ANGALIA LIVE NEWS

Friday, February 10, 2017

Rais Magufuli akutana na Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akihutubia Mabalozi wanaziwakilisha nchi mbalimbali nchi Tanzania na wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa (hawapo pichani) wakati wa hafla ya kuanza mwaka mpya iliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam
Kutoka kulia ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Augustine Mahiga na Katibu Mkuu wa Wizara Balozi Dkt.Aziz P. Mlima wakifuatilia hotuba ya Mhe. Rais Magufuli 
Sehemu ya Waheshimiwa Mabalozi wakifuatilia hotuba 
Sehemu nyingine ya Waheshimiwa Mabalozi wakifuatilia hotuba 
Hotuba ikiendelea 
Rais Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na Balozi wa China nchini Tanzania Mhe.Lu Youqing 
Rais Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na Balozi wa Kuwait Nchini Tanzania Mhe. Jasem Ibrahim Al Najem 
Rais Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na Mratibu Mkazi wa Mashika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maaendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini Tanzania, Bw. Alvaro Rodriguez 
Rais Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na Balozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia Congo nchini Mhe. Jean Pierre Tshampanga Mutamba 
Rais Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika Balozi Joseph Sokoine kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki 
Rais Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Celestine Mushy 
Rais Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na Mkurugenzi wa Kitengo cha Sheria Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Baraka Luvanda 
Mkuu wa Kitengo cha Mawaliano Serikalini na Msemaji wa Wizara Bi. Mindi Kasiga akizungumza katika hafla hiyo 
Rais Mhe. Dkt. Magufuli na Waziri Mhe. Balozi Dkt. Mhiga wakiwa katika picha ya pamoja na Waheshimiwa Mabalozi 
Rais Mhe. Dkt. Magufuli na Waziri Mhe. Balozi Dkt. Mahiga wakiwa katika picha ya pamoja Wawakilishi wa Mashirika mbalimbali ya Kimataifa nchini Tanzania 
Rais Mhe. Dkt. Magufuli na Waziri Mhe. Balozi Dkt. Mahiga wakiwa katika picha ya pamoja na Watendaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais Magufuli akutana na Mabalozi na wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli amewashukuru Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa kwa ushirikiano na mchango wao kwa Serikali ya Tanzania ambao umesaidia kufikia malengo ya Serikali kwa mwaka uliopita wa 2016. Rais Magufuli aliwasihi Waheshimiwa Mabalozi waendelee kuisaidia Serikali ili kufikia malengo iliyojiwekea kwa mwaka 2017.
Mhe. Rais Magufuli ametoa shukrani hizo leo wakati wa hafla ya kuukaribisha mwaka mpya (Diplomatic Sherry Party) iliyofanyika Ikulu,  Dar es Salaam kati yake, Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa  yaliyopo nchini.
Katika hotuba yake, Mhe. Rais Magufuli alisema kuwa mwaka 2016 ambao ulikuwa mwaka wake wa kwanza tangu achaguliwe kuwa Rais wa Awamu ya Tano umekuwa wa mafanikio makubwa ambapo nchi imendelea kudumisha amani, mshikamano, umoja na Muungano umeimarika. Aidha katika mwaka huo,  Serikali  imeongeza jitihada za kuimarisha demokrasia, kupiga vita rushwa, ujangili na ufisadi.
Mhe. Rais Magufuli aliongeza kusema kuwa, Serikali ya Tanzania imefanikiwa kiuchumi na kuwa nchi ya pili yenye uchumi unaokua kwa kasi barani Afrika ikitanguliwa na Ivory Coast. Uchumi wa Tanzania ulitarajiwa kukua kwa asilimia 7.2 mwaka jana kutoka asilimia 7.0 mwaka uliotangulia. Pia kiwango cha mfumuko wa bei kilipungua kutoka asilimia 6.5 mwezi Januari 2016 hadi kufikia asilimia 2.5 mwezi Oktoba mwaka huohuo.
Akizungumzia suala la ukusanyaji mapato, Mhe. Rais Magufuli alisema kwamba Serikali inasimamia kikamilifu suala hilo ambapo kwa sasa  kiwango cha ukusanyaji wa mapato kimeongezeka kutoka shilingi bilioni 850 hadi kufikia shilingi trilioni 1.2 kwa mwezi.
Kuhusu mpango wa maendeleo wa miaka mitano 2016/2021, Rais Magufuli aliwaeleza Mabalozi hao kuwa, mpango huu unalenga kujenga Uchumi wa Viwanda ili kuiwezesha Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025 kama Dira ya Maendeleo ya Taifa inavyoelekeza.
Alieleza kuwa katika kutekeleza Mpango huo kiasi cha shilingi Trilioni 107 kinahitajika na kati ya hizo  Serikali itatoa shilingi trilioni 59 ambazo ni wastani wa shilingi trilioni 11.8 kila mwaka kwa kipindi cha miaka mitano ijayo. Utekelezaji wa mpango huo umeshaanza ambapo Serikali katika Bajeti yake ya mwaka 2016 imetenga kiasi cha shilingi trilioni 29.5  ambazo ni sawa na asilimia 40 ya Bajeti ya Serikali kwa ajili ya Bajeti ya Maendeleo. Kiwango hicho ni cha juu zaidi kuwahi kutengwa kwenye bajeti ya maendeleo katika historia ya Tanzania.
Fedha hizo zimeelekezwa kwenye ujenzi wa miundombinu wezeshi kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda kama vile nishati, barabara, reli  na maji. Aliongeza kusema kuwa Kati ya fedha hizo shilingi trilioni 5.5 zimetengwa kwa ajili ya miundombinu ya usafirishaji na shilingi trilioni 1.2 zimetengwa kwa ajili ya nishati ya umeme. “Hii imetuwezesha kuendelea au kuanza utekelezaji wa miradi mikubwa ya usafiri ikiwemo reli, barabara, anga, maji pamoja na miradi ya umeme. Tuliweza pia kununua ndege mpya sita ambazo bila shaka zitasaidia kukuza sekta ya utalii nchini”
Kwa muktadha huo, Rais Magufuli aliwaomba Mabalozi kushawishi wawekezaji kuja kuwekeza katika ujenzi wa Reli wa kiwango cha kimataifa kutoka Dar Es Salaam hadi Mwanza na Kigoma na kuunganisha hadi nchi za Burundi, DRC na Rwanda. Serikali kwa kutumia fedha zake za ndani itaanza kujenga kilomita 300 kuanzia Dar  Es Salaam hadi Morogoro.
Vile vile, Serikali imeweka kipaumbele kwenye kuboresha huduma za jamii ikiwemo sekta ya elimu iliyotengewa trilioni 4.8  na sekta ya afya kiasi cha trilioni 1.9. Kupitia mpango huu wa kuboresha sekta ya elimu, kiwango cha udahili kwa watoto wanaojiunga na darasa la kwanza na kidato cha kwanza na wale wanaopokea ufadhili wa masomo ya juu kimeongezeka mara dufu ikilinganishwa na miaka iliyopita.
Akizungumzia masuala ya Diplomasia, Mhe. Rais Magufuli aliwaeleza Mabalozi na Wawakilishi hao wa Mashirika ya Kimatifa kuwa mahusiano ya kidiplomasia kati ya Tanzania na nchi ningine  yameimarika ambapo Viongozi Wakuu kutoka nchi mbalimbali wamefanya ziara nchini Tanzania. Aidha, yeye binafsi, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na Viongozi wengine Serikalini wamefanya ziara za kuimarisha ushirikiano kwenye nchi mbalimbali. Katika ziara hizo, Tanzania imesaini mikataba mbalimbali ya ushirikiano. Mhe. Rais aliahidi kuwa Tanzania itaendelea kuwa mwanachama mwaminifu kwenye Mashirika ya Kimataifa na Kikanda ikiwemo Umoja wa Afrika (AU), Umoja wa Mataifa (UN), Jumuiya ya Madola, Jumuiya ya Afrika Mashariki na mengine.
“Tunawashukuru sana Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa na Kikanda kwa kazi nzuri mnayoifanya hapa nchini kwetu. Mafanikio yote haya niliyoainisha yamewezeshwa na ushirikiano wenu na naahidi Serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwenu ili muweze kufanya kazi zenu vizuri” alisema Rais Magufuli.
Vilevile aliwaomba Mabalozi hao kuendelea kushirikiana na Tanzania ili kuiwezesha kufikia malengo yake na aliwakaribisha wawekezaji kuja kuwekeza nchini na kutumia fursa za malighafi, nguvukazi na soko kubwa lililopo nchini.
Halikadhalika, Mhe. Rais Magufuli alianisha changamoto zinazochangia kukwamisha jitihada mbalimbali za Serikali ikiwa ni pamoja na Mabadiliko ya Tabianchi na kuiomba Jumuiya ya Kimataifa kushirikiana katika kukabiliana na changamoto hii ili kuziwezesha jamii zetu kufikia maendeleo na ustawi. Pia kupitia Mabalozi hao alizipongeza nchi zilizoridhia Mkataba wa Paris kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi na kueleza kuwa Tanzania imeanza mchakato wa kuridhia Mkataba huo tangu mwezi Aprili, 2016.
Katika hatua nyingine, Mhe. Rais aliwaeleza rasmi Mabalozi hao azma ya Serikali ya kuhamishia Makao Makuu mjini Dodoma katika kipindi cha miaka mitano ya utawala wake na kuwaomba Mabalozi hao nao waanze mchakato wa kuhamia Dodoma.
“Mwaka jana wakati nakabidhiwa uenyekiti wa Chama cha Mapinduzi niliahidi ndani ya miaka mitano Serikali itahamia Dodoma. Tayari Waziri Mkuu na baadhi ya Wizara zipo Dodoma. Nawaomba Mabalozi nanyi muanze kufikiria kuhamia Dodoma kwani Serikali imekwishatenga viwanja kwa ajili yenu, alisisitiza Rais Magufuli.
Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Mabalozi ambaye pia ni Balozi wa Zimbabwe hapa nchini, Mhe. Edzai Chimonyo alisema kuwa anaipongeza Serikali ya Tanzania chini ya uongozi wa Rais Magufuli kwa hatua kubwa  ya maendeleo iliyopiga katika kipindi cha mwaka mmoja wa utawala wake. Alisema kuwa katika kipindi hiki wameshuhudia uchumi ukikua, nidhamu katika utumishi wa umma, ukusanyaji wa mapato kuongezeka, na kiwango cha mfumuko wa bei kupungua.
Aidha, aliongeza kuwa wanaunga mkono mpango wa Serikali wa kujenga miundombinu wezeshi ikiwemo Reli kwa vile kutawezesha kukuza biashara na nchi jirani na mataifa mengine kwa ujumla. Pia alipongeza jitihada za Serikali katika kukuza ushirikiano na Sekta Binafsi ambayo ina mchango mkubwa kwenye maendeleo na kupongeza juhudi za Tanzania kwenye usuluhishi wa migogoro kwenye Ukanda wa Maziwa Makuu na kuitaja Tanzania kuwa ni Kisiwa cha Amani.
Kuhusu Mabalozi kuhamia Dodoma, Balozi Chimonyo alisema Jumuiya ya Mabalozi inaunga mkono wazo hilo na wapo tayari kuhamia Dodoma kama ilivyopangwa.
                                                             -Mwisho-
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,

Dar es Salaam, 10 Februari, 2017

1 comment:

Anonymous said...

Mbona JPM anazungumza kiswahili wakati mabalozi wote hawana translator ina maana mabalozi wote wanajua kiswahili. Nchi nyingine wakuu wao wanazungumza lugha zao lakini wanakuwa na translator hivyo wageni hawaachwi nyuma, mnalionaje hilo wadau.