitendo vinavyoendelea ndani ya dayosisi hasa baada ya uamuzi wa askofu mkuu, ambavyo baadhi ya makasisi/ mashemasi na wainjilisti wanavifanya pasipo kujua kiini cha tatizo, havina afya na hatima njema kwa dayosisi yao.
“Vitendo hivyo ni utovu wa hali ya juu sana wa nidhamu na viapo vyao vya utii. Sisi kama wakristo, tunazidi kumwomba Mungu awafumbue macho ili waweze kuona nia njema ya Askofu wetu Mkuu ya kuisaidia Dayosisi yetu na Kanisa,” alisema Haule.
Alifafanua kuwa kundi linaloumuunga mkono Dk Mokiwa hadi kushindwa kumheshimu Askofu Mkuu wa Kanisa Angalikana Tanzania, ni uasi wa hali juu dhidi ya mamlaka za juu za kanisa hilo na athari zake zitakuwa kubwa kwa dayosisi hiyo.
“ Kwetu tunaona huu ni uasi wa hali ya juu kutokea ndani ya kanisa letu. Mtu yeyote yule alitarajia kuwa Makasisi au Maaskofu wenye kumjua Mungu vizuri wangesimama nasi katika maombi ya kuliombea kanisa badala ya kuendelea kushindana kulivuruga kanisa,” linasema tamko hilo.
Waumini hao wamesambaza tamko hilo ambalo jana walilisoma katika Kanisa la Anglikana Magomeni kwenda kwa Dk Chimeledya ambaye ni askofu mkuu, wakristo, makanisa yote ya Anglikana Dayosisi ya Dar es Salaam, Msajili wa Vyama vya Kijamii na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA).
Alisema kuwa kikatiba, uaskofu sio ajira na hivyo hata baada ya kuteuliwa, askofu anapewa hati ya uaskofu na sio barua ya ajira kama ilivyo kwa waajiriwa.
Alifafanua kuwa askofu mkuu akitangaza kutomtambua askofu, hiyo inatosha kwa askofu husika kutambua hali yake. Haule alisema athari ya ukaidi wa kutotii mamlaka na kuendelea na jukumu la uaskofu ni pamoja na uwezekano wa mhusika kusababisha dayosisi kutumbukika jimboni na hatima yake kutengwa.
Aliongeza kuwa kwa kuwa Dayosisi ya Dar es Salama ni sehemu ya Kanisa la Angalikana Tanzania na haina katiba au cheti chake cha usajili, masuala mengi ya kisheria yanayohusu mali na madeni ya kanisa yanaweza kuathirika, kwa kuwa kwa kukosa kibali cha Bodi ya Wadhamini.
“Hatua ya kung’anga’ania madaraka kunaweza kusababisha mhusika kushtakiwa kwa kupitisha uamuzi wakati akijua kuwa yeye sio askofu kikatiba,” alisema Haule.
Mokiwa bado halali Mara baada ya Dk Chimeledya kutangaza kumvua uaskofu Dk Mokiwa kutokana na kugoma kujiuzulu kama alivyoshauriwa, Katibu Mkuu wa Dayosisi ya Dar es Salaam, Padri Jonathan Senyagwa alitangaza kuwa hawatambui uamuzi huo kwani umekiuka taratibu za kanisa hilo.
Pia Halmashauri ya Kudumu ya kanisa hilo, imemwandikia Askofu Mkuu Dk Chimeledya na kumweleza kuwa Dk Mokiwa bado ni askofu halali, kwa mujibu wa kanuni na kwamba Dayosisi ya Dar es Salaam haina mgogoro na askofu wake, kama inavyodaiwa na askofu mkuu Tanzania.
Katibu wa Sinodi ya Dar es Salaam, Jerome Napella katika barua yake hiyo alisema kilichopo ni uvamizi wa Dayosisi ya Central Tanganyika inayoongozwa na Dk Chimeledya dhidi ya dayosisi ya Dar es Salaam inayoongozwa na Dk Mokiwa, jambo ambalo linaiumiza dayosisi ya Dar es Salaam.
Nao mashemasi na wainjilisti wa Dayosisi ya Dar es Salaam ambao ni wachungaji wa makanisa 15 yaliyoko ndani ya Dayosisi ya Dar es Salaam, walitoa tamko na kueleza kuwa watu wanaomshutumu Dk Mokiwa, wanapandikiza chuki na uchochezi ndani ya dayosisi yao na kuwataka waache mara moja.
“Sisi mashemasi na wainjilisti tunameshimu na kumtii askofu wa dayosisi yetu ya Dar es Salaam ambaye pia ni Rais wa Baraza la Makanisa barani Afrika.
Harakati zinazoendelea sasa za kuvuruga huduma yake hatuziungi mkono na wala hatuzikubali,” inasema sehemu ya tamko hilo ambalo limesainiwa na wainjilisti 15. Utetezi wa KAT Katibu Mkuu wa Kanisa Anglikana Tanzania (KAT), Mchungaji Chinyong’ole alisema kwamba uongozi wa kanisa hilo, hauna chuki na Dk Mokiwa na taratibu za kumwondoa madarakani zimefuata.
Dk Mokiwa alivyopinga Dk Mokiwa baada ya habari za kung’olewa kwake kutangazwa kwenye vyombo vya habari, aliitisha mkutano na waandishi wa habari na akasema kuwa mgogoro katika dayosisi hiyo ni wa kutengenezwa na hauna uhalisia.
“Mambo mengi ya kutengenezwa, yametengenezwa huko baa Sinza na kusainiwa barabarani humo. Mimi mwenyewe Desemba 18 mwaka juzi niliwaita watu hawa nikae nao lakini walikimbia,” alisema Mokiwa.
Dk Chimeledya akataa malumbano Baada ya kauli ya Dk Mokiwa, Askofu Mkuu Dk Chimeledya alisema hayuko tayari kuendeleza malumbano wala mgogoro. Alisema alishatoa taarifa yake na inatosha.
HABARI LEO
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake